vitunguu saumu vizima na punje zake baada ya kuvunjwa 02

Kilimo cha vitunguu saumu Tanzania: Uzalishaji, Masoko na Faida

Kilimo cha vitunguu saumu nchini Tanzania kinapata umaarufu kwa kasi kama biashara ya kilimo yenye matumaini, kutokana na ongezeko kubwa la mahitaji ya ndani na katika soko la kimataifa. Vitunguu saumu, kwa harufu na ladha yake kali na ya kipekee, uwezo wake kitiba, na kutumika kwake katika matumizi mbalimbali ya mapishi, vimejipatia nafasi muhimu katika majiko ya kaya nyingi za Kitanzania. Umaarufu wake haujaja tu kwa bahati, bali ni ushahidi wa matumizi yake lukuki na faida zake nyingi za kiafya.

Hali mbalimbali za hewa na udongo wenye rutuba nchini Tanzania hutoa mazingira bora kwa kilimo cha vitunguu saumu. Kuanzia milima ya kijani ya Arusha na Kilimanjaro hadi tambarare za Morogoro na Singida, maeneo mbalimbali ya kijiografia ya nchi yetu yanachangia katika ukuaji wa zao hili muhimu. Kila eneo lina faida za kipekee; iwe ni baridi kali la milimani linalonenepesha punje na kuzipa ladha yake ya ukali au udongo wenye rutuba usiotuamisha maji unaostawisha na kuleta tija kwenye vitunguu saumu.

vitunguu saumu vizima na punje zake baada ya kuvunjwa 01
Picha 1: Vitunguu saumu vizima (bulbs) na punje (cloves) zake.

Kwenye makala hii, tutaangalia mambo muhimu kwenye  kilimo cha vitunguu saumu nchini Tanzania, na kutoa mwongozo kamili kwa wakulima wenye uzoefu na wale wapya kwenye uwanja huu. Tutazidadavua mada muhimu kama vile kuchagua aina za vitunguu saumu zinazofaa kwa eneo lako, kutekeleza mbinu bora za kilimo, na kugusia mienendo ya soko la vitunguu saumu.

Ukielewa misingi hii, utakuwa na maarifa ya kutosha kufanikiwa katika kilimo cha vitunguu saumu, kukidhi mahitaji ya soko, na hatimaye kuchangia kwenye ukuaji wa sekta ya vitunguu saumu nchini.

Uwe mkulima mzoefu anayetaka kuangazia fursa kwenye mazao mengine au mkulima mpya anayetaka kuanza safari ya kilimo, kitabu hiki kinalenga kukupa maarifa ya msingi na mwongozo wa vitendo utakaohitaji ili kufanikiwa katika kilimo cha vitunguu saumu. Ambatana nasi tunapoibua fursa na changamoto kwenye kilimo hiki, na uone jinsi utakavyoweza kuifanya kuwa biashara yenye faida na mafanikio.

Mahitaji ya Kiikolojia

Hali ya hewa na maji/mvua

Vitunguu saumu vinapendelea hali ya joto la kati ya nyuzi 12 – 24 za sentigredi. Wastani wa mm 500 – 600 za mvua zinatosha kwa msimu wote wa uzalishaji.

Unyevu anga na/au mvua nyingi sana huvutia magonjwa ya ukungu. Kwa mantiki hii vitunguu saumu vinafaa zaidi kulimwa katika maeneo yoyote ambayo yanamvua chache na uhakika wa maji ya kumwagilia.

Udongo na Mwinuko

Vitunguu saumu hupendelea udongo wenye rutuba usiotuamisha maji na wenye pH ya kati ya 5.5 – 7.5. Vitunguu saumu vinapendelea maeneo yenye miinuko ya kati ya mita 1000 hadi 2500 kutoka usawa wa bahari.

Udongo wa tifutifu kichanga (sandy loam) unafaa zaidi kwa vitunguu saumu kwa kuwa unapitisha hewa vizuri na hautuamishi maji. Udongo wa mfinyanzi mzito hauruhusu vitunguu kujitanua na hutunza maji kwa muda mrefu sana hivyo kuozesha vitunguu.

Mikoa inayolima vitunguu saumu Tanzania

Kwa hapa Tanzania vitunguu saumu vinalimwa zaidi katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Manyara, Arusha, na Kilimanjaro. Mikoa mingine ni Morogoro (Mgeta) na Singida. Maeneo ya nyanda za juu yana miinuko stahiki , hali ya hewa ya baridi na mtawanyiko mzuri wa mvua (vitu) ambavyo huchagiza sana ustawi wa vitunguu saumu hasa vya hardneck.

Uchaguzi wa mbegu bora, upandaji na
utunzaji wa vitunguu saumu

Mbegu za vitunguu saumu

Vitunguu saumu vipo vya aina mbili: Vitunguu saumu vya shingo laini (soft-neck garlic) na Vitunguu saumu vya shingo ngumu (hard-neck garlic). Aina hizi zote zinalimwa hapa nchini.

Vitunguu saumu vya shingo laini (Soft-neck Garlic)

Hivi ni vitunguu saumu ambavyo shina lake au shingo yake ni laini na ina tabia ya kuanguka (au kulala) vitunguu vinapokomaa. Shina la vitunguu hivi huwa ni laini hata baada ya vitunguu kuvunwa na inaweza kusokotwa kama kamba. Dalili ya kukomaa vitunguu hivi ni kulala au kuanguka kwa shina lake.

Mfano wa vitunguu saumu vya shingo laini ni Egyptian white garlic na Chinese white garlic.

Sifa za vitunguu saumu vya shingo laini

  • Shingo yake ni laini kiasi kwamba inaweza kukunjwa au kusokotwa kama kamba.
  • Vina punje (cloves) ndogondogo nyingi (12 – 25) zilizopangwa katika safu nyingi ndani ya tunguu (bulb). Kutokana na uwingi wa punje, matunguu (bulbs) yake ni makubwa kuliko ya hardneck.
  • Vina ladha na harufu yenye ukali wa wastani, inayofaa kwa matumizi ya kawaida ya nyumbani. Ladha yake ni laini kuliko ile ya vitunguu saumu vya shingo ngumu.
  • Ni rahisi kulima na vinahifadhika kwa muda mrefu zaidi: kati ya miezi 10 hadi 12.
  • Vinastawi katika maeneo yenye hali za hewa mbalimbali, kuanzia baridi hadi joto la wastani, na vinaweza kupandwa katika maeneo ya kitropiki na uwanda wa kati.

Vitunguu saumu vya shingo ngumu (Hard-neck Garlic)

Hivi ni vitunguu ambavyo shina lake (au shingo yake) ni ngumu kama mti na hubakia imesima hata vitunguu saumu vinapokomaa. Dalili ya kukomaa kwa aina hii ni majani kubadilika rangi kuwa kahawia na kuanza kukauka.

Mfano wa vitunguu saumu vya shingo ngumu ni mexican purple garlic.

Sifa za vitunguu saumu vya shingo ngumu

  • Vitunguu saumu vya hardneck hutoa shina linaloitwa scape. Shina hilo linaanzia kwenye kitako cha kitunguu na kupanda hadi kwenye shingo, na hivyo kuvipa jina la “hard-neck – shingo ngumu”. Shingo yake ni ngumu na hubaki imesimama kama mti, na hutoa maua kwa juu.
  • Vina punje (cloves) chache kubwa (4 – 12) zilizopangwa katika mduara mmoja ndani ya tunguu (bulb) kuzunguka shingo ngumu (scape). Matunguu yake ni madogo kuliko ya softneck.
  • Vina ladha na harufu kali zaidi inayopendwa na wapishi wengi.
  • Ni vigumu kulima na vinahifadhika kwa muda mfupi zaidi: kati ya miezi 4 hadi 8.
  • Vinapendelea zaidi katika maeneo yenye baridi kali, na hivyo kustawi vizuri zaidi maeneo ya nyanda za juu. Hali hii ya baridi ndio hufanya vitengeneze punje (cloves) nene zenye ladha na harufu kali.

