Utangulizi

Ili uweze kupata miche bora ya mpunga kwa ajili ya kupanda shambani ni lazima kwanza uwe na mbegu bora, pili uandae kitalu bora na mwisho uitunze miche wakati wote iwapo kitaluni.


Uandaaji Wa Mbegu Bora Ya Mpunga Kabla Ya Kupanda

Kabla ya kupanda, mbegu ya mpunga inabidi iandaliwe vizuri. Shughuli zote zinazofanyika katika maandalizi hayo zinalenga kuirahisishia mbegu kuota kwa kiwango kinachotakiwa ili mkulima aweze kupata miche bora ya kupandikiza baadaye.

Ili mbegu iote vizuri inahitaji unyevu wa kutosha, joto la kutosha na hewa ya kutosha. Lengo hasa la matayarisho haya ni kuhakikisha kuwa mbegu ya mpunga imepata unyevu, joto na hewa ya kutosha kuota (kuchipua) kwa ulinganifu.

Utayarishaji wa mbegu una hatua kuu tatu: kuondoa mapepe na uchafu mwingine, kuloweka na kuatamisha mbegu. Soma hapa kujua aina bora ya mbegu ya mpunga.


Kuchagua Mbegu Bora (Kuondoa Mapepe)

Lengo la kuchagua mbegu ni kuondoa mapepe ili kupata mbegu iliyojaa vizuri.

Njia za kuondoa mapepe

 • Kupeta kutumia ungo au upepo
 • Kupembua kwa maji safi yasiyo na chumvi
 • Kupembua kwa maji ya chumvi (ya bahari au yaliyochang’anywa na chumvi ya jikoni)

Njia ya kupembua kwa maji yaliyochang’anywa na chumvi ni bora zaidi kwani huondoa kiasi kikubwa cha mapepe ambayo hayawezi kuondolewa kwa kupeta au kwa kutumia maji yasiyo ya chumvi. Mbegu inayobakia ni nzuri sana ambayo itatoa miche mizuri zaidi kitaluni.


Soma makala hizi;


Kupembua mbegu ya mpunga kwa maji yaliyochang’anywa na chumvi

Mahitaji

 • Mbegu yenye mapepe
 • Chombo cha kupembulia (ndoo, sufuria n.k.)
 • Maji safi (lita 10)
 • Chumvi (kilo 1.5)
 • Chombo cha kuwekea mbegu iliyopembuliwa
 • Kijiti cha kukorogea

Jinsi ya kufanya

 1. Chang’anya maji (lita 10) na chumvi (kilo 1.5) kwenye chombo cha kupembulia na ukoroge kwa kijiti mpaka chumvi yote iyeyuke. (Hatua hii haihitajiki iwapo maji ya bahari yatatumika).
 2. Weka mbegu yenye mapepe katika mchang’anyiko wa maji na chumvi.
 3. Koroga kwa kijiti kwa muda wa kama dakika moja kisha acha maji yatulie na mapepe yaelee juu ya maji
 4. Engua mapepe na uyatupe
 5. Rudia hatua (3) na (4) uhakikishe kuwa mapepe yote yameondolewa
 6. Mwaga maji ya chumvi na uoshe mbegu kwa maji safi kuondoa masalia ya chumvi kwenye mbegu.
 7. Kausha mbegu kwa matumizi ya baadaye au loweka mbegu kwa ajili ya kuatamisha mara baada ya kupembua.

Kuloweka Mbegu Ya Mpunga

Lengo lake ni kuiwezesha mbegu kunyonya unyevu wa kutosha.

Mahitaji

 • Mbegu safi (iliyopembuliwa)
 • Chombo cha kulowekea (ndoo, mtungi, pipa n.k.)
 • Maji safi
 • Chombo cha kuwekea mbegu iliyolowana
 • Dawa ya kuzuia magonjwa (kama inapatikana)

Jinsi ya kufanya

 1. Pima mbegu ya kuloweka
 2. (Kiasi cha mbegu hutegemea ukubwa wa shamba, kilo 30-40 hutosha hekta moja au kilo 12-16 kwa ekari moja)
 3. Weka kiasi cha maji kinachofunika mbegu vizuri kwenye chombo cha kulowekea.   
 4. Kama dawa ya kuzuia magonjwa inabidi itumike, chang’anya vizuri na maji kabla ya kuweka mbegu.
 5. Zamisha mbegu kwenye maji na iache kwenye maji kwa muda wa masaa 24 – 48.

