Mpunga ni zao la pili la chakula kwa umuhimu linalolimwa sehemu nyingi nchini Tanzania. Umuhimu wa zao hili umeongezeka kuanzia muongo uliopita kutokana na jamii za mijini na vijijini kupendelea zaidi kula wali na kupunguza ulaji wa vyakula vingine na kulifanya zao hili kuwa la chakula na biashara.

Mvua ni chanzo kikuu cha maji kwenye kilimo cha mpunga. Viwango vya mahitaji ya maji katika kukua kwa mpunga hutofautiana miongoni mwa aina za mpunga. Ni kwa jinsi hii mpunga hupandwa katika mazingira mbalimbali kutegemea na mahitaji yake ya maji.

Zipo aina tatu kuu za mazingira yanayolimwa mpunga kulingana na upatikanaji wa maji na hali ya mwinuko wa nchi. Mazingira haya ni kilimo cha mpunga wa mabondeni kinachotegemea mvua (72%), kilimo cha mpunga wa kwenye miinuko (20%) na kilimo cha mpunga cha umwagiliaji (8%).


Kiasi cha mpunga kinachozalishwa nchini kimekuwa kikiongezeka mwaka hadi mwaka kutoka tani 41,000 mwaka 1970 hadi tani 811,500 mwaka 1998. Ongezeko hili limetokana na kuongezeka kwa eneo linalolimwa mpunga na kwa kiasi kutokana na kuongezeka kwa miradi midogo ya umwagiliaji pamoja na matumizi ya tekinolojia bora za kilimo.

Maeneo yanayolima mpunga kwa wingi Tanzania: ni Morogoro maeneo ya bonde la kilombero/Ifakara, Dakawa, Malolo; Mbeya: Kyela, Mbarali; Shinyanga: Kahama; Mwanza, Bonde la Ruvu mkoani Pwani. Na maeneo mengine mengi.

shamba-la-mpunga
Sehemu ya shamba la mpunga uliostawi vizuri

pH ya udongo (Soil pH)

pH ni kipimo kinachoonyesha kiwango cha tindikali au nyongo katika udongo. Udongo waweza kuwa tindikali (ph ndogo kuliko 7), nyongo (ph kubwa kuliko 7), au katikati (neutral) – ph ya 7. Tindikali au nyongo ya udongo hupimwa kwa kutumia pH mita. Mazao mengi hustawi zaidi katika udongo wenye hali ya tindikali ya wastani (kipimo cha pH 5.5 hadi 7.0). Mpunga hustawi kwenye udongo wa mfinyanzi wenye tindikali ya wastani na virutubisho vya kutosha.


Je ungependa kupata Muongozo wa kilimo cha mpunga utakao kufahamisha gharama za uzalishaji na hatua zote za utunzaji wa mpunga? Wasiliana nasi ujipatie copy yako

Click to Tweet

Kuandaa Shamba, Kupanda na Kupalilia

Kuandaa shamba, kusafisha, kulima/kutifua

Ni vyema mashamba yaandaliwe mapema kabla ya msimu wa kupanda haujaanza ili kumpa mkulima fursa ya kupanda kwa wakati unaotakiwa. Kuna njia mbalimbali zinazotumika kuandaa mashamba. Kati ya njia hizi ni pamoja na kufyeka, kung’oa visiki na kulima. Shamba linaweza kulimwa kwa kutumia:

 • Jembe la mkono – wengi wanatumia
 • Jembe la kukokotwa na wanyama kama ng’ombe
 • Power tillers
 • Matrekta

Baaada ya kulima, shamba linawekwa maji ili liloane vizuri na kisha udongo unachanganywa vizuri na maji ili kutengeneza tope. Hii ni kuchavanga (puddling). Hii inarahisisha:

 • Kupandikiza miche
 • Kuhifadhi maji

Mbegu Bora za Mpunga

Matumizi ya mbegu bora ni muhimu katika upatikanaji wa mavuno mengi na bora. Kuna makundi mawili makuu ya mbegu ambayo ni:

Mbegu za asili za mpunga: Ni zile ambazo zimetumika miaka mingi katika historia ya kilimo. Kuna aina nyingi za mipunga ya asili inayolimwa sehemu mbalimbali hapa nchini kama Supa, Kahogo, Kula na Bwana, Shingo ya mwali, n.k. Wakulima wanazipenda mbegu hizi kutokana na kuwa na sifa kama vile ladha nzuri, uvumilivu wa matatizo mbalimbali ya kimazingira na kwa sababu ya uwezo wa mbegu hizi kustahimili katika hali mbaya ya hewa na hazihitaji uangalizi wa hali ya juu. 

Sifa hizi ni matokeo ya mbegu hizi kumudu mazingira na uchaguzi wa mbegu uliofanywa na wakulima kwa miaka mingi. Hata hivyo, nyingi ya mbegu hizi zina uwezo mdogo wa kuzaa, zinachelewa kukomaa, ni ndefu na rahisi kuanguka.