Elephant Garlic

Elephant garlic sio vitunguu saumu halisi. Ni aina ya vitunguu (allium) ambavyo kimuundo vinafanana sana na vitunguu saumu. Vinatengeneza matunguu (bulbs) yenye punje (cloves) chache nene sana, na matunguu (bulbs) yake ni makubwa kuzidi yale ya vitunguu saumu.

Licha ya kuwa vinafanana (karibu kila kitu) na vitunguu saumu, elephant garlic ni aina (species) tofauti kabisa. Hivi vipo kwenye kundi la jamii ya vitunguu vinavyoitwa leeks. Vitunguu hivi vipo kwenye species ya Allium ampeloprasum wakati vitunguu saumu vipo katika species ya Allium sativum. Sijui kama Elepahant garlic vinalimwa hapa nchini (nifahamishe kama unajua), ninachojua huwa vinaingizwa kutoka nje.

uwiano wa punje za elephant garlic na vitunguu saumu vya kawaida
Picha 3: Punje (cloves) za elephant garlic (kushoto) na punje na kitunguu saumu cha kawaida (kulia)

Jinsi ya kuandaa mbegu ya vitunguu saumu

  • Tambua ewe mkulima ya kuwa mbegu ya vitunguu saumu haiuzwi kwenye maduka ya pembejeo za kilimo (angalau) kwa sasa, hivyo ukitaka mbegu ni lazima ukanunue kwa mkulima au mzalishaji wa vitunguu saumu.
  • Ukishanunua, kama umenunua vitunguu vilivyo kauka vizuri, chambua na uondoe udongo, mizizi na (ngozi au) maganda yaliyokauka ambayo yapo loose.
  • Kama havijakauka vizuri basi visambaze mahali penye  mzunguko mzuri wa hewa na kivuli au pasipo fikiwa na jua la moja kwa moja kwa muda wa wiki mbili. Usianike vitunguu saumu juani kama mahindi au vitunguu maji.
  • Utakapotaka kupanda, vunjavunja vitunguu saumu ili upate punje au vidole (cloves) kimoja kimoja kutoka kwenye matunguu kama ambavyo unachambua unapotaka kumenya kwa ajili ya mapishi. Usimenye ngozi ya vidole vyake, acha vibaki na ngozi yake vile vile. Ona picha hapa chini.
  • Kumbuka kuwa hizo punje au vidole ya vitunguu saumu (cloves) ndio mbegu tutakayoipanda shambani. Usivunje vitunguu vyako kama bado hujajiandaa kupanda, kwa sababu vitaoza ikiwa utavisubirisha kwa muda kiasi.
  • Wakati wa kupanda chagua punje za  vitunguu saumu (cloves) nene kwani ndizo zitakazokupa vitunguu vikubwa. Ukipanda punje nyembamba tambua kuwa utazalisha vitunguu chenga chenga.
punje za vitunguu saumu baada ya kuvunja vunja matunguu
Picha 4: Mbegu za vitunguu saumu

Jinsi ya kupanda vitunguu saumu

Msimu wa vitunguu saumu

Vitunguu saumu hupandwa kuanzia mwezi March hadi May. Kipindi ni kizuri kwa kuwa vitunguu saumu vinapata muda wa kujenga mizizi yake kabla ya kipindi cha joto kuanza. Lakini pia unaweza kupanda kati ya mwezi Oktoba na Desemba wakati wa mvua za vuli.

Kama unategemea mvua, muda wa kupanda iwe ni wakati wa mvua za mwanzo. Na kama unaweza kumwagilia unaweza kupanda kuanzania mwezi May.

Sasa unaweza kujipatia Kitabu (PDF) cha Mwongozo wa kilimo cha Vitunguu Saumu sasa hivi kwa bei nafuu sana. Kitabu hiki kimeboreshwa zaidi kwa ushauri wa kitaalam, mapendekezo ya kiasi, na aina za mbegu bora, mbolea na viuatilifu vya kutumia pamoja na mchanganuo wa bajeti ya kilimo na faida. Bofya hapa kukipata ndani ya Whatsapp au bofya hapa kukipata kwa email.

Maandalizi ya shamba

  • Andaa shamba lako mapema kabla ya muda wa kupanda.
  • Shamba bora liwe halijalimwa jamii yoyote ya vitunguu kwa angalau misimu mitatu iliyopita. Mazao jamii ya vitunguu (Alliums) ni vitunguu maji (A. cepa), vitunguu saumu (A. sativum) na leeks (A. ampeloprasum).
  • Safisha shamba lako na utifue udongo kwa kina cha sm 15 – 20. Piga halo kuhakikisha udongo wote ni laini na hakuna mabonge ya udongo yaliyobaki.
  • Sawazisha shamba lako ili kuondoa maeneo yote ya kutuamisha maji (lower spots).
  • Andaa shamba kulingana na mfumo wa umwagiliaji utakao utumia. Tengeneza mifereji na majaluba ikiwa utatumia umwagiliaji wa mifereji.
  • Tengeneza matuta ambamo juu yake utapanda vitunguu ikiwa utatumia umwagiliaji wa matone.
  • Weka samadi kiasi cha tani 15 kwa ekari moja.

Upandaji wa vitunguu saumu

Kiasi cha mbegu: Kg 200 – 300 za vitunguu saumu zinatosha kwa ekari moja. Hii itakupa kiasi cha kilogram 180 – 200 za punje za vitunguu saumu baada ya kuvunjavunja.

Mbolea ya kupandia: Weka kg 80 za mbolea ya DAP au TSP. Ichanganye vizuri na udongo na hakikisha haigusani na vitunguu.

Nafasi ya kupandia: Panda kwa nafasi ya sm 15 x sm 30. Nafasi kati ya mashimo ndani ya mstari ni sm 15 na nafasi kati ya mstari mmoja na mwingine ni sm 30. Kina kiwe kati ya sm 2 – 3 kwenda chini. Panda mbegu moja katika kila shimo.

Hatua za kupanda Vitunguu saumu…

  • Mwagilia shamba lako angalau siku moja kabla ya siku ya kupanda. Au mwagilia mara tu baada ya kupanda kama hukumwagilia mwanzo.
  • Chagua punje nene za vitunguu saumu (cloves) ndio uzitumie kama mbegu. Usichukue vipunje vidogo-vidogo. Ukubwa wa vitunguu vyako utategemea ukubwa wa punje utakazopanda.
  • Chimba mashimo ya kupandia kwa nafasi na kina tulichoeleza hapo juu; sm 15 x 30 na sm 2 – 3 kwenda chini.
  • Weka punje moja ya kitunguu saumu kwenye kila shimo, huku upande wa mizizi utangulie chini na upande uliochongoka uangalie juu kisha fukia kwa udongo laini.
  • Fanya hivyo mpaka utakapo maliza kupanda shamba lako lote.
upandaji wa vitunguu saumu bustanini
Picha 5: Upandaji wa vitunguu saumu bustanini

Umwagiliaji wa vitunguu saumu

Mmea wa vitunguu saumu una mfumo wa mizizi michache na mifupi sana kwa hivyo, unakuwa mwepesi kuathirika kutokana na ukosefu wa maji wakati wote wa msimu wa ukuaji.

Kinapotokea kipindi chochote cha ukame kwenye udongo, hasa wakati wa kukomaa kwa vitunguu, kitasababisha kupungua kwa mavuno. Kwa hiyo ni muhimu sana kuhakikisha kuwa vitunguu saumu vinapata maji kila vinapohitaji ili kujihakikishia mavuno mazuri.