Usiache kusoma makala hizi;


Kuatamisha Mbegu Ya Mpunga

Lengo lake ni kuiwezesha mbegu kupata joto na hewa ya kutosha ili iweze kuchipua vizuri.

Mahitaji

 • Mbegu iliyolowekwa kwa muda wa kutosha
 • Magunia mawili yasiyo na mbegu  zingine za mpunga au uchafu mwingine
 • Mifuko inayopitisha maji na hewa (hiari)
 • Kichanja  kifupi

Jinsi ya kufanya

 1. Lowesha magunia ya kuatamishia mbegu
 2. Tandaza gunia lenye unyevu juu ya kichanja penye kivuli
 3. Toa mbegu kwenye maji na kuziosha vizuri (mara 2 au 3)
 4. Tandaza mbegu kwenye kichanja. Mbegu zikiwa chache, ziweke kwenye mfuko wa kuatamishia na uufunge vizuri ukiacha nafasi ya kutosha kuzitawanya kwenye tabaka lenye unene usiozidi sentimeta 5. Weka mfuko kwenye gunia juu ya chanja na zitawanye inavyowezekana. Kwa mbegu nyingi, weka kwenye gunia juu ya chanja moja kwa moja na sambaza vizuri kwenye tabaka lenye unene usiozidi sentimeta 5.
 5. Funika mbegu kwa gunia jingine lenye unyevu
 6. Geuza mbegu hizo mara kwa mara ili zipate hewa ya kutosha na kuota kwa ulinganifu. Zikionyesha kupoteza unyevu, zinyunyizie maji kiasi.
 7. Pima joto (kwa mkono au kipima joto) mara kwa mara na kuhakikisha joto la kawaida (nyuzi joto 20 hadi 30 za sentigredi)
 8. Atamisha kwa muda mpaka mbegu ichipue (masaa 24 – 48).

Angalizo (kumbuka):

Ni muhimu kuzingatia muda wa kuatamisha mbegu na kuzichunguza mara kwa mara. Muda wa kuatamisha ukiwa mfupi, mbegu itaota vikonyo vifupi tu (bila mizizi kutokeza). Muda wa kuatamisha ukizidi, uotaji utazidi, mizizi inakuwa mirefu na kujikunja. Hii ina sababisha mizizi kukatika wakati wa kusia mbegu kwenye kitalu.


Uandaaji Wa Kitalu Cha Mbegu ya Mpunga

Vitalu ni sehemu ambayo miche ya mimea huzalishwa kwa ajili ya kupandwa baadaye shambani. Vitalu huandaliwa ili kupata miche yenye siha iliyolingana. Kitalu kinapaswa kiandaliwe karibu na shamba (kuepuka mwendo mrefu wa kusafirisha miche), panapopatikana maji (kwa urahisi wa kumwagilia) na sehemu yenye mwanga wa kutosha ili miche isidhoofike kwa kukosa mwanga.

Vitalu bora zaidi ni vitalu tepetepe, yaani vitalu ambavyo hustawishwa sehemu yenye maji mengi na kwa muda mrefu huwa vimelowana. Ubora wa vitalu hivi unatokana na kwamba:

 • Mbegu kidogo hutumika kwa ajili ya kupanda shamba kubwa
 • Miche huwa na kimo na siha vinavyolingana
 • Miche huota kwa pamoja na kukua haraka
 • Ni rahisi kudhibiti magugu, magonjwa na wadudu waharibifu
 • Ni rahisi kung’oa miche kwa kupandikiza bila kuiumiza

Mahitaji

 • Kamba
 • Pegi (mambo) za kutosha
 • Kifaa cha kusawazishia
 • Jembe
 • Chombo cha kupimia begu