Mbegu zilizoboreshwa: Hizi ni zile zilizoboreshwa kutokana na mbegu za asili. Mfano wa mbegu zilizoboreshwa ni kama vile Katrin, IR54, na IR64. Zinazaa sana hasa kwa kilimo cha umwagiliaji. Hata hivyo, hazikidhi ladha ya walaji na ukobolekaji wake si mzuri na baadhi hazistahimili kwenye mazingira mengi ya kawaida. Hii imezifanya mbegu hizi kukubalika na wakulima kwa kiwango kidogo sana. 

Mbegu bora nyingine zilizozalishwa kutoka utafiti na kuonekana kupendwa kwa ajili ya mavuno mengi na ladha nzuri kama TXD88 na TXD85. Hivi karibuni imetolewa mbegu nyingine iitwayo TXD306 (SARO5), mbegu hii hupendwa na wakulima, wafanyabiashara na walaji kutokana na sifa yake ya mavuno mengi, punje ndefu kiasi na nzito, ladha nzuri na yenye kunukia pindi ipikwapo na kuliwa.

Mbolea za kupandia mpunga

Kabla ya kuweka mbolea hakakisha kuwa majaruba yanatengenezwa ili kuhakikisha maji hayaingii na kutoka kiholela. Mbolea ya kupandia huwekwa kwa kusia katika jaruba kabla ya kuchavanga. Kuchavanga husaidia kuchanganya udongo na mbolea na pia kutengeneza eneo zuri la kupandikiza miche. Baadaye miche hupandikizwa.

Viwango vya mbolea za kupandia mpunga

Kiwango cha mbolea za kupandia kilichopendekezwa ni kilo 20 phosphate (P) kwa hektari ambayo ni sawasawa na kiasi mifuko mitatu kwa hekta ya DAP (= mfuko mmoja kwa ekari), au mifuko miwili kwa hekta ya Minjingu Phosphate (= mfuko mmoja na nusu kwa ekari) au mifuko minne na nusu kwa hekta ya Minjingu Mazao (= mifuko miwili kwa ekari).


Jinsi ya kupanda mpunga Kitaalam

Kuna njia mbili kuu zinazotumika kupanda mpunga shambani. Njia hizo ni ile ya kupanda mbegu moja kwa moja shambani na ile ya kupandikiza miche.

 • Kupanda mbegu moja kwa moja

Njia hii hutumika kwa kupanda mbegu moja kwa moja kwenye shamba lililotayarishwa vizuri. Njia ya kawaida waitumiayo wakulima ni ile ya kumwaga na kufukia mbegu (broadcasting). Njia zingine ni zile za kupanda mbegu kwenye mashimo yaliyo kwenye mstari na kwa kuzingatia nafasi maalum au mbegu hupandwa kwenye mashimo bila kufuata mstari na bila kuzingatia nafasi iliyopendekezwa (dibbling). Vile vile mbegu hupandwa kwa kunyunyizwa kwenye vifereji vyenye vina vifupi na kufukiwa pasipo kuwa na nafasi kati maalum kati ya punje na punje (seed drilling)

 • Kupandikiza miche

Njia hii hutumika kwa kupanda mbegu kwanza kwenye kitalu kabla ya kuzihamishia shambani. Mara nyingi mbegu zetu hutumia wiki tatu hadi nne baada ya kuota kwenye kitalu na kufikia umri wa kupandikizwa shambani. Katika shamba la mpunga miche hupandikizwa shambani kwenye mstari na kwa nafasi maalum au kupandikizwa holela bila kuzingatia nafasi maalum za kupanda.

Inashauriwa kupandikiza miche katika kina cha sentimeta 2 hadi 3. Ukipanda kina kirefu machipukizi huchelewa kujitokeza. Baada ya kupandikiza miche, machipukizi hujitokeza baada ya siku 5 hadi 10.

Kupandikiza-mpunga
Kupandikiza miche ya Mpunga

Nafasi ya kupanda mpunga Mpunga

Nafasi ya kupanda mpunga mbegu bora ni sm 15 kwa sm 15 au sm 20 kwa sm 20. Kwenye mpangilio wa mistari miwili miwili (double rows), nafasi kati ya mistari miwili ni sm 10, nafasi kati ya mmea na mmea katika kila mstari ni sm 20, na nafasi kati ya mistari miwili na mistari miwili mingine (double rows) ni sm 40. Mbegu za asili zipandwe kwa nafasi ya sm 20 kwa sm 20 au sm 25 kwa sm 25 au sm 30 kwa sm 30.

Kupanda kwa nafasi ni kati ya njia bora za kilimo inayomwezesha mkulima kupata mazao bora. Hivyo ni muhimu sana kuzingatia kupanda kwa mistari na kufuata nafasi zinazoshauriwa na wataalamu wa kilimo.


Muda wa kupanda Mpunga

Muda wa kupanda unatofautiana kutoka eneo moja kwenda jingine kulingana na majira ya mvua. Kwa mfano katika wilaya ya Morogoro tarehe za kupanda ni kuanzia desemba hadi januari kwa mpunga wa muda mrefu. Kwa mpunga wa muda wa kati na muda mfupi, tarehe ya kupanda ni februari hadi machi.

Kupalilia Mpunga

Ni muhimu shamba lipaliliwe ili kuondoa magugu. Magugu ni mimea hivyo hushindana na mimea iliyopandwa na mkulima kwa kunyonya virutubisho ardhini. Magugu yanaweza pia kuhifadhi wadudu na magonjwa yanayoweza kushambulia mimea iliyopandwa na hivyo kupunguza mavuno.

Katika kilimo cha mpunga, ni muhimu shamba lipaliliwe siku 14 hadi 21 baada ya mimea kuota kufuatana na hali ya shamba wakati wa kupanda. Ni vizuri katika kilimo cha mpunga, shamba lipaliliwe mara mbili, kutegemeana na hali ya magugu katika shamba. Unaweza kupalilia kwa kung’olea kwa mkono, kwa mashine au kwa kutumua viua magugu (herbicides) kama vile 2, 4-D (Two Four D).

Utafiti unaonyesha kwamba, shamba la mpunga ambalo halijapaliliwa linaweza kupunguza mavuno kwa asilimia 60 hadi 100 ya mavuno yanayotarajiwa. Hata kama mkulima atatumia mbegu bora, aina na kiasi cha mbolea zinazoshauriwa, kupanda kwa mstari pamoja na mbinu nyingine bora zinazoshauriwa, bila kupalilia hali hii itaathiri mavuno yake.


Mbolea za kukuzia mpunga

Ni mbolea zinazotumika baada ya mimea kuota kwa lengo la kuikuza mimea ili itoe mavuno bora. Mara nyingi mbolea hizi zinatoa kirutubisho cha naitrojeni. Kiwango kinachopendekezwa ni kilo 60 naitrogeni kwa hektari, ambacho ni sawasawa na kiasi cha mifuko miwili ya UREA au Minne na Nusu Ya CAN au Mitatu ya SA. Mbolea inayotumika mara kwa mara ni Urea. Hata hivyo mbolea zingine kama SA inaweza kutumika kama kuna mahitaji ya salfa. CAN inaweza kutumika kama kuna mahitaji maalum ya nitrate na ammonium. Kwenye mpunga, mbolea ya kukuzia inawekwa wiki mbili baada ya kupandikiza miche na irudie tena baada ya wiki nne.

Kuweka mbolea: Mbolea ya kukuzia hutiwa kwa kusia wiki mbili baada ya kupandikiza, na kurudia mwezi mmoja baadaye. Ni vyema kuweka mbolea za kukuzia mara mbili ya kiasi kinachopendekezwa.

Shamba-la-Mpunga-uliopandikizwa
Shamba la mpunga uliopandwa kwa mistari

Kudhibiti Magonjwa na Wadudu Wanaoshambulia Mpunga

Magonjwa Yanayoshambulia Mpunga

Magonjwa ya mpunga yamegawanyika katika makundi matatu kulingana na vimelea visababishi ambavyo ni fungasi, virusi na bakteria.

i) Rice blast (Ukungu)

Unaosababishwa na Pyricularia oryzae.

Dawa/Kudhibiti: Mbegu bora inayostahimili ugonjwa, kupanda mapema, kung’oa mimea iliyoathirika ama kunyunyiza dawa za kuua ‘vectors’ kama vile inzi weupe (white flies).

ii) Brown leaf spot

Unaosababishwa na Helminthosporium spp.

Dawa/Kudhibiti: Panda mbegu kwa udongo unaofaa, weka mbolea ya kuzuia au tibu mbegu na dawa.

iii) Sheath rot

Unaosababishwa na Acrocylindrium oryzae.

Dawa/Kudhibiti: Kwa sasa hakuna njia ya kuzuia

iv) Rice Yellow Mottle Virus (RYMV) – Kimnyanga

Hivi karibuni ugonjwa wa kimyanga umetajwa kama ugonjwa hatari sana kwa mpunga hapa Tanzania.

Dawa/Kudhibiti: Panda mbegu zilizoboreshwa, zinazostahimili magonjwa au ng’oa mimea iliyoathirika.

Magonjwa yasababishwayo na bakteria nayo wametajwa kuwa na madhara makubwa kwa uzalishaji wa mpunga hapa nchini. Bakteria hawa wanajumuisha Acidovorax avenae subsp. Avenae asababishae ugonjwa wa bacterial stripe, Pantoea aglomerans, asababishae ugonjwa wa palea browning na Xanthomonas oryzae p.v. oryzae.


Wadudu wanaoshambulia mpunga