Unaweza kumwagilia vitunguu saumu kwa njia ya mifereji (furrow irrigation), matone (drip irrigation) au kwa sprinkla.

shamba la vitunguu saumu vilivyoota vizuri
Picha 6: Bustani ya vitunguu saumu iliyoota vizuri

Kuweka matandazo: kufunika uso wa udongo kwa kutumia majani au vifaa vingine ili kuhifadhi unyevu wa udongo na kupunguza uotaji magugu ni muhimu. Njia hii pia inaweza kuwa na ufanisi katika kudhibiti ugonjwa wa kutu kwani matandazo yanaweza kulinda udongo kutokana na matone ya mvua yanayodondoka.

Athari za magugu na jinsi ya kuyadhibiti

Athari za magugu shambani

Magugu ni hatari sana shambani kwa sababu hushindania maji, mwanga na virutubisho dhidi ya vitunguu saumu. Na kwa kuwa vitunguu saumu vina mizizi michache na mifupi, katika ushindani huu vyenyewe huwa ndio wahanga zaidi na magugu hushinda.

Athari ya magugu kwenye shamba la vitunguu saumu ni kama ifuatavyo…

  • Kupunguza ubora na mavuno ya vitunguu saumu kutokana na kushindwa kugombea mahitaji muhimu katika ukuaji wake.
  • Kuongezeka kwa maambukizi ya wadudu na magonjwa. Hii inatokana na baadhi ya magugu kuhifadhi visumbufu hivi vya mazao.
  • Kuongeza gharama za utunzaji kama vile vibarua wa palizi na viutilifu.
  • Kukwamisha zoezi la uvunaji ikiwa magugu yataachwa mpaka wakati wa kuvuna vitunguu saumu.

Sasa ili kuepuka athari hizi, zifuatazo ni njia za kudhibiti magugu kwenye shamba la vitunguu saumu.

Jinsi ya kudhibiti Magugu

(a) Palizi kwa Jembe la Mkono

Inapotokea shamba lako limezidiwa na magugu, au baada ya dawa kufanyakazi na baadhi ya magugu kubaki, palizi kwa kutumia vijembe vidogo vya mkono au kung’olea kwa kutumia mikono huwa ndio suluhisho pekee kuokoa vitunguu vyako.

Palizi ifanyike baada ya vitunguu saumu kuchipua ili kuepuka kuving’oa kwa bahati mbaya.

  • Palizi ya Kwanza: Wiki 1 hadi 2 baada ya miche kuchipua.
  • Palizi ya Pili: Wiki 4 hadi 6 baada ya miche kuchipua.
vitunguu saumu vimestawi shambani
Picha 7: Shamba safi la vitunguu maji lisilo na magugu

(b) Palizi kwa Kutumia Viuagugu

Ikiwa magugu yataendelea kuota unaweza kupiga dawa za kuulia magugu zinazochagua magugu (selective herbicides) na kuacha vitunguu kama vile Sufen au Oxfen. Viuatilifu hivi vinaufanisi zaidi kwa magugu machanga hivyo zingatia hatua ya ukuaji wa magugu kabla ya kupiga.

Angalizo: Zingatia kanuni bora za matumizi ya viuatilifu kama vile kusoma vibandiko vya kwenye vifungashio, kutumia vipimo vilivyo pendekezwa na kutumia zana za kujikinga wakati wakutumia viuatilifu hivi.

Mahitaji ya mbolea za vitunguu saumu

Mbolea za kupandia vitunguu saumu

Tunashauri mbolea za kupandia vitunguu ziwe na kirutubishi cha phosphorous. Mbolea kama DAP na TSP zinafaa zaidi kupandia. Tumia kiasi cha mfuko mmoja na nusu (kg 75) wa DAP au TSP kwa ekari moja.

Mbolea hii iwekwe kwenye mifereji au mashimo ya kupandia lakini hakikisha haigusani moja kwa moja na vitunguu wakati wa kupanda.

Ukipata samadi au mbolea ya mboji, weka tani 15 na uichanganye vizuri na udongo. Unapoitumia samadi hakikisha unaiweka kwanza shambani kabla hujapanda ili uichanganye wakati wa kupiga halo.

Mbolea za kukuzia vitunguu saumu

Mara tu baada ya vitunguu kuchipua weka mbolea ya CAN kiasi cha kg 75 kwa ekari. Mwezi mmoja baadae weka mbolea ya NPK kiasi cha kg 100 kwa ekari, na baada ya mwezi mmoja mwingine weka mbolea ya MOP (Muriate of Potash) kg 50 au  (ukikosa, weka) NPK kiasi cha kg 75 kwa ekari.

Uwekaji wa mbolea: mbolea zote za kukuzia ziwekwe kwa juu (top dressing) kwa kuzitawanya kwa usawa (broadcasting) kama umepanda kwenye majaluba au kwa sesa. Na weka kwa usawa  pembezoni mwa mistari ya vitunguu (basal application) kama umepanda kwenye matuta.

Mwagilia mara tu baada ya kuweka mbolea isipokuwa tu kama unatumia umwagiliaji wa mifereji ambapo  utatakiwa kumwagilia kwanza kabla ya kuweka mbolea. Hii ni muhimu sana ili kuhakikisha mbolea yote inafyonzwa na mimea haraka iwezekanavyo.

shamba la vitunguu saumu vilivyostawi
Picha 8: Shamba la vitunguu saumu lililostawi vizuri

Utambuzi na Udhibiti wa Magonjwa na Wadudu waharibifu wa vitunguu saumu

Mbinu shirikishi za udhibiti wa wadudu na magonjwa kwenye vitunguu saumu 

 Uwezo wako wa kununua na kutumia viuatilifu isiwe sababu ya kuwa mzembe na kuacha shamba lako lishambuliwe na wadudu na magonjwa. Matumizi ya viuatilifu yanatakiwa kuwa ni njia ya mwisho katika jitihada zako za kupambana na visumbufu.

Yafuatayo ni baadhi ya mambo unayotakiwa kuyafanya ili kupunguza kasi ya mashambulizi ya wadudu na magonjwa shambani kwako …

  • Fanya mzunguko wa mazao kwenye shamba lako. Usirudie kulima vitunguu saumu kwenye shamba ulilolima msimu uliopita.
  • Chagua na panda mbegu zenye afya na zisizo na maambukizi ya wadudu wala magonjwa. Chagua punje nene zilizojazia.
  • Tibu mbegu kabla ya kupanda dhidi ya wadudu wa ardhini na fangasi. Hii itakusaidia kuepuka mashambulizi ya mwanzoni kabisa.
  • Weka nafasi ya kutosha kati ya mimea ili kuboresha mzunguko wa hewa na kupunguza unyevunyevu.
  • Hakikisha shamba lako halina magugu na ni safi muda wote. Magugu huwapa hifadhi wadudu ambao baadae huja kushambilia mazao yako.
  • Epuka kutuamisha maji shambani wala kukausha shamba kwa muda mrefu sana. Maji mengi shambani au ukavu kupitiliza huipa stress mimea, kitu ambacho hupunguza uwezo wa mimea kujilinda dhidi ya wadudu na magonjwa vamizi.
  • Ukimwagilia shamba lako; epuka kumwagilia maji kutokea juu (mfano kwa sprinkler), na usimwagilie jioni sana. Vitendo hivyo huchochea kutokea kwa magonjwa ya fangasi / ukungu. Badala yake mwagilia asubuhi ili maji yakauke kabla ya kuingia usiku.
  • Epuka kuweka mbolea za naitrojeni kwa wingi hasa katika hatua za mwishoni mwa uzalishaji, kwani mbolea nyingi za naitrojeni katika hatua hiyo huvutia mashambulizi ya wadudu na magonjwa ya fangasi.
  • Chunguza shamba lako mara kwa mara kuangalia uwepo wa magonjwa au wadudu, na uchukue hatua stahiki mapema sana.
  • Usiache mabaki ya mimea ya vitunguu saumu shambani, yakusanye na uyachome ili kuepuka kutunza vimelea vya magonjwa mpaka msimu ujao.
  • Nyakati za mvua nyingi na joto kali, jihami dhidi ya magonjwa ya fangasi kwa kupulizia viuatilifu vya kujilinda kama vile vyenye viambata vya mancozeb hata kama hujashambuliwa.
  • Wakati wa udhibiti wa visumbufu shambani, epuka kutumia viuatilifu vya aina moja kila wakati kwani baadhi ya visumbufu hujitengenezea usugu; yaani uwezo wa kujilinda na kutodhurika na sumu waliyoizoea.