Jinsi ya kufanya

 • Safisha vizuri eneo la kutengeneza kitalu
 • Lima/tifua vizuri na lainisha udongo
 • Ondoa takataka zote
 • Acha udongo utulie kwa muda wa kama siku moja
 • Udongo ukiishatulia weka mipaka ya kila kitalu (upana meta 1-1.5 na urefu kutegemea urefu wa shamba)
 • Kama vinahitajika vitalu zaidi ya kimoja acha nafasi ya sentimeta zisizopungua 50 kati ya kitalu kimoja na kingine
 • Inua kitalu kwa kuchukua udongo/tope kutoka kwenye nafasi kati ya vitalu na kuuweka juu ya bapa la kitalu (Nafasi iliyotolewa udongo itatumika kama njia ya kupitishia maji ya kumwagilia, kutolea maji ya ziada na kupitia wakati wa kuhudumia vitalu)
 • Sawazisha vema kitalu na lainisha udongo wa juu.
 • Tawanya (sia) mbegu kwa uwiano mzuri juu ya bapa la kitalu, mbegu zisirundikane sehemu moja. Mbegu zisizidi gramu 100 (kiganja kimoja) kwa meta moja ya mraba
 • Pigapiga mbegu polepole kwa kutumia viganja vya mikono ili mbegu iingie kwenye kina kifupi ndani ya udongo. (Hii husaidia mbegu zishikane vizuri na udongo, zisiliwe na wanyama au ndege).

Utunzaji Wa Kitalu Cha Mbegu ya Mpunga

Lengo ni kupata miche yenye siha na inayolingana, kwa wakati ufaao kupandikiza. Miche yenye siha hutoa mizizi haraka na hutoa machipukizi mengi na yenye nguvu siku chache baada ya kupandikiza.


Kitalu bora cha mbegu ya mpunga
Kitalu bora cha mbegu ya Mpunga

Sifa za miche mizuri

 • Mifupi na minene kiasi (yenye podo la jani lenye urefu wa sentimeta 2-5)
 • Yenye majani mafupi, yaliyosimama, mapana kiasi na yenye nguvu
 • Yenye mizizi mingi na yenye nguvu
 • Isio na magonjwa au wadudu ili isichelewe kuota mizizi
 • Yenye kimo na unene unaolingana au kukaribiana sana

Uangalizi wa kina cha maji (Au mahali inapowezekana kumwagilia)

 • Baada ya kusia, kitalu kiwe na unyevu tu kwa muda wa siku kama 3 hivi, maji yasionekane juu ya uso wa kitalu.
 • Kuanzia siku ya 4 hadi 8 baada ya kusia, kina cha maji juu ya uso wa kitalu kiwe chini ya sentimeta 5 (kama urefu wa pingili ya juu ya dole gumba). Wakati huu miche inakuwa na majani yasiyopungua mawili.
 • Baada ya siku 8 kina cha maji kiongezwe lakini kisizidi sentimeta 5 (urefu wa dole gumba). Kiasi hiki kiwepo shambani hadi siku ya kung’oa miche.
 • Siku ya kung’oa miche kina cha maji kiongezwe hata kufikia sentimeta 10 ili kurahisisha ung’oaji na uoshaji wa miche tayari kwa kupandikizwa.

Kuweka mbolea ya kukuzia:

 • Kama miche inaonekana ya rangi ya kijani na yenye afya wiki moja (kwa mpunga wa muda mfupi) au wiki mbili (kwa mpunga wa muda wa wastani) baada ya kuota, hakuna haja ya kuweka mbolea ya kukuzia.
 • Kama miche inaonekana ya njano-njano kwa muda uliotajwa hapo juu, weka mbolea za kukuzia (mfano Urea au salfeti ya ammonia (SA) kutegemea kiwango cha sehemu inayohusika. Kama viwango husika havipo, ongeza walau gramu 8 za Urea au 16 za SA kwenye meta moja ya eneo.
 • Wakati wa kuweka mbolea hakikisha udongo una unyevu wa kutosha kuyeyusha mbolea (Mwagilia au weka mbolea muda mfupi kabla ya mvua kunyesha).
 • Tawanya mbolea kwa ulinganifu kwenye sehemu yote ya kitalu. Katika kipindi cha baridi, mbolea ya kukuzia iwekwe mapema zaidi kuishtua mimea isisinzie, ikue haraka.

