Kabichi (kabeji) ni moja ya mbogamboga zinazolimwa kwa wingi nchini Tanzania, inalimwa katika mashamba madogo madogo na makubwa ya kibiashara. Hulimwa zaidi katika mikoa ya nyanda za juu kama vile Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, na Iringa, yenye hali ya hewa ya baridi na mvua za kutosha. Hata hivyo, kabichi pia hulimwa katika maeneo ya nyanda za kati na chini yenye umwagiliaji mzuri. Ni rahisi kulima kabichi na ina mzunguko mfupi wa ukuaji, kwa kawaida hukomaa ndani ya miezi 3 hadi 4, na kuifanya kuwa chaguo la kuvutia kwa wakulima wanaotafuta faida ya haraka kwenye uwekezaji.
Kabichi ni moja ya mbogamboga zinazoliwa sana nchini Tanzania kutokana na kuwa na matumizi mengi, unafuu wake na faida zake kiafya. Kabichi ina vitamini nyingi muhimu kama vile Vitamini C, ambayo huongeza kinga, na vitamini K, ambayo ni muhimu kwa kuganda kwa damu na afya ya mifupa. Pia ni chanzo bora cha nyuzi lishe (dietary fiber), kuboresha usagaji chakula na afya ya moyo. Kwa sababu ya upatikanaji wake na unafuu wake, kabichi ni chakula maarufu katika nyumba nyingi za Kitanzania, mara nyingi hujumuishwa katika milo kama kitoweo, au saladi kwa milo mikuu kama vile ugali, wali, chipsi na nyama.
Mbali na faida zake kiafya, kilimo cha kabichi pia hutoa faida za kijamii na kiuchumi kama vile kuongeza mapato kwa wakulima wazarishaji, kuboresha usalama wa chakula, na kutoa fursa za ajira katika uzalishaji, usafirishaji na uuzaji masokoni.
Kitaalam, kabichi ipo katika kundi la mimea la brassica. Kundi hili linahusisha mbogamboga zote za jamii ya kabichi ambazo hujumuisha kabichi za vichwa, kabichi za majani na kabichi za mizizi. Kabichi za vichwa (head cabbage) ni kama vile Kabichi nyeupe, kabichi nyekundu, kabichi ya kichina (pe-tsai), na Savoy. Kabichi za majani (leaf cabbage) ni kama vile Sukuma wiki, figiri (saro au loshuu) na pak choi (chainizi ya kawaida). Na za mizizi (root cabbage) ni kama vile turnip na radish.
Kwenye makala hii tutajadili kuhusu kilimo cha kabichi za vichwa (head cabbages).
Unahitaji nini ufanikiwe katika kilimo cha mbogamboga hii ya Kabichi?
Kimsingi nimeandika makala hii ili kujibu swali hili, nikuombe utulivu na umakini wako wakati tukichambua kipengele kimoja baada ya kingine katika jitihada za kujibu swali hili. Mambo ya kujifunza ni mengi sana, kwa hiyo ukiona kuna jambo hatujalijadili au hujalielewa basi tuulize kwenye form ya maoni mwishoni mwa makala hii. Lakini pia tushirikishe uzoefu wako juu ya kilimo cha kabichi: kimekufaidisha kiasi gani? au kilikupiga? Na je, umeona fursa yoyote kwenye kilimo cha kabichi?
Sasa tuendele kujibu swali la msingi: Unahitaji nini ili ufanikiwe kwenye kilimo cha kabichi?
Mahitaji ya kiikolojia
Hali ya hewa
Kilimo cha kabichi kinahitaji sana hali ya hewa ya ubaridi. Jotoridi la 150C – 200C linafaa sana kwa uzalishaji wa kabichi. Hata hivyo zao hili ni sensitive sana kwa mabadiliko ya hali hewa.
Jotoridi la hewa likishuka mpaka 100C linapunguza kasi ya ukuaji wa kabichi na kuchochea kuchanua (flowering), ingawa ukuaji wake unaendelea hata joto likishuka mpaka 50C. Joto likizidi sana, zaidi ya 250C, linasimamisha ukuaji wake.
Mimea michanga ya kabichi ina uwezo mkubwa zaidi wa kuhimili joto la chini sana na la juu sana.
Udongo na mwinuko
Kwa ujumla kabichi hustawi karibu kwenye udongo wa aina zote; kuanzia udongo wa kichanga laini (Sandy loam) hadi udongo wa mfinyanzi (Heavy soils). Udongo wa kichanga laini (Sandy loams) hutoa mazao mengi au kabichi zenye uzito mkubwa ukifuatiwa na mfinyanzi wa kati (Clay loams).
Udongo wenye tindikali nyingi huzorotesha ukuaji wa kabichi. Udongo mzuri kwa kabichi ni ule ulio na tindikali kati ya ph 5.5 – 7.5. Huhitaji udongo wenye rutuba ya kutosha; hasa ule ulio na nitrojenia pamoja na Fosifora ya kutosha. Mbolea aina ya Samadi (FYM) huongeza ukuaji na ubora wa kabichi kuliko mbolea za viwandani.
Kabichi inastawi vizuri zaidi katika maeneo yenye miinuko ya mita 1200 – 2000 juu ya usawa wa bahari.
Maeneo yanayolima kabichi
Hapa Tanzania kabichi hulimwa karibu maeneo yote ya nyanda za juu; kama vile Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Njombe na Songwe, maeneo ambayo ni ya baridi karibu msimu wote wa mwaka. Pia hulimwa katika maeneo ya uwanda wa kati kama vile baadhi ya maeneo ya Tanga na Morogoro.
Jinsi ya kuandaa shamba
Shamba kwa ajili ya kilimo cha kabichi linatakiwa lisafishwe mapema, kabla ya mvua kunyesha na kulingana na ukanda na hali ya hewa ya eneo husika. Baada ya kusafisha shamba kinachofuata ni kukatua (ploughing) na kupiga halo (harrowing). Shamba likatuliwe kwa kina cha sentimeta 30 mpaka 45 sawa na futi moja mpaka moja na nusu (rula 1 – 1.5).
Lengo la kukatua ni kuchanganya udongo, kuchimbua magugu, kufanya udongo upitishe maji na hewa kirahisi na kuchanganya mabaki ya mazao ya msimu uliopita na udongo.
Lengo la kupiga halo (harrow) ni kuvunja-vunja mabonge ya udongo hivyo kufanya udongo kuwa laini na kukatakata magugu magugu yaliyolichimbuliwa shambani.
- Shamba liandaliwe mwezi 1 – 2 kabla ya kupanda miche.
- Choma magugu juu ya udongo ili kua vimelea vya magonjwa na wadudu waharibifu wa mazao.
- Mwagilia maji ya kutosha kwenye udongo siku 1-2 kabla ya kuhamishia miche shambani ili kupooza ardhi na kusawazisha udongo.
- Andaa mashimo ya miche ya kabichi kulingana na idadi ya miche uliyonayo, nafasi na aina ya kabichi.
- Weka mbolea (samadi/mboji) ya kutosha kwenye mashimo.
- Nafasi kati ya mche hadi mche iwe wastani wa sentimeta 50 – 60 kwa sentimeta 50 – 60 kutegemeana na aina au zao litakalo changanywa na kabichi.
Mbegu bora na Upandaji wa kabichi
Uchaguzi wa mbegu bora za kabichi
Aina za kabichi zinazolimwa tanzania
Kabichi zipo za jamii tatu…
- Kabichi za Maua: kama broccoli na cauliflower
- Kabichi za Majani na Vichwa: za vichwa ni kama vile Kabichi nyeupe, kabichi nyekundu, kabichi ya kichina (pe-tsai), na Savoy. Za majani ni kama vile Sukuma wiki, figiri (saro au loshuu) na pak choi (chainizi ya kawaida).
- Kabichi za mizizi: ni kama vile turnip na radish.
Zifuatazo ni baadhi ya aina za kabichi za vichwa zinazolimwa kwa wingi zaidi nchini Tanzania…
- Glory F1
Aina hii huvumilia hali ya jua kali, na haipasuki ingawaje huchelewa kukomaa. Ina umbo la mviringo (Vichwa vyake).
- Copenhagen Market
Sifa kubwa ya Copenhagen ni kukomaa mapema; ingawaje vichwa vyake hupasukapasuka. Vichwa vyake navyo ni vya mviringo.
- Prize Drum Head
Ina vichwa vikubwa ambavyo ni bapa. Sifa nyingine ya kabichi hizi ni kwamba zinavumilia hali ya ukame / jua; lakini huchelewa kukomaa na hupasuka kirahisi.
- Ox heart
Ina sifa kadhaa ambazo hupendelewa sana na walaji kama vile; ladha tamu na kukomaa mapema. Kabichi au vichwa vyake ni vidogo vilivyochongoka mithili ya moyo wa ng’ombe (hujulikana kama chapa moyo).
- Early Jersey Wake Field
Hukomaa mapema na in vichwa vikubwa ambavyo hufunga vizuri; umbo la kichwa chake huonekana la kuchongoka kidogo. Lakini si kama lile la chapa moyo.
- Zipo aina nyingine kama: Danish Ball Head, n.k.
Jinsi ya kuandaa kitalu cha kabichi
Sehemu ya utakayoifanya kuwa kitalu cha kabichi hakikisha ina sifa zifuatazo…
- Kitalu kiwe karibu na maji ya kutosha na ya kudumu.
- Andaa kitalu sehemu iliyo wazi na yenye udongo ulio na rutuba ya kutosha.
- Eneo la kitalu kama ni kubwa liwe sehemu tambarare au kwenye mwinuko wa wastani ili kuepuka maji kutuama kwenye kitalu.
- Kitalu cha kabichi kiwekwe sehemu ambayo haikuwa na zao la kabichi au jamii ya kabichi msimu uliopita.
- Andaa kitalu sehemu ambayo ni rahisi kuhamishia miche shambani au kusafirisha kwenda sehemu nyingine kwa urahisi.
Kuandaa matuta ya Kusia mbegu za Kabichi
Kuna aina tatu za matuta: ya kunyanyulia udongo (Raised seedbed), ya Makingo (Sunken seedbed), na Matuta ya Kawaida (Flat seedbed).
Mbali na matuta yaliyotajwa hapo juu; mbegu zinaweza kuatikwa kwenye vyombo mbalimbali kama vile tray maalum za kupandia miche (seedling trays), vijisanduku vidogo vilivyojazwa udongo, n.k.
Fuata utaratibu huu hapa wakati wa kuandaa matuta ya kitalu
- Tuta liwe na upana kati ya sentimita 90 – 120; urefu unaweza kuwa wowote ili mradi muhudumu aweze kutoa huduma nyingine zote kitaluni bila kukanyaga miche.
- Lima kwa kukwatua kina cha kutosha kati ya sentimita 15 – 20 ili kuruhusu mizizi kusambaa vizuri ardhini.
- Choma takataka juu ya kitalu au weka nyasi juu ya kitalu, kisha funika kitalu kwa nailoni kwa muda wa majuma 5 – 8 ili kudhoofisha vimelea vya magonjwa na wadudu walioko kwenye udongo.
- Wakati wa kuandaa kitalu ongeza mbolea aina ya vunde, mboji au samadi, kisha isambaze (na uvuruge) ili ichanganyikane vizuri na udongo.
- Changanya kiasi cha debe 1 hadi 2 kila baada ya mita moja (wastani wa hatua moja) ya mraba.
- Tuta lisiwe na mabonde mabonde au mawe ambayo yanaweza kuzuia usambaaji mzuri wa mbegu kwenye tuta. (Tuta lisawazishwe vizuri ili mbegu zisambae vizuri, jambo ambalo litazuia mbegu kufukiwa kina kirefu na kusababisha mbegu kutokuota.)
Jinsi ya kupanda mbegu za kabichi
Sia (panda) mbegu za kabichi kwa kufuata utaratibu huu hapa …
- Hakikisha ubora na uotaji wa mbegu kabla ya kusia kitaluni (Germination test).
- Sia mbegu kwenye mistari kulingana na ukubwa wa tuta; umbali kati ya mstari na mstari iwe kati ya sentimita 15 – 20.
- Kina cha mstari kisiwe cha kutisha bali kiwe kati ya sentimeta 1 – 2.
- Matuta yamwagiliwe maji ya kutosha siku moja kabla ya kusia mbegu. Tumia chombo cha kumwagilia maji (watering can).
- Sambaza mbegu vizuri kwenye mstari; ili kuhakikisha mbegu zimesambaa vizuri; changanya mbegu na mchanga laini kisha sia kwa uangalifu, ili kuzuia msongamano wa miche kitaluni.
- Mbegu zitakazo siwa kwenye tuta lisilo na mistari zisambazwe vizuri kuepuka msongamano wa miche. Msongamano wa miche kitaluni huongeza kasi ya magonjwa ya ukungu kama vile Damping Off.
- Weka matandazo kiasi ambacho hakitazuia kuota kwa mbegu.
- Baada ya kusia mbegu mwagilia maji kwa chombo (watering can) kiasi cha kutosha kulingana na unyevunyevu ulioko ardhini.
Utunzaji wa mbegu ya Kabichi Kitaluni
- Mwagilia maji mara kwa mara kiasi cha kutosha kulingana na kiasi cha unyevunyevu ardhini.
- Ondoa matandazo mara baada ya mbegu kuota kisha weka chanja ili kupunguza mionzi ya jua ambayo inaweza kuunguza miche michanga hasa kipindi cha jua kali.
- Miche iliyoota kwenye nafasi ya kutosha huepuka magonjwa ya mnyauko; hivyo huwa na afya ya kuridhisha.
- Punguza miche (thinning) ibakie kwenye nafasi ya kutosha kati ya sentimeta 3 – 5 kutegemeana na aina ya mbegu.
- Weka matandazo kati ya mistari ya miche ili kupunguza magugu na kuzuia kasi ya matone ya mvua pamoja kurutubisha udongo.
- Miche imwagiliwe hadi kufikia kiwango cha kuhamishia sham-bani.
- Punguza kiwango cha kumwagilia maji siku chache kabla ya kuhamishia miche shambani, kati ya siku 6 – 12.
- Miche ya kabichi hukaa kitaluni kwa muda wa wiki nne mpaka sita. Ingawa aina nyingi huwa tayari zinapofikisha siku 30 tangu zilipoota.
Kiasi cha Mbegu kwa Ekari
Ili kupanda ekari moja ya kabichi unahitaji mbegu kiasi cha gramu 300 – 500. Kwa hekta moja utahitaji gramu 750 – 1250 za mbegu ya kabichi. Hii inategemeana na nafasi ya kupandia utakayoitumia.
Upandaji wa kabichi
Msimu wa kupanda kabichi
Kabichi inaweza kupandwa katika misimu miwili Tanzania: msimu wa masika (March – June) na vuli (September – December). Licha ya kuwa kabichi inahitaji hali ya hewa ya ubaridi na unyevu unyevu, inaweza kustawi katika vipindi vyote vya mwaka ilimradi tu uweze kumwagilia kwa utaratibu wakati wa ukame.
Nafasi ya kupandia kabichi
Nafasi ya kupanda inategemea aina ya mbegu, lengo la mavuno, hali ya udongo na zana zinazotumika kupandia. Nafasi kati ya mche hadi mche iwe wastani wa sentimeta 60 kwa sentimeta 60 kutegemeana na aina au zao litakalo changanywa na kabichi. Nafasi za sm 45 kwa sm 60, sm 50 kwa sm 60 pia zinafaa.
Jinsi ya kupanda kabichi
Kuna njia mbili kuu za kupanda kabichi. Njia hizi ni kupanda kwa matuta na kupanda kwa sesa. Kwa uzalishaji mzuri wa kabichi, tunashauri utumie njia ya matuta.
Kabichi huanza kuoteshwa kitaluni na baada ya siku 30 au hung’olewa na kupandwa shambani.
Fuata utaratibu ufuatao wakati wa kupandikiza miche ya kabichi shambani …
- Mwagilia kitalu cha miche masaa machache kabla ya kuhamishia shambani ili wakati wa kung’oa miche, mizizi ishikamane vizuri na udongo.
- Mashimo yaandaliwe mapema katika nafasi zinazopendekezwa. Nafasi tunazopendekeza ni sm 45 x 60, sm 50 x 60, na sm 60 x 60.
- Miche mizuri ni ile iliyo na afya nzuri, yenye majani kati ya 3 – 5, na iliyo na mizizi yenye afya na ya kutosha.
- Miche ipandwe siku hiyo hiyo ya iliyong’olewa toka kitaluni.
- Hamishia miche shambani wakati wa jioni ili kuepuka mionzi mikali ya jua. Kama utapanda wakati wa vipindi vya baridi unaweza kahaimishia miche shambani wakati wa asubuhi.
- Ng’oa miche kwa uangalifu pamoja na udongo wake kwa kutumia vifaa maalum ili mizizi isidhurike.
- Panda miche shambani kimo kile kile ilichokuwa kitaluni.
- Mwagilia miche maji ya kutosha mara tu baada ya kupanda.
Mbolea za kupandia kabichi
Kabichi ni zao lenye njaa sana. Usipolipa mbolea yakutosha, kabichi hazitajitanua na hivyo kufanya zisitoe mavuno yakutosha.
Wakati wa kupanda kabichi weka samadi au mbolea ya mboji kiasi cha tani 4 kwa ekari kama mbolea ya kupandia. Hata hivyo samadi au mboji iwekwe wakati wa kuandaa shamba ili ichanganyike vizuri na udongo.
Lakini pia unaweza kupanda kwa kutumia (mchanganyiko wa) mbolea ya DAP kiasi cha kg 75, pamoja na Urea kg 50 na MOP kg 30 kwa ekari. Mbolea za kupandia ziwekwe wakati wa kupanda miche ya kabichi shambani.
Au unaweza kutumia NPK (2:3:1) kiasi cha kg 150 kwa ekari. Na hii ni mbolea bora zaidi ikiwa utaipata.
Sasa unaweza kujipatia Kitabu cha (PDF) Kilimo cha Kabichi sasa hivi kwa bei nafuu sana. Kitabu hiki kimeboreshwa zaidi kwa ushauri wa kitaalam na picha ili uweze kuelewa na kutekeleza mbinu bora tulizoelezea. Bofya hapa kukipata ndani ya Whatsapp au bofya hapa kukipata kwa email.
Mbinu za utunzaji wa kabichi
Udhibiti wa magugu kwenye kabichi
Palizi kwa jembe la mkono
Magugu ni lazima yaondolewe shambani ili kuepusha yasishindane na mazao yako kutumia maji, rutuba, nafasi na mwanga. Vitu hivi vyote ni muhimu sana katika ustawi na uzalishaji wa mazao yako ya kabichi.
Kabichi zinatakiwa zipaliliwe kuanzia ya wiki 3 hadi 4 baada ya kupandikiza kutegemeana na hali ya hewa au magugu yanapojitokeza.
Jembe la mkono linafaa kwa palizi kwa vile linaweza kuondoa aina zote za magugu.

Palizi kwa Kutumia Viuagugu
Kabla ya kupanda kabichi: Viuagugu vinavyotumika kabla ya kupanda ni Paraquat na Glyphosate, mfano: Gramaxone, na Round up. Viuagugu hivi vipigwe wakati magugu yana ukijani na sio yakiwa makavu. Na lengo la kutumia viuagugu hivi ni kusafisha shamba kwa kuwa vinaua aina zote za magugu shambani, na kama kuna mazao (yote yatakufa pia).
Baada ya kupanda kabichi: Usitumie dawa yoyote kwa ajili ya kuua magugu kwenye shamba la kabichi mpaka utakathibitisha kuwa haitaathiri mazao yako ya kabichi. Hivyo basi shirikiana na wataalam katika kuhaikisha hilo.
Angalizo: Zingatia kanuni bora za matumizi ya viuatilifu kama vile kusoma vibandiko vya kwenye vifungashio vya dawa na jinsi ya kutumia viuatilifu hivi, kutumia vipimo vilivyo pendekezwa na kutumia zana za kujikinga wakati wakutumia viuatilifu hivi.
Mahitaji ya mbolea kwenye kilimo cha kabichi
Mbolea za kupandia
Kabichi ni zao lenye njaa sana. Usipolipa mbolea yakutosha, kabichi hazitajitanua na hivyo kufanya zisitoe mavuno yakutosha.
Wakati wa kupanda kabichi weka samadi au mbolea ya mboji kiasi cha tani 4 kwa ekari kama mbolea ya kupandia. Hata hivyo samadi au mboji iwekwe wakati wa kuandaa shamba ili ichanganyike vizuri na udongo.
Lakini pia unaweza kupanda kwa kutumia (mchanganyiko wa) mbolea ya DAP kiasi cha kg 75, pamoja na Urea kg 50 na MOP kg 30 kwa ekari. Mbolea za kupandia ziwekwe wakati wa kupanda miche ya kabichi shambani.
Mbolea za kukuzia kabichi
Ili kustawisha kabichi ni muhimu sana kuweka mbolea ya kukuzia. Weka mbolea ya NPK (4:1:2) kiasi cha kg 50 kwa ekari. Au changanya kg 30 za Urea na kg 10 za MOP na kg 7 za DAP kisha uweke kwenye ekari moja zote kwa pamoja.
Mchanganyiko huu wa mbolea ya kukuzia uwekwe (yaani urudiwe) katika tatu tofauti: siku kumi baada ya kupandikiza miche shambani, halafu urudiwe tena siku 20 baada kupandikiza miche na mwisho uwekwe tena (kiasi kile kile) siku 10 baada tu ya kabichi kuanza kutengeneza vichwa.
Angalizo: Hakikisha unatumia viwango sahihi vya mbolea. Na njia sahihi ya kujua upungufu wa virutubisho kwenye udongo ni kupima udongo wako. Pima udongo!
Mbolea za Asili
Samadi: Mbolea hii inatokana na masalia ya Wanyama tunaowafuga majumba; kama vile ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku, nguruwe, farasi, n.k. Mabaki haya ni pamoja na kinyesi, mkojo, matandiko na mabaki ya malisho. Kwa maeneo ambayo samadi inapatikana matumizi ya tani 10 ya samadi iliyooza vizuri kwa ekari itasaidia uzaaji mzuri wa kabichi na mazao mengine yatakayofuata kwenye kilimo mzunguko (crop rotation).
Mbolea za asili zina kiwango kidogo cha virutubisho ukilinganisha na zile za viwandani kwa hivyo unahitaji tani nyingi kwa ekari moja kufikia kiwango kinachohitajika.
Mbolea ya mboji: Mboji inatengenezwa kwa kutumia mchanganyiko wa masalia ya mimea, matawi ya yaliyodondoka, magugu, majivu na takataka zingine za nyumbani. Ikiwezekana, ongeza samadi kwa kiasi kidogo wakati wa utengenezaji wa mboji. Ikiwa utahitaji kujifunza zaidi kuhusu mbolea ya mboji soma kwenye makala niliyo-link hapa.
Angalizo: Samadi na mboji bora ni ile iliyoozeshwa vizuri kwa kutunzwa na kuhifadhiwa kivulini. Usitumie plastiki ama vipande vya chuma kutengeneza mboji.
Magonjwa na wadudu hatari kwa kabichi
Magonjwa na wadudu ni katika visumbufu ambavyo visipodhibitiwa kwa wakati vinaweza kukusababishia hasara ya hadi asilimia 100%. Yaani usipofanya jitihada za makusudi kudhibiti visumbufu hivi utaishia kutovuna chochote.
Magonjwa ya kabichi
Magonjwa ni kati ya vikwazo vikubwa kwenye juhudi za kuongeza uzalishaji wa kabichi Tanzania na yanaweza kusababisha hasara kwa asilimia mia moja (100%) yasipodhibitiwa.
(i) Uozo Mweusi (Black rot)
Huu ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vidogo sana jamii ya Bakiteria aina ya Xanthomonas spp kwa jina la kitaalam. Ugonjwa huu hushambaulia kabichi na jamii yake, na hushamiri sana maeneo yanayoambatana na joto pamoja na unyevunyevu.
Dalili za Uozo Mweusi
- Ingawa vimelea vya Uozo mweusi baadhi huishi ardhini au kwenye mbegu; dalili za mashambulizi huonekana mapema kwenye majani yaliyokomaa.
- Uozo huonekana kwenye majani ya kabichi hasa kwenye ncha za majani/pembezoni mwa jani.
- Shina linapokatwa huwa na mchanganyiko wa rangi ya udongo na nyeusi.
- Mara nyingine Uozo huu hubadilika kuwa aina nyingine tofauti kidogo ya uozo ambao hutoa harufu mbaya sana (soft rot).
- Alama kama ya “V” huonekana kwenye ncha za majani yaliyokomaa ikiwa na mchanganyiko wa rangi nyeusi na njano (inayoashiria uozo).
Ueneaji wa Uozo Mweusi
- Kupitia mbegu za kabichi silizoshambuliwa na uozo mweusi msimu uliopita.
- Kupitia maji ya kumwagilia hasa kama yanapita maeneo yaliyosham-buliwa na ugonjwa huu; na mara nyingine vimelea hivi hupeperushwa na upepo toka mmea mmoja au shamba hadi shamba.
- Vimelea vya uozo mweusi huingia ndani ya majani ya kabichi kupitia kwenye mmea au vidonda vilivyosababishwa na jembe wakati wa kupalilia au kushambuliwa na wadudu kama Nondo Mgongo Almasi wa kabichi (DBM).
Udhibiti husishi wa Uozi Mweusi:
- Sia mbegu ambazo hazikushambuliwa na Uozo mweusi.
- Miche inayoonyesha kuwa na uozo mweusi isihamishiwe shambani.
- Ondoa masalia ya kabichi shambani (choma moto pamoja na maotea yote baada ya mavuno).
- Magugu jamii ya kabichi yasiachwe karibu na shamba la kabichi.
- Kitalu cha kabichi kiandaliwe mapema iwezekanavyo,na mara baada ya kulima choma moto juu ya kitalu ili kuua vimelea vya ugonjwa huu kabla ya kusia mbegu.
- Jaribu kukwepa maji ya kumwagilia yanayopita kwenye shamba la kabichi ambalo limeathiriwa na ugonjwa wa uozo mweusi.
- Sumu zinazoweza kutumiwa ni pamoja na jamii ya copper. Hata hivyo sumu hizi hupunguza mashambulizi pale zinapotumiwa kwenye hatua za mwanzo wa mashambulizi tu.
(ii) Kuoza shingo (Bacterial Soft rot)
Ugonjwa huu husababishwa na vijidudu vya bakteria ambavyo viko kwenye udongo. Dalili za mashambulizi ya vimelea hivi ni pamoja na kabichi kubadilika rangi, kuoza na kutoa harufu mbaya.
Jinsi ya Kuzuia ugonjwa wa Kuoza Shingo
- Epuka kujeruhi kabichi hasa wakati wa kuvuna.
- Epuka kulundika kabichi sehemu moja kwa muda mrefu.
- Kabichi zihifadhiwe sehemu yenye ubaridi wa kutosha na yenye kuruhusu hewa ya kutosha.
- Mara baada ya kuvuna kabichi ni vizuri kung’oa na kuchoma masalia yote.
- Usirudie kupanda kabichi eneo moja wakati wote (eneo lililo kuwa na kabichi msimu uliopita lipandwe zao lingine tofauti na kabichi au jamii yake. (Badili mazao).
(iii) Uozo shina (Black leg)
Chanzo cha ugonjwa huu ni vimelea vya jamii ya ukungu; ambao husababisha madoa yaliyodidimia kwenye shina karibu na usawa wa ardhi; ambayo husababisha kuvimba kwa shina; uozo rangi ya kahawia ambayo huonekana shina likikatwa/pasuliwa; madoa meusi kwenye majani yaliyozungukwa na uyoga mweusi.
Kuzuia kuoza kwa shina:
- Andaa shamba mapema mara baada ya kuvuna.
- Ondoa masalia yote ya kabichi na magugu jamii ya kabichi shambani.
- Badili mazao
- Epuka kupanda kabichi maeneo yanayotuamisha maji.
- Tumia sumu za viwandani kama vile; Biddi star, Nyotaz, Ridomil gold, DKmino 76WG, DKmethyl, Zetanil 76WG, Snowthane M45, e.t.c
(iv) Ugonjwa wa Kiuno au Kinyausi (Damping Off)
Kiuno au Kinyausi ni moja kati ya magonjwa hatari kwenye vitalu vya mbogamboga; kabichi ikiwa moja ya mimea inayoshambuliwa sana na kiuno. Ugonjwa huu husababishwa na vimelea vya jamii ya ukungu kama vile: Fusarium spp; Rhizoctonia na Phytophthora spp.
Mara nyingi ugonjwa huu hujitokeza zaidi kwenye vitalu, hasa kwenye mimea iliyooteshwa sehemu ambayo kulikuwa na ugonjwa huo msimu uliopita. Vimelea vya ugonjwa huu hubaki ardhini kwa muda mrefu.
Mashambulizi na dalili zake
- Miche huonekana imenyauka kwenye visehemu vichache kitaluni (patches)
- Vidonda vinavyoonekana kuwa na majimaji (water soaked) kwenye shina, ambavyo hatimae huozesha shina.
- Kuoza kwa miche kabla majani hayajajitokeza juu ya ardhi.
- Miche iliyo mikubwa kiasi huonekana kuwa myembamba kwenye shina mithili ya waya.
- Miche iliyoshambuliwa na ugonjwa huu kama haikukauka ni rahisi sana kushambuliwa na magonjwa mengine.
Jinsi ya Kudhibiti Ugonjwa wa kiuno
- Andaa shamba mapema; lima kina cha kutosha ili kuruhusu udongo uwe na maji / unyevunyevu wa wastani.
- Hakikisha udongo una maji / unyevunyevu wa wastani.
- Weka matandazo.
- Unguza takataka juu ya vitalu ili kuua vimelea vya ugonjwa huu au funika kitalu kwa karatasi ya nailoni kwa muda wa majuma mawili au zaidi kabla ya kusia mbegu kitaluni, kutegemeana na hali ya hewa.
- Punguza miche kitaluni pale ambapo inaonekana kusongamana au wakati wa kusia mbegu, sia kwenye nafasi ya kutosha kuepuka msongamano wa miche kitaluni. Nafasi nzuri na ya kutosha ni kuanzia sentimita 15 – 20 mstari hadi mstari na sentimia 2-5 mche hadi mche. Nafasi hii itakupa miche bora na yenye afya nzuri.
- Kitalu kiwe sehemu iliyo wazi, ambayo haiko chini ya kivuli kizito. Ondoa magugu yote kwenye kitalu ili kupunguza kivuli kizito pamoja na kuruhusu mzunguko mzuri wa hewa kitaluni (free air circulation / movement)
- Weka majivu kitaluni au kuzunguka mmea
- Chagua miche yenye afya tu wakati wa kuhamishia miche shambani.
- Tumia sumu za viwandani kama vile; Ridomil gold, DKmino 76WG, DKmethyl, Zetanil 76WG, Snowthane M45, e.t.c
(v) Ubwiri Vinyoya (Downy Mildew)
Ugonjwa huu husababishwa na vimelea vya jamii ya ukungu. Mara nyingi hujitokeza kwa wingi wakati miche iko kitaluni; hasa vipindi vya baridi na unyevunyevu.
Mashambulizi na dalili zake
- Mashambulizi hujitokeza mapema kwenye wakati miche ikiwa kitaluni.
- Sehemu zinazoshambuliwa mapema ni zile ambazo ni teketeke (laini).
- Dalili za mashambulizi hujitokeza kwenye majani machanga, ambayo huwa na mviringo wa kijani kilichopauka, chenye kuzungukwa na rangi ya njano.
- Rangi kama ya kijivu au poda nyeupe huitokeza chini na juu ya jani, kuhashiria (Ukungu) ambao huonekana kuwa na vijidonda vidogo vidogo.
- Ukungu huu huendelea kubaki kwenye majani ya spinach; au Chinese cabbage hata baada kuvuna.
- Kama ukungu wa aina hii haukudhibitiwa unaweza kusababisha hasara kati ya asilimia 40 – 90 ya miche michanga kitaluni.
Jinsi ya Kudhibiti Ubwiri Vinyoya
- Badili mazao
- Kitalu kiwe safi wakati wote.
- Choma magugu/masalia ya kabichi baada ya kuvuna.
- Panda kabichi sehemu ambayo haituamishi maji.
- Jaribu sumu za asili.
- Tumia sumu za viwandani kama vile; Biddi star, Nyotaz, Ridomil gold, Zetanil, Rio gold, Snowthane M45, e.t.c
- Epuka kusongamanisha miche kitaluni.
- Kumwagilia maji kupita kiasi.
- Nyunyizia sumu za asili kama vile maziwa fresh + majivu + sabuni (mchanganyiko). Uwiano: Maziwa fresh : Maji : Sabuni (Lita 1 : lita 10 : gramu 10)
(vi) Club rot (Uvimbe wa mizizi)
Uvimbe wa mizizi ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vya jamii ya Ukungu (Plamodiophora brassicae). Vimelea hivi vikiwa kwenye mazingira mazuri hudumu kwenye ardhi kwa muda mrefu; yaani hadi miaka 10.
Dalili za mashambulizi ya Club rot:
- Uvimbe au virungu vingi kwenye mizizi vyenye ukubwa na umbile tofauti.
- Kudumaa kwa mmea (Stunted growth)
- Kusinyaa kwa mmea (wilting)
- Kijani chepesi / mpauko kilicho changanyikana na rangi ya njano.
- Kukauka kwa mmea.
- Kupasuka kwa ardhi pale kabichi ilipooteshwa (cracking of the soil).
NB: Club rot huathiri jamii yote ya kabichi na hujitokeza zaidi ukanda wa baridi.
Jinsi ya Kudhibiti Uvimbe wa mizizi
- Hakikisha kuwa shamba lina mbolea (samadi) ya kutosha (FYM).
- Panda mbegu ambazo hazikushambuliwa na ugonjwa wa ukungu; (clean certified seeds).
- Panda aina ya kabichi stahimilivu kwa ugonjwa huu.
- Panda aina ya kabichi zinazokomaa mapema.
- Badili mazao.
- Ng’oa kabichi zilizoshambuliwa kisha choma moto.
- Tumia mbinu mbalimbali kubadili tindikali kwenye udongo.
Wadudu waharibifu wa Kabichi
(i) Nondo mgongo almasi (Diamond back moth: Plutella xylostella)
Nondo Mgongo wa Almasi ni mdudu hatari sana kwenye zao la kabichi. Mdudu huyu hupatikana maeneo yote yanayolima kabichi. Asipodhibitiwa husababisha hasara kubwa kuanzia mavuno hadi ubora wa kabichi yenyewe. Kiwavi wa kabichi huzaana kwa haraka sana; tena kwa kipindi kifupi.
Mdudu huyu hushambulia mazao yote ya jamii ya kabichi na magugu ya jamii ya kabichi.
Mazingira yanayomfaa Nondo Mgongo Almasi (DBM):
- Hupendelea zaidi mazingira ya joto (kipindi cha kiangazi / ukame) kipindi ambacho huzaliana kwa wingi.
- Mazingira yaliyo na masalia ya kabichi (baada ya kuvuna).
- Kuwepo kwa mimea mingine (magugu n.k) jamii ya kabichi karibu na shamba la kabichi.
- Kutobadili mazao kwenye shamba la kabichi kwa muda mrefu.
Mashambulizi na dalili zake:
Nondo Mgongo Almasi hushambulia jani la kabichi upande wa chini ya jani, na kusababisha vitobo au uwazi mithili ya kioo kwenye jani. Mashambulizi haya huanzia kitaluni hadi shambani.
Matokeo ya mashambulizi…
- Mmea hukua kwa tabu hasa kama mashambulizi yameanzia kitaluni.
- Mavuno hupungua (uzito wa kabichi)
- Bei ya kabichi ya namna hii thamani yake sokoni hupungua.
- Kabichi iliyoshambuliwa na funza/kiwavi uwezekano wa kushambuliwa na magonjwa ni mkubwa sana (Secondary source of disease infection) kama vile: Magonjwa ya ukungu, Bacteria (black & soft rot disease).
Jinsi ya Kudhibiti Nondo Mgongo Almasi
- Masalia yote ya kabichi yaondolewe shambani mara baada ya kuvuna.
- Ondoa / choma magugu yote jamii ya kabichi wakati wa kuandaa shamba.
- Kitalu cha kabichi kiandaliwe mbali na shamba ambalo lina kabichi ambazo zimeanza kukomaa.
- Wakati wa kukagua shamba jaribu kuua viwavi wa kabichi kwa mkono kama ni wachache.
- Mwagilia maji kitaluni kwa kutumia ndoo (watering can au sprinkler kwenye shamba) kutegemeana na uwezo ulionao.
- Usirudie kupanda kabichi eneo moja mfululizo.
- Changanya mazao (intecropping) kwa mfano, vitunguu maji, vitunguu saumu (onion/garlic).
- Tengeneza mazingira mazuri ya viumbe marafiki, hasa kwa kuweka matandazo, kupunguza kiwango cha unyunyiziaji sumu za viwandani na kuweweka mbolea ya samadi ya kutosha.
- Baadhi ya viumbe marafiki ni pamoja na Diadegma spp, Oomysus spp n.k.
- Tumia sumu za asili kama vile: Muarobaini (Neem), MFORI na Utupa.
- Tumia dawa kama Snowtiger, Duduwill, Snowcron, Ninja Plus 5EC, Wilcron, Profecron, e.c.t. mara uwaonapo wadudu.
(ii) Nzi wa Kabichi (Cabbage Saw Fly: Athalia spp)
Hawa ni wadudu wanaofanana sana na inzi; tofauti iliyopo ni kwamba; inzi hawa wana mchanganyiko wa rangi nyeusi na njano kwenye mbawa; pia inzi hawa viwavi/funza wake hushambulia majani ya kabichi na kubakisha vishipa vya majani.
Viwavi hawa wakishaingia kwenye hatua ya inzi kamili hawana madhara. Vipindi vya mashambulizi makubwa ni wakati mimea ingali michanga.
Mazingira ya Inzi wa Kabichi
Mazingira ya Inzi wa kabichi yanafanana sana na yale ya Nondo Mgongo Almasi. Mdudu huyu hushamiri vipindi vya joto; na hushambulia kabichi pamoja na jamii yake kama Nondo Mgongo Almasi; isipokuwa tofauti ipo kwenye mashambulizi na dalili zake.
Mashambulizi na Dalili za Inzi wa Kabichi:
- Mashambulizi hufanywa na inzi hawa wakiwa katika hatua ya kiwavi.
- Kiwavi hushambulia majani ya kabichi na kuacha vijishipa vidogo (midribs);
- Matokeo ya mashambulizi haya ni ama kudumaa kwa mmea au kutoendelea tena kutengeneza chakula cha mmea.
Kiwavi huyu anafanana sana na yule wa Nondo Mgongo Almasi; tofauti kubwa iliyopo ni idadi ya miguu; Inzi wa kabichi ana pair sita za miguu wakati Nondo Mgongo Almasi ana pair nne.
Tofauti nyingine ni ile ya buu kuwa kwenye udongo wakati buu wa Nondo Mgongo Almasi huwa kwenye majani ya kabichi.
Ukubwa: Kiwavi wa Inzi wa kabichi ni mkubwa zaidi ukilinganisha na yule wa Nondo Mgongo Almasi. Hatua ya kiwavi ni hatari kwani kiwavi ndiye anaye kula na kufanya madhara kwenye kabichi.
Jinsi ya kudhibiti Inzi wa Kabichi
- Haribu mazingira anayopendelea kuzalia: Mazingira machafu na masalia ya kabichi za msimu uliopita yaliyoko karibu na shamba la kabichi yafukiwe au lisha mifugo (ng’ombe n.k.)
- Nyunyuzia muarobaini.
- Tumia dawa kama Dudu plus ya ETG, Pilarmida, Abanil, Ninja Plus 5EC, Dudu Acelamectin, e.c.t. mara uwaonapo wadudu.
(iii) Vidukari (kimamba – Aphids)
Hawa ni wadudu wadogo wenye rangi ya kijani na nyeusi au khaki; baadhi huwa na mbawa. Mbali na kimamba kufyonza kabichi; kimamba hueneza magonjwa jamii ya virusi ambavyo hudhoofisha sana kabichi.
Dalili nyingine ya mashambulizi ya kimamba, ni kubadilika majani na kuwa rangi ya nyeupe au njano iliyopauka; kudumaa kwa mmea na hatimaye hukauka.
Kudhibiti kimamba wa kabichi
- Epuka kuotesha kabichi vipindi vya joto (ikibidi).
- Weka majivu kenye majani yaliyo na kimamba.
- Tengeneza mazingira mazuri ya wadudu marafiki.
- Nyunyizia MFORI uliovundikwa kwa siku 10 – 14 kwa uwiano wa 1:3-5.
- Nyunyizia mchanganyiko wa maji na sabuni kiasi cha vijiko viwili vya mchanganyiko huo kwa lita ya maji (10-20) ml/lita.
- Tumia dawa kama General 200SL, Protector 750WG, Abanil na Ninja Plus 5EC, Dudu Acelamectin, e.c.t. mara uwaonapo wadudu.
NB: Wadudu wanaoshambulia Sukuma wiki, Chinese Cabbage na Cauliflower wengi wao wanafanana sana na wale wanaoshambulia Kabichi (Kwa mfano DBM, Kimamba n.k) hivyo njia za kudhibiti wadudu na magonjwa kwenye mazao haya zinafanana.
(iv) Sota (Cutworm)
Sota in mdudu anayeshambulia mazao ya aina nyingi kitaluni; Baadhi ya mazao yanayoshambuliwa na sota ni pamoja na Pamba, mpunga, viazi, tumbaku, jamii yote ya nafaka na mboga mboga: (cereals and vegetables)
Mdudu huyu huishi ardhini; na hukata mimea/miche ikiwa bado michanga. Hukata shina usawa wa ardhi, hivyo kusababisha mmea kushindwa kukua hasa jamii ya mboga-mboga. Mimea inayoweza kujitahidi kukua ni michache sana hasa ile ya jamii ya nafaka kama vile mahindi, mtama n.k.
Sota wadogo hula majani mbalimbali, wakati sota wakubwa hukata shina la mmea na mizizi. Ukataji huu hufanyika usiku. Miche iliyooteshwa kwenye mistari sota anapoanza kula huendelea na mstari huo hadi amalize ndipo ahamie mstari mwingine.
Kwa miche iliyooteshwa bila mistari; sota huendelea kukata kata miche yoyote ile iliyo karibu naye.
Mashambulizi na dalili za mashambulizi:-
- Majani yaliyokatwa na sota huonekana karibu na shina.
- Mche uliokatwa nao huonekana karibu na shina kama ulikuwa mkubwa.
- Kunyauka kwa mmea.
- Mara chache kinyesi au sota mwenyewe huonekana karibu na shina; kuashiria kuwa tatizo linaloonekana ni la sota na si mdudu mwingine au mnyama aliyesababisha tatizo hilo.
Kuanzia mayai hadi mdudu kamili huchukua mwezi mmoja hadi miwili kutegemeana na hali ya hewa. Kipindi kirefu ni kile cha funza ambacho kipindi chote cha hatua ya funza ndicho cha uharibifu kwenye mazao.
Jinsi ya Kudhibiti wa mdudu Sota
- Lima/andaa shamba mapema hasa mwezi mmoja kabla ya kusia mbegu; ili kutandaza funza juu ya ardhi ambako watashambuliwa na ndege, wadudu wengine au kuunguzwa na jua.
- Pale inapowezekana okota funza kwa mikono na kuwaua.
- Ongeza unyevu nyevu kwenye kitalu au shambani ili kusababisha mazingira mabaya kwenye udongo
- Weka majivu kuzunguka mmea au kwenye kitalu.
- Rudishia miche iliyokatwa na sota (gap filling)
- Tumia dawa kama Spidex, Multi Alpha, Dudu will, Profecron, Wilcron, Ninja Plus 5EC, e.c.t. mara uwaonapo wadudu.
(iv) Minyoo Fundo (Root Knot Nematode)
Hawa ni wadudu aina ya minyoo ambao huishi ardhini na hawaonekani kirahisi kwa macho. Wadudu hawa hushambulia mizizi ya kabichi jambo ambalo hudhoofisha ukuaji wa kabichi; pamoja na kabichi kushindwa kufunga vizuri.
Dalili na mashambulizi
- Kudumaa kwa mmea.
- Rangi ya kabichi hubadilika kutoka kijani kuwa njano kidogo.
- Mafundo fundo/nundu nundu kwenye mizizi.
- Kuoza kwa mizizi michanga.
- Kupasuka kwa mizizi.

Jinsi ya Kudhibiti Minyoo Fundo
- Kagua shamba mara kwa mara.
- Epuka kupanda kabichi kwenye eneo moja mfululizo (badili mazao); panda mazao mengine kama mahindi, vitunguu n.k.
- Ondoa masalia ya kabichi shambani ambayo yanaweza kueneza wadudu hawa, kisha yachomwe moto.
- Andaa shamba mapema.
- Tumia mbolea za asili (samadi, mboji, vunde) kila msimu kupunguza kuzaliana kwa wadudu hawa.
- Panda mbegu/miche inayostahimili mashambulizi.
- Tafuta viuatilifu vilivyothibitika kuudhibiti minyoo fundo.
Kanuni za usalama na matumizi ya viuatilifu
Viuatilifu ni kemikali na kemikali ni sumu, hivyo umakini ni muhimu sana wakati wote unapokuwa unazitumia. Soma hapa namna sahihi za matumizi ya viuatilifu
Uvunaji wa kabichi na Fursa za masoko
Uvunaji wa kabichi
Muda wa kuvuna
Kabichi hukomaa na kuwa tayari kuvunwa kati ya miezi 2 – 4 kutegemeana na aina ya kabichi, matunzo na aina ya udongo; kuanzia kuotesha mbegu kitaluni. Muda mzuri wa kuvuna ni asubuhi au jioni wakati hakuna jua kali.
Dalili za kabichi kukomaa
- Kufikia muda wake wa kukomaa tangu ipandwe. Hakikisha unajua mbegu uliyopanda inachukua muda gani kukomaa.
- Kabichi zilizokomaa zina majani yenye rangi ya kijani kibichi ambayo ni magumu (imara), na vichwa vyake ni vikubwa na vimejazia vizuri.
- Kabichi zilizokomaa zina majani yenye mviringo wa kijani kilichopauka, chenye kuzungukwa na rangi ya njano. Rangi kama ya kijivu au poda nyeupe hujitokeza chini na juu ya jani, kuashiria ukungu ambao huonekana kuwa na vijidonda vidogo vidogo.
Maandalizi ya kuvuna
Unapokaribia wakati wa kuvuna, fanya yafuatayo:
- Andaa usafiri na/au mteja kama utauzia shambani.
- Andaa utaratibu na vifaa vya uvunaji. Hii ni pamoja na vibarua, visu au mapanga, mifuko/viroba na kamba za kushonea.
- Panga wakati wa kuvuna: Kabichi zinapaswa kuvunwa asubuhi mapema au jioni ili kuepuka joto kali la mchana.
Jinsi ya kuvuna Kabichi
Kabichi inavunwa kwa kukata shina lake karibu sentimita 2.5 – 4 kutoka kwenye kichwa cha kabichi kwa kutumia kifaa chenye makali ya kutosha kama vile kisu au panga.
- Punguza majani ya nje, kiasi cha majani matatu au manne ya kijani ili kuzuia isinyauke au kupata vidonda na kuoza wakati wa kusafirisha.
- Muda mzuri wa kuvuna ni asubuhi au jioni wakati hakuna jua kali.
- Hifadhi kabichi kwenye kivuli wakati wa kuvuna.
- Kabichi zilizooza au zenye vidonda zisichanganywe na nzuri.
- Tenganisha kabichi kufuatana na ukubwa na ubora.
Kabichi huharibika haraka sana kutokana na kiasi kingi cha maji yaliyoko kwenye majani, hivyo ni vyema ikauzwa au ikatumika mapema baada ya kuvuna. Zile zinazotakiwa kusafirishwa, zisafirshwe mapema mara tu baada ya kuvuna. Au zihifadhiwe sehemu yenye ubaridi na mzunguko mzuri wa hewa.
Kiasi cha mavuno kwa ekari
Mavuno ya kabichi kwa ekari moja ni kati ya tani 20 hadi 60 kwenye shamba lililotunzwa kwa kufuata taratibu tulizoeleza au kanuni zingine za kilimo bora zinazolazimiana na mazingira yako. Hii ni sawa na tani 50 mpaka 120 kwa hekta moja. Hata hivyo kiasi cha mavuno kinategemeana na aina ya mbegu utakayopanda.
Fursa za masoko
Mahitaji ya kabichi nchini Tanzania yanaendelea kukua kutokana na ongezeko la watu, kukua kwa miji na kuongezeka kwa matumizi ya mbogamboga. Masoko ya mijini kama Dar es Salaam, Dodoma, na Mwanza ni miongoni mwa wanunuzi wakuu, ambapo watumiaji hutafuta mazao katika misimu yote ya mwaka. Kadiri mazoea ya lishe yanavyobadilika kuelekea kwenye lishe bora, mahitaji ya mboga kama kabichi yanatarajiwa kukua zaidi.
Mbali na masoko ya ndani, pia kuna fursa zinazojitokeza kwa wakulima wa kabichi katika masoko ya nje. Nchi kama Kenya, Uganda, na Zambia huagiza kabeji zinapokabiliwa na upungufu. Endapo patakuwa na mipango mizuri, wakulima wa Tanzania wanaweza kuzalisha kabichi katika misimu ambayo bei iko juu, hivyo kuongeza faida. Kilimo cha mkataba na kujenga ushirika na taasisi kama shule, maduka makubwa, hoteli, na migahawa ni njia zingine za ubunifu zinazoweza kuwasaidia wakulima kupata bei nzuri na soko la uhakika.
Kwa kuzingatia mbinu bora za uzalishaji na nyakati zenye mahitaji makubwa sokoni, wakulima wa kabichi wanaweza kuongeza maradufu uzalishaji, kunufaika na fursa za masoko na kukuza mapato yao kwa kiasi kikubwa.
Sasa unaweza kujipatia Kitabu cha (PDF) Kilimo cha Kabichi sasa hivi kwa bei nafuu sana. Kitabu hiki kimeboreshwa zaidi kwa ushauri wa kitaalam na picha ili uweze kuelewa na kutekeleza mbinu bora tulizoelezea. Bofya hapa kukipata ndani ya Whatsapp au bofya hapa kukipata kwa email.

Jr,nikipanda mbegu mojakwamoja shambani inafaa,au lazima nioteshe kitalu?
Ni muhimu kunyunyiza viuadudu wakati mbegu bado ziko kwenye kitalu??
Nahitaji kujifunza zaidi kulima kabeji
kazi nzuri mnatupa nguvu sisi wakulima asanteni sanaa
Darasa ni la moto San nimependa ulivyo elezea cabbage mm nimwanafunzi wa Horticulture Huku mwanza City college. Leo nimeamua kutoka nje na elimu chuon Ili nipate elimu ,Zaid napenda kilimo mwenzio
Vijana tuepuke umaskin kupitia kilimo cha kisasa Tanzania Horticulture
Asante sana kwa elimu hiyo. Kweli nimejifunza vitu vingi kuhusu kilimo cha kabeji.
Ninahitaji kujua, kuwa mbegu ya GLORY F1 inachuka muda mrefu kukomaa, je! Inatumia miezi mingapi kukomaa?