Magonjwa ya vitunguu saumu

(i) Uozo mweupe (White Rot)

Ugonjwa wa uozo mweupe unasababishwa na fangasi aitwaye Sclerotium cepivorum. Huu ni ugonjwa mbaya zaidi wa vitunguu saumu, mara nyingi unaweza kuangamiza mimea yote shambani au katika sehemu ya shamba. Fangasi huyu huzalisha sclerotia ambazo zinaweza kubaki kwenye udongo kwa miaka mingi.

Ugonjwa wa muozo mweupe hukua vizuri katika udongo wenye unyevu mwingi na unaweza kuendelea kuwa hai kwa muda mrefu, hivyo kufanya ugonjwa huu kuwa mgumu kudhibiti.

Dalili

Juu ya Ardhi: Katika hatua za mwanzo, muozo mweupe ni vigumu kutofautisha na magonjwa mengine. Dalili zake ni pamoja na udumavu wa mimea, majani ya nje kuanza kuwa ya njano na kufa kwanza, kisha majani mengine na shina kuu kufa pia. Hatimaye, shina juu ya kitunguu saumu huanza kuoza.

Chini ya Ardhi: Fangasi husababisha kuoza kwa kitunguu na mizizi inayozunguka. Sehemu zilizoathirika huwa laini na kuoza, jambo ambalo hupelekea kifo cha mmea.

Athari kwa mazao

Muozo mweupe husababisha hasara kubwa za mazao kutokana na kuharibika kabisa kwa vitunguu. Hii husababisha kupungua kwa mavuno na mara nyingi inahitaji kuanza upya katika eneo tofauti.

Njia za kudhibiti

  • Usiachie mabaki ya vitunguu saumu shambani; kusanya na utupe mabaki vizuri, ikiwezekana kwa kuyachoma. Epuka kutengeneza mbolea ya mabaki ya mimea ya vitunguu saumu.
  • Tumia mimea kama haradali, ambayo hufanya kazi kama dawa za kiasili za kufukiza udongo na husaidia kudhibiti vijidudu vya udongo huku ikijenga rutuba kwenye udongo.
  • Tumia viuakuvu vyenye kiambata cha tebuconazole, Iprodione, au Fludioxonil mfano Folicure EC 250, Tebufarm 25WP, Rovral 250Flo (/~500Flo). Pulizia kwenye shimo wakati wa kupanda, na kwa mimea mikubwa pulizia kwenye udongo ifike kwenye mizizi.

(ii) Ubwiri vinyoya (Downy mildew)

Ubwiri vinyoya unasababishwa na fangasi aitwaye Peronospora destructor. Huathiri vitunguu saumu na mimea mingine ya jamii ya allium, kama vile vitunguu na leeks. Ugonjwa huu hukua vizuri katika hali ya baridi na unyevunyevu, na unakua vizuri zaidi katika joto la takriban 24°C.

Ubwiri vinyoya husambaa kwenye hali ya baridi na mvua, ikiwa ni pamoja na umande mzito, ukungu, na hali ya hewa ya mvua. Inapendelewa na joto la wastani na unyevunyevu unaozidi kwenye kivuli cha majani.

Dalili za ugonjwa

Majani: Madoa ya rangi ya kijivu, yenye umbo la mstatili hadi urefu wa milimita 3, ambayo yanaweza kuwa na rangi ya zambarau au kujaa maji. Madoa haya mara nyingi huwa na ukungu wa rangi ya kijivu au nyeupe chini ya majani. Majani yanaweza kuwa ya njano, kushindwakusimama wima, na hatimaye kufa.

Vitunguu (bulbs): Vitunguu vilivyoathirika vinaweza kuwa vidogo, kunyauka, na kubadilika rangi. Vinaweza kutengeneza maeneo laini yenye maji, hasa karibu na shingo. Vitunguu vilivyoathirika vinaweza pia kuchipua mapema au kukauka, huku ukungu wa kijivu au sclerotia nyeusi vikionekana kati ya magamba.

Athari kwa mazao

Ukungu unaweza kusababisha upotevu mkubwa wa mavuno na ubora wa vitunguu kutokana na kufa kwa majani na kuoza kwa vitunguu (bulbs). Hii huathiri ustawi wa mazao na ubora wa uhifadhi.

Njia za kudhibiti ugonjwa

  • Chagua mbegu za vitunguu (bulbs) na punje (cloves) safi na zenye afya.
  • Tumia viuakuvu vyenye Chlorothalonil na mancozeb kama vile Farmerzeb, Dithane M-45, DKzeb, Ridomil gold 68WG, Linconil, n.k.
  • Epuka kumwagilia maji kupita kiasi, kupanda mimea kwa ukaribu karibu sana, na hakikisha udongo hautuamishi maji.
  • Ondoa magugu, mabaki ya mazao na sehemu za mimea zilizoathirika.

(iii) Baka zambarau (Purple Blotch)

Baka zambarau husababishwa na fangasi aitwaye Alternaria porri. Ugonjwa huu huathiri vitunguu saumu na mimea mingine ya jamii ya allium, kama vile vitunguu, leeks, na chives. Ugonjwa huu unakua vizuri katika hali ya joto na unyevu, na ni tatizo kubwa katika mazingira hayo.

Baka zambarau hukua haraka katika hali ya joto na unyevunyevu. Dalili zinaweza kuonekana ndani ya siku 1–4 baada ya kuambukizwa, hali inayotegemea msimu, muda wa kupanda, na hatua ya ukuaji wa mmea.

purple blotch on garlic
Picha 10: Ugonjwa wa Baka zambarau kama unavyoonekana kwenye majani ya vitunguu

Dalili za ugonjwa

Majani: Angalia vidonda vidogo vilivyobonyea na vilivyojaa maji kwenye majani ya zamani ambavyo hubadilika kuwa rangi ya zambarau hadi kahawia, mara nyingi vikiwa na miduara ya njano. Vidonda hivi vinaweza kupanuka, kuvuka na kuua jani. Majani yaliyoathirika yanaweza kuwa ya njano-kahawia, kushindwa kusimama wima, na hatimaye kunyauka.

Vitunguu (bulbs): Vitunguu vilivyoathirika vinaweza kupata maeneo laini yaliyojaa maji, hasa karibu na majeraha ya shingo yaliyotokana na ung’oaji. Maeneo haya yanaweza kuwa na ngozi nyembamba, na vitunguu vinaweza kuwa na rangi ya zambarau nyekundu giza au kahawia/nyeusi.

Athari kwa mazao

Baka zambarau linaweza kuharibu vitunguu saumu vibaya kwa kusababisha majani kunyauka na kuoza kwa vitunguu. Hii husababisha kupungua kwa mavuno na ubora, jambo ambalo linaathiri uwezo wake kuuzika sokoni.

Njia za kudhibiti ugonjwa

  • Tibu mbegu kwa kutumia mafuta ya mwarobaini, mafuta ya nyonyo, mafuta ya karafuu, au Trichoderma viride. Loweka mbegu kwenye mchanganyiko kwa dakika 25–30, kisha ziache zikauke kwa dakika 15 kabla ya kupanda.
  • Tumia viuakuvu kama vile Xantho 5EC, Korovil, Indazole, DKzeb, Nyotaz, Sevenstar 240EC, n.k.

(iv) Kutu (Rust – Puccinia allii)

Ugonjwa wa Kutu husababishwa na fangasi aitwaye Puccinia allii. Ni ugonjwa unaoenezwa kwa njia ya hewa kutoka kwenye mabaki ya mimea iliyoambukizwa, kama vile mabaki ya mazao na maotea. Hali zenye unyevuanga mwingi, kama zile zinazopatikana katika mazingira ya pwani au wakati wa mvua nyingi, zinafaa kwa ukuaji wa ugonjwa huu.

Kutu inakua vizuri katika mazingira yenye unyevu mwingi na mzunguko hafifu wa hewa. Ugonjwa huu huenea kwa kasi katika hali ya hewa ya mvua na joto.

garlic rust
Picha 11: Athari za ugonjwa wa Kutu kwenye vitunguu saumu

Dalili za ugonjwa

Dalili za awali ni madoa madogo meupe ya mviringo (yanayo refuka) kwenye majani na mashina. Ugonjwa unapoendelea, madoa haya hubadilika kuwa vidonda vya rangi ya machungwa vilivyo mduara mrefu. Maambukizi makubwa husababisha majani kuwa ya njano, kunyauka, na kukauka. Vitunguu vinaweza kuwa vidogo na vyenye ubora duni.

Athari kwa mazao

Kutu husababisha uharibifu mkubwa kwa kupunguza utendaji wa majani, hali inayopunguza usanisinuru (photosynthesis). Hii husababisha vitunguu kuwa vidogo na vya ubora wa chini, na kupungua mavuno kwa ujumla.

Njia za kudhibiti ugonjwa

  • Panda vitunguu saumu kwenye eneo lenye jua na mzunguko mzuri wa hewa, pamoja na udongo unaopitisha maji vizuri. Epuka kumwagilia moja kwa moja juu ya mimea.
  • Ondoa na uharibu sehemu zilizoambukizwa za mimea, ikiwa ni pamoja na majani na vitunguu (bulbs). Ikiwa mimea imeambukizwa vibaya, fikiria kuiharibu ili kuzuia kuenea zaidi.
  • Tumia viuakuvu venye propiconazole kama vile Molgard 25EC, Bayleton 250EC, Rustall 375EC. Tumia viuakuvu vyenye Sulphur na Copper kama njia ya kuzuia au mara tu dalili za awali zinapoonekana.

(v) Muozo fusari wa vitunguu

Muozo Fusari wa vitunguu upo wa aina mbili na zote husababishwa na fangasi wa Fusariamu. Aina ya kwanza ni Muozo Fusari wa vitunguu (bulb rot) ambayo husababishwa na Fusarium proliferatum. Na aina ya pili ni Muozo Fusari wa Kitako (basal rot) ambayo husababishwa na Fusarium culmorum na Fusarium oxysporum. Fangasi hawa hupatikana ardhini na wanaweza kuishi kwenye aina mbalimbali za udongo.

Fangasi wa Fusariamu hukua vizuri katika hali ya joto na unyevu mwingi. Fangasi hawa ni maarufu katika aina mbalimbali za udongo na wanaweza kuishi kwa muda mrefu.

Dalili za ugonjwa

Muozo Fusari wa Kitako (basal rot): Hushambulia kutokea chini ya kitunguu (bulb), na kusababisha vidonda vilivyo na mipaka ya rangi nyekundu. Ugonjwa huu unaendelea polepole na hauna sclerotia kama kwenye muozo mweupe.

Muozo Fusari wa Vitunguu (bulb rot): Husababisha vidonda vya rangi ya kahawia vinavyoonekana kama maji juu ya vitunguu (bulbs). Upande wa chini wa kitunguu hauathiriki sana. Tofauti na muozo mweupe, ugonjwa huu hauna sclerotia.

fusarium basal rot
Picha 12: Athari ya ugonjwa wa fusarium basal rot

Athari kwa mazao

Aina zote mbili za Muozo Fusari  husababisha kupungua kwa ubora na mavuno ya vitunguu saumu. Basal rot hushambulia vitunguu kutoka chini kuelekea juu, wakati bulb rot husababisha kuoza na madoa kwenye punje za vitunguu saumu (cloves).

Njia za kudhibiti ugonjwa

  • Tumia vitunguu imara na vyenye afya kwa kupanda. Hakikisha udongo unapitisha maji vizuri na epuka unyevu wa kupita kiasi. Weka mifereji ya kutolea maji.
  • Ondoa na uharibu mimea iliyoathirika ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa.
  • Tumia viuakuvu kama vile Nativo 300SC, Pearl 500SC, Innovex 600SC, nk.

(vi) Muozo shingo wa Botrytis

Muozo shingo wa Botrytishusababishwa na fangasi Botrytis porri. Ugonjwa huu huathiri sana sana vitunguu saumu, na kusababisha hasara kubwa.

Ugonjwa huu hustawi katika mazingira yenye unyevunyevu mwingi na joto la wastani. Huonekana kwa mara ya kwanza wakati wa kifuku au majira ya mapema ya kiangazi, hasa katika hali za unyevu.

botrytis neck rot
Picha 13: Athari za ugonjwa wa Muozo shingo wa Botrytis

Dalili zake

Shingo na Vitunguu (bulbs): Kwanza, shingo inayoonekana kama imejaa maji huanza kuharibika karibu na usawa wa udongo. Fangasi husambaa chini kuelekea kwenye vitunguu (bulbs), na kushambulia sehemu ya ndani huku sehemu ya nje ya kitunguu ikiwa haionyeshi dalili yoyote mwanzoni. Baada ya kukausha, vitunguu vilivyoathirika huonyesha rangi kali ya zambarau na kuoza kwa ngozi za nje, wakati ngozi za ndani zinakuwa ngumu, za kahawia, au nyeusi.

Uhifadhi: Wakati wa uhifadhi, ugonjwa huu unaweza kusababisha ukungu wa kijivu na sclerotia kubwa nyeusi, tofauti na sclerotia ndogo inayopatikana kwenye uozo mweupe.

Athari kwa mazao

Muozo shingo wa Botrytis husababisha uharibifu mkubwa kwa vitunguu, ikisababisha kushuka kwa ubora na mavuno. Ugonjwa huu unaweza kuendelea wakati wa uhifadhi, na kuathiri zaidi vitunguu na kusababisha hasara za kiuchumi.

Njia za kudhibiti ugonjwa

  • Weka nafasi ya kutosha kati ya mimea ili kuboresha mzunguko wa hewa na kupunguza unyevunyevu.
  • Epuka kumwagilia maji kupita kiasi na matumizi ya nitrogen mwishoni mwa msimu, ambayo inaweza kuzidisha ugonjwa.
  • Tumia viuakuvu vyenye chlorothalonil kama Twigathalonil 500SC, Linconil, Dithane M-45, nk.
  • Hakikisha vitunguu saumu vinakauka vizuri na kuwe na mzunguko mzuri wa hewa ili kuepusha mashambulizi zaidi wakati wa uhifadhi.

Wadudu waharibifu wa vitunguu saumu

(i) Vidomozi (Leaf miners)

Vidomozi ni nzi wadogo waliopo kwenye genus ya Liriomyza, ambapo lava wao (mabuu) hula kwa ndani ya majani ya vitunguu saumu, wakisababisha njia au vifereji vilivyopinda pinda. Wadudu kamili (adults) ni nzi wadogo wenye rangi nyeusi (urefu wa mm 2-3), na majike hutaga mayai kwenye kuta za majani.

Mabuu yanapototolewa, hula na kutengeneza mashimo ndani ya majani kabla ya kuanguka kwenye udongo ili kukomaa. Mzunguko wa maisha yao unachukua takriban wiki mbili katika hali ya hewa ya joto, na hivyo kufanikisha vizazi vingi ndani ya msimu mmoja.

garlic leafminer pupae
Picha 14: Mabuu wa vidomozi wakiwa kwenye vitunguu

Dalili za uwepo wa vidomozi

  • Mashimo yanayoonekana kwenye majani: Njia zinazojipinda au madoa kwenye majani kutokana na ulaji wa mabuu.
  • Majani yaliyoathirika yanageuka rangi ya njano, na baadhi ya maeneo yanakufa.
  • Maambukizi makali husababisha ukuaji dhaifu wa mimea na vitunguu saumu vidogo.
  • Majani yanaweza kunyauka na kufa mapema.

Madhara ya vidomozi kwa vitunguu saumu

  • Majani yaliyoathiriwa hupunguza uwezo wa utengenezaji wa chakula, hivyo kupunguza ukuaji.
  • Mimea iliyodumaa husababisha vitunguu saumu kutoa chenga chenga, na hivyo kupunguza mavuno kwa ujumla.
  • Kuongezeka kwa hatari ya magonjwa kwa kuanzisha njia za maambukizi ya pili kutoka kwa fangasi au bakteria.

Mbinu za Kudhibiti vidomozi

  • Lima kwa kubadilisha mazao kila msimu ili kuharibu mzunguko wa maisha wa vidomozi.
  • Weka wadudu wa asili wanaoangamiza vidomozi kama nyigu wa Diglyphus isaea.
  • Tumia dawa za wadudu zenye kuchagua kama Abanil 18EC, Dudu Acelamectin 5%EC, Spidex 215EC, n.k
  • Epuka dawa za wadudu zenye wigo mpana ili kulinda wadudu marafiki ikiwa utataka kuwatumia.

(ii) Vithiripi (Thrips)

Vithiripi ni wadudu wadogo, wenye miili myembamba, wenye urefu wa karibu 1/12 hadi 1/16 ya inchi. Rangi yao inaweza kutofautiana kutoka njano hadi giza. Wadudu wazima wana mabawa madogo yenye vinywele pembeni, huku hatua za ukuaji za awali zikiwa hazina mabawa.

Tabia za ulaji

Vithiripi, hasa Thrips tabaci, hula kwa kukata tishu za mimea na kufyonza utomvu. Wanapatikana sana kwenye sehemu zenye majani mengi, hasa kwenye ncha za majani, na kusababisha uharibifu mkubwa.

Mzunguko wa maisha yao

Vithiripi wanaweza kukamilisha mzunguko wao wa maisha kutoka yai hadi mdudu kamili ndani ya wiki 2 kulingana na joto. Wanaweza kutoa hadi vizazi 8 kwa mwaka. Wakati wa majira ya baridi, wanaishi kwenye mashamba ya kunde, nafaka, sehemu zenye magugu, na kwenye mabaki ya vitunguu.

onion thrips
Picha 15: Vithiripi wakiwa kwenye majani ya vitunguu

Dalili za uwepo wao

Majani: Uwepo wa michirizi myeupe au ya fedha kwenye majani. Majani yaliyoharibika yanaweza kunyauka, kudondoka, au kufa. Mavi: Madoa meusi kwenye majani kutokana na kinyesi cha vithiripi.

Athari kwa mazao

Vithiripi husababisha uharibifu mkubwa kwa mimea ya vitunguu kwa kunyonya utomvu, na kusababisha majani kunyauka na kufa. Pia wanaweza kusambaza magonjwa ya virusi, na kuhatarisha afya ya mimea.

Njia za Kudhibiti wadudu hawa

  • Hakikisha shamba lina unyevu wa kutosha na epuka matumizi ya ziada ya mbolea yenye nitrojeni, kwani kiwango kikubwa cha nitrojeni huvutia zaidi vithiripi.
  • Dhibiti magugu ili kupunguza sehemu za kuishi wadudu hawa.
  • Fuatilia kwa ukaribu idadi ya vithiripi; vithiripi 15 kwa mmea mmoja ni kiwango cha tahadhari, na unatakiwa kuanza kudhibiti.
  • Tumia viuatilifu kama Attakan 350SC, Ninjaplus, Profecron, Duduba 450EC, n.k.

(iii) Utitiri mwekundu (Tetranychus urticae)

Utitiri mwekundu ni wadudu kutoka familia ya Tetranychidae, ambayo ina spishi karibu 1,200. Wanafamalia wa subclass ya Acari la Class ya Arachnida.

Utitiri mwekundu (Tetranychus urticae) ni mdudu mdogo, mwenye miguu minane, akihusiana kwa karibu na buibui. Majike wana rangi nyekundu na wana jozi minne za miguu, wakati madume yana rangi ya shaba. Mara nyingi hawaonekani hadi wanapojenga makoloni makubwa na kutoa utando wa wavu.

Tabia za ulaji: Utitiri mwekundu hunyonya utomvu wa mimea, na kusababisha uharibifu mkubwa kwa mimea ya vitunguu saumu.

Dalili za uwepo wao

  • Mabadiliko ya Majani: Majani ya vitunguu hubadilika kuwa magumu, manene yaliyojazia, na kuonyesha rangi ya njano-kahawia, kana kwamba yameungua nyuma.
  • Majani huwa na vishimo vidogo vya rangi nyeupe vilivyotokana na ulaji wao.
  • Mimea kudumaa: Maambukizi makubwa yanaweza kusababisha mimea ya vitunguu kudumaa.
red spider mite tetranychidae
Picha 17: Utitiri mwekundu kwenye shina la mmea

Athari kwa mazao

Uharibifu: Utitiri mwekundu husababisha uharibifu mkubwa, ikiwa ni pamoja na kuharibika kwa majani na kudumaa kwa mimea ya vitunguu.

Kupungua kwa Mazao: Maambukizi hupunguza ukuaji wa mimea na hatimaye kusababisha kupungua kwa mavuno na ubora wa vitunguu.

Njia za kudhibiti wadudu hawa

  • Weka Phytoseiulus, utitiri mdogo, usio na madhara, unakula utitiri mwekundu na Neoseiulus californicus, aina ya utitiri unaowinda utitiri katika mazao mbalimbali.
  • Chunguza mimea mara kwa mara kuona dalili za awali za maambukizi na tumia mikakati ya usimamizi wa wadudu jumuishi ili kudhibiti idadi ya utitiri.
  • Tumia viuatilifu kama Abanil 18EC, Bamic 20EC, Agromectin 1.8EC, n.k. Pia unaweza kutumia poda ya Sulphur (2.5 kg/ha).
  • Utitiri mwekundu unaweza kuwa na upinzani dhidi ya dawa za kemikali, hivyo udhibiti wa kibiolojia na mbinu mbadala ni muhimu kwa usimamizi bora.

(iv) Utitiri wa vitunguu (Bulb Mites)

Utitiri wa vitunguu (bulb mites) wapo katika familia ya Acaridae. Utitiri wa vitunguu ni wadogo, weupe wa maziwa wenye miguu ya kahawia, wenye urefu wa kati ya 0.02–0.04 inchi. Mara nyingi wanaonekana wakiwa wameshikana kwenye sehemu ya chini ya mizizi ya vitunguu au sehemu zilizoharibiwa.

bulb mites
Picha 16: Athari za utitiri kwenye punje za vitunguu saumu

Tabia za ulaji

Utitiri wa vitunguu hula bulb za vitunguu, wakisababisha uharibifu shambani na wakati wa uhifadhi. Wanatoboa vitunguu na kuruhusu vijidudu vya magonjwa kuingia.

Dalili za uwepo wao

  • Kukauka: Mimea ya vitunguu inaweza kuonyesha dalili za kukauka kwa ujumla, huku ncha za majani zikibadilika kuwa kahawia.
  • Alama za ulaji: Ngozi ya nje ya kitunguu kuwa na alama za kuliwa.
  • Kutengana kwa bamba la chini: Bamba la chini kujitenga kwa urahisi kutoka kwenye kitunguu.

Athari kwa mazao

Uharibifu shambani: Katika shamba, utitiri wa vitunguu unaweza kusababisha mimea kuwa dhaifu na kudumaa mwanzoni mwa msimu.

Wakati wa kuhifadhi: Wakati wa kuhifadhi, vitunguu vinaweza kuwa vyepesi, vinabonyea kwa urahisi, na kuwa na rangi ya njano-kahawia vikimenywa. Majeraha ya midomo yao yanaweza kusababisha kuoza kwa vitunguu na maambukizi ya fangasi.

Njia za kudhibiti wadudu hawa

  • Loweka punje za vitunguu saumu (kabla ya kupanda) kwenye maji ya moto (540C) kwa dakika 10 – 20. Au loweka kwenye maji yenye sabuni na mafuta ya taa au ya transformer (mineral oil) masaa 24 kabla ya kupanda.
  • Chovya punje za mbegu ya vitunguu kwenye mchanganyiko wa sulphur na kiuatilifu chenye dimethoate (kama vile Dudu-ethoate) kabla ya kupanda.
  • Safisha na uondoe mabaki ya mimea ya vitunguu kwa kuyachoma au kutupa mbali. Epuka kuacha mabaki shambani.
  • Weka wadudu rafiki kama ladybugs, lacewings, na nyigu wa kuparasi (parasitic wasps) kwa ajili ya kudhibiti idadi ya utitiri.
  • Tumia viuatilifu kama Profecron 720EC, Atom 2.5EC, Agro-zinon 60EC, Nogozone 60EC, n.k.

(v) Nematodi wa shina na kitunguu (Bloat Nematode)

Nematodi ni minyoo midogo sana, wasioonekana kwa macho bila kutumia darubini. Ditylenchus dipsaci ni nematodi husika anayesababisha kuoza kwa shina na kitunguu katika vitunguu.

stem and bulb nematode
Picha 14: Athari za ugonjwa wa Bloat Nematode

Tabia za ulaji

Nematodi hawa hula sehemu za ndani za vitunguu (bulb), wakisababisha uharibifu mkubwa. Wanaingia ndani ya kitunguu na wanaweza kusababisha maambukizi ya pili kutoka kwa fangasi na bakteria. Nematodi wa mizizi (Pratylenchus sp.), ingawa hawaingii kwenye kitunguu, hushambulia mizizi na kusababisha udumavu.

Mzunguko wa maisha na hatua ya uharibifu

Mzunguko wa maisha wa nematodi unahusisha mayai, lava, na mnyoo kamili (adult nematode). Hatua hatari zaidi ni nematodi kamili (adult nematode), ambao hula tishu za mimea. Wanastawi katika hali ya joto na unyevunyevu, na huonekana wakileta uharibifu mkubwa wakati wa hali hizo.

Dalili za uwepo wao

Majani: Majani ya vitunguu saumu kujikunja na kubadilika muonekano.

Vitunguu: Vitunguu vinaweza kubadilika kuwa vya kahawia, kupasuka, na kuvimba (bloat). Ngozi ya nje inaweza kupasuka na kujitenga na sehemu ya chini ya kitunguu.

Uchunguzi wa Nematodi: Uchunguzi wa kimaabara unahitajika kuthibitisha uwepo wa nematodi. Tumia mbinu za kuchukua sampuli ya udongo na vitunguu ili kuchunguza maambukizi.

Athari kwa mazao

Mimea ya vitunguu iliyoathiriwa na nematodi wa shina na vitunguu (bulb) inaonyesha kudumaa na kupunguza mavuno. Vitunguu huanza kuoza, na inaweza kusababisha maambukizi ya pili na kupunguza ubora wa mazao kwa ujumla.

Njia za kudhibiti wadudu hawa

  • Panda mbegu zilizokomaa, safi na zenye afya. Mbegu hizo zinatakiwa zisiwe na maambukizi ya vimelea vya wadudu au magonjwa yoyote. Hii ni nguzo muhimu sana ya udhibiti wa wadudu hawa.
  • Fanya mzunguko wa mazao na uzingatie usafi mzuri wa shamba ili kupunguza idadi ya nematodi. Epuka kupanda vitunguu saumu kwenye mashamba yaliyowahi kuathiriwa na nematodi.
  • Ondoa na uharibu mimea iliyoathiriwa na epuka kutumia zana au vifaa vilivyoambukizwa.
  • Panda mimea ya kufunika udongo kama vile haradali kwenye mashamba yasiyotumika kwa vitunguu. Haradali husaidia kuboresha udongo na kutumika kama kifukizaji cha asili dhidi ya nematodi.

Uvunaji na masoko ya vitunguu saumu

Uvunaji wa vitunguu saumu

Maandalizi ya kuvuna

Vitunguu saumu huwa tayari kuvunwa miezi 4 mpaka 6 tangu kupanda kutegemeana na hali ya hewa. Ni muhimu kujua muda sahihi wa kuvuna kwa sababu ukivuna vitunguu ambavyo havijakomaa huwa vinanyauka vinapokaushwa.

Na ukichelewa kuvuna baada ya kukomaa utasababisha vitunguu kuwa na madoa, kupoteza mizizi na maganda (wrapper) ya matunguu (bulbs) kuoza hali inayosababisha punje za vitunguu kupasuka kutokana na kushambuliwa na ukungu mweusi.

Zifuatazo ni dalili zitakazokuonesha kuwa vitunguu saumu vimekomaa…

  • Majani ya vitunguu saumu kubadilika rangi kutoka kijani kwenda njano na kwenda kaki au kukauka majani ya chini. Hii ni dalili muhimu sana kwa vitunguu saumu vya hard-neck.
  • Shingo ya vitunguu saumu kuanza kuanguka na/au kulala usawa wa ardhi. Hii ni dalili muhimu sana kwa vitunguu saumu vya soft-neck.
  • Ng’oa vitunguu vichache na uangalie matunguu; vunja tunguu uone punje zake, kama zimegawanyika vizuri basi vitunguu vimekomaa na unaweza kuvuna.
  • Fanya uchunguzi mapema na ukishagundua kuwa vitunguu vimekomaa sitisha umwagiliaji wiki mbili au tatu kabla ya siku ya kuvuna.

Jinsi ya kuvuna Vitunguu saumu

Kwa vitunguu saumu vilivyopandwa kwenye udongo mwepesi, vuna kwa kung’oa kwa mkono. Ikiwa udongo ni mzito zaidi au vitunguu vilipandwa kwa kina kirefu, tumia uma kwa uangalifu kung’oa mmea kama ulivyo.

Tingisha kidogo ili kuondoa udongo uliozidi. Usipigize vitunguu kwa vitunguu au kwa kitu kingine chochote ili kuondoa udongo kwani kufanya hivyo kutaviponda na kufanya viwahi kuharibika vitakapohifadhiwa.

shamba la vitunguu saumu uvunaji
Picha 18: Uvunaji wa vitunguu saumu ukiendelea shambani

Ukaushaji wa Vitunguu saumu

Vitunguu saumu sio kama vitunguu maji, vinatofautiana sana mchakato wake mpaka kuingia sokoni.

Baada ya kuvuna, vitunguu saumu hukaushwa. Mchakato wa kukausha unasaidia vitunguu saumu kupunguza unyevu na kuzoea hali nje ya shambani. Kukaushaa kuna umuhimu (mkubwa sana) ikiwa vitunguu havijakomaa vizuri, kwani vitunguu vinaendelea kunyonya unyevu na virutubisho kutoka kwenye mashina na majani baada ya kung’olewa.

Katika maeneo makame, baadhi ya wakulima huweka vitunguu vilivyong’olewa kwenye mafungu mafungu shambani ili kukausha juani. Hata hivyo, njia hii haipendekezwi kwani baadhi ya vitunguu saumu vinaweza kuungua na jua, na mabadiliko makubwa ya joto kati ya mchana na usiku huathiri vitunguu na kupunguza ubora wake.

vitunguu saumu vinakaushwa shambani
Picha 19: Ukaushaji (curing) wa vitunguu saumu shambani (juani)

Ni bora kukaushia sehemu yenye kivuli ambapo mabadiliko ya joto siyo makubwa. Acha mimea ya vitunguu maji ikiwa kamilifu (usiondoe majani, mashina wala mizizi) na uitundike kwa mafungu au kuiweka kwenye vichanja katika sehemu kavu na yenye hewa ya kutosha isiyo na joto kali.

Acha vitunguu vikae kwa angalau wiki 2 – 4, ingawa unaweza kuvikausha kwa muda mrefu zaidi (kwa mfano miezi 2), na hiyo itafanya vitunguu kuhifadhika kwa muda mrefu zaidi. Ikiwa huna haraka ya kuuza au unataka kuhifadhi kwa muda mrefu zaidi, viache vitunguu saumu vikiwa na majani yake mpaka utakapotaka kuuza, havitaharibika.

kichanja maalumu cha kukaushia vitunguu saumu
Picha 20: Ukaushaji (curing) wa vitunguu saumu kivulini

Mapato ya vitunguu saumu

Kukata majani na Kuondoa uchafu

Baada ya kuvikausha vitunguu kwa angalau wiki 3, kata majani ya vitunguu saumu takriban inchi moja (sm 2.5) juu ya kitunguu na mizizi, kisha ondoa ngozi ya nje bila kufunua punje za vitunguu. Safisha udongo wowote uliobaki, na vitunguu vyako vitakuwa tayari kwa kuuza.

Ikiwa unataka kusubiri kwa muda kabla ya kuuza tunashauri uhifadhi vitunguu saumu kwenye mifuko ya net ambayo inaruhusu hewa kuingia na kutoka kwa urahisi.

Lakini pia kama huna haraka ya kuuza au unataka kuhifadhi kwa muda mrefu zaidi, viache vitunguu saumu vikiwa na majani na mizizi yake bila kuikata mpaka utakapotaka kuuza, havitaharibika.

ghala maalum la kukaushia vitunguu saumu
Picha 21: Ghala maalum la kukaushia vitunguu saumu

Mavuno ya vitunguu saumu kwa ekari

Ekari moja ya vitunguu saumu inaweza kutoa kati ya tani 3 mpaka tani 5 kutegemeana na aina ya mbegu, matunzo ya shamba na hali ya hewa. Vitunguu saumu vya soft-neck vinauzao mkubwa zaidi kwa ekari kuliko vya hard-neck. Wakati elephant garlic vinauzao mkubwa zaidi kuliko vitunguu saumu vya soft-neck na vya hard-neck.

magunia ya vitunguu saumu shambani
Picha 22: Magunia ya vitunguu saumu na vingine vikiwa bado havijakatwa majani yako shambani

Masoko na mwenendo wa bei ya vitunguu saumu

Vitunguu saumu ni moja kati ya mazao ambayo yanayouzika katika masoko yote nchini Tanzania hasa ukanda wa pwani unaohusisha mikoa ya Tanga, Morogoro, Pwani, Lindi, Mtwara, Dar es salaam na visiwani Zanzibar na Pemba.

Kwa sasa uzalishaji wa vitunguu saumu nchini ni mdogo sana ukilinganisha na mahitaji ya sokoni, na kwa sababu hiyo mzigo wowote unauzika vizuri kabisa sokoni ilimradi tu ukidhi viwango vya ubora na afya.

Bei ya vitunguu saumu mwaka huu (2024) ilikuwa yakustaajabisha sana. Miezi yote ya mwanzoni hadi kufikia June, vitunguu saumu vilikuwa kama dhahabu nyeupe. Bei ilianza kupaa kama utani kuanzia TZS 3500 kwa kilo, ikaenda TZS 7000, na kidogo tu ikawa TZS 14,000.

Siku moja nikiwa namnunulia mke wangu mboga-mboga na viungo sokoni nikaenda vinapouzwa vitunguu saumu, bei niliyoisikia pale sikuamini ikabidi niulize tena, lakini yule bwana aliirudia kama ilivyo (TZS 20,000 kwa kilo moja) huku akiwa busy na wateja wengine. Nilitafakari kwa muda kisha nikacheka halafu nikaomba nipimiwe robo ya kilo. Hapo nilikuwa soko la Madizini (Turiani) mkoani Morogoro.

Mpaka mwishoni mwa mwezi August 2024, bei ya vitunguu saumu kwenye soko lile lile ilikuwa TZS 6000 – 8000 kwa kilo moja. Bei kama hiyo, mwanzoni mwa mwezi September, nimeikuta soko la Mawenzi Morogoro. Ni mabadiliko makubwa sana (kutoka TZS 20,000 mpaka TZS 6000) lakini ndio hali halisi ya bei za mazao, hupanda na kushuka kulingana na uhitaji na upatikanaji wake sokoni.

Kwa mkulima, miezi mizuri sokoni ni kuanzia February mpaka July na miezi ya sikukuu kama December. Upatikanaji wa vitunguu saumu sio mkubwa katika kipindi hiki, hivyo basi ukifanya timing vizuri unaweza kukutana na bei nzuri itakayokupa faida mara dufu.

vitunguu saumu vilivyo katwa majani baada ya kukauka vizuri
Picha 23: Vitunguu saumu vilivyokauka vizuri na kukatwa majani yake

Sasa unaweza kujipatia Kitabu (PDF) cha Mwongozo wa kilimo cha Vitunguu Saumu sasa hivi kwa bei nafuu sana. Kitabu hiki kimeboreshwa zaidi kwa ushauri wa kitaalam, mapendekezo ya kiasi, na aina za mbegu bora, mbolea na viuatilifu vya kutumia pamoja na mchanganuo wa bajeti ya kilimo na faida. Bofya hapa kukipata ndani ya Whatsapp au bofya hapa kukipata kwa email.

Pls share this post

20 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

  1. Asante sana na Mungu akubaliki kwa elimu unayoitoa kwetu sisi tunaitaji kujifunza juu ya ukulima uliokuwa na faida nzuri kwa nyakati zote

  2. Nimefurahi kujifunza ulimaji wa vitunguu swaumu, Je Kwa Hali ya hewan ya mkoa wa mara- BUNDA inaweza kuzalishwa vitunguu swaumu?

  3. Kwanza nikupongeze kwa elimu bora pia nimepata mwanga wapi kwa kuanzia. Nina eneo la kama robo eka naliandaa kwa ajili ya vitunguu swaumu.
    Usiache kutoa elimu bora asante pia tuna thamini juhudi zako.