Kuzuia au Kuondoa Magugu, Magonjwa na Wadudu

 • Kama magugu yakionekana shambani ni vizuri yaondolewe mara (kwa kupalilia) ili yasinyonye rutuba ya udongo, na kwa kuepuka kuyapandikiza shambani baadaye.
 • Wadudu wanaoharibu miche ya mpunga wakionekana wauawe kwa njia salama inavyowezekana.
 • Magonjwa yanayotibika yatibiwe kwa dawa zinazofaa. Miche iliyoshambuliwa na magonjwa yasoyotibika ing’olewe mapema na kufukiwa mbali na kitalu. Soma hapa matumizi sahihi ya viuatilifu.
 • Eneo lote la kitalu na mazingira yake lisafishwe kila mara kuondoa maficho ya wadudu, magonjwa na wanyama waharibifu (mfano panya). Soma hapa namna ya kudhibiti panya.

Baada ya kufahamu namna ya kuandaa na kutunza kitalu cha mbegu ya mpunga, sasa soma hapa jinsi ya kuandaa kitalu cha miche ya mbogamboga.

5 1 vote
Article Rating

Mtalula Mohamed

I like blogging. In order utilize my profession I chose to share, to blog, a few tips and tricks about farming and agriculture to anyone interested.

Subscribe
Notify of
guest
18 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Peter kulwa
Peter kulwa
1 year ago

Asante kwa mawazo mazuri unasaidia sana

Bertha L juma
Bertha L juma
1 year ago

Asant kwa elimu nzur

Kayanja
Kayanja
1 year ago

Jambo zuri sana, endelea kutuelimisha

Mohamed Mtalula
Mohamed Mtalula
Reply to  Kayanja
10 months ago

Shukrani sana, endelea kuwa nasi.

pat
pat
10 months ago

sasa kwa heka moja unaweza pata mpunga kiasi gaaaaaan???

Mohamed Mtalula
Mohamed Mtalula
Reply to  pat
10 months ago

Tumeeleza kwenye makala hii, tafadhali isome hapa: https://www.mogriculture.com/2017/03/kilimo-cha-mpunga/

pat
pat
10 months ago

unaweza pata mpunga kias gan kwa heka moja

Mohamed Mtalula
Mohamed Mtalula
Reply to  pat
10 months ago

Tumeeleza kwenye makala hii, tafadhali isome hapa: https://www.mogriculture.com/2017/03/kilimo-cha-mpunga/

Shacks Chagalu
Shacks Chagalu
8 months ago

Tunashukuru kwa elimu ya kilimo mnayo tupa,walau tunaongeza upeo na tija kwa vile tusivyo fahamu.

Mtalula Mohamed
Mtalula Mohamed
Reply to  Shacks Chagalu
1 month ago

karibu sana, na endelea kuwa nasi

Last edited 1 month ago by Mtalula Mohamed
salum igoye
salum igoye
8 months ago

mbegu kwenye kitalu huchukua mda gan kupandwa shambani

Mtalula Mohamed
Mtalula Mohamed
Reply to  salum igoye
1 month ago

Mbegu ya mpunga ipandwe ikifikisha siku 21. [Katika usimamizi mzuri] unaweza kupanda hata kuanzia siku 14 tu

ndisha Joseph
ndisha Joseph
6 months ago

nimeipenda Sana kazi yako, Mimi ni mkulima wa mpunga asante Sana kwa msaada huo MUNGU akubariki usife moyo endelea kutusaidia.

Mtalula Mohamed
Mtalula Mohamed
Reply to  ndisha Joseph
1 month ago

Shukran sana kwa kunipa moyo

Emmanuel shau
Emmanuel shau
4 months ago

Asante naomba unitumie kwenye email yangu immashau@gmail.com

error: Content is protected !!
18
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x

Join Our Farming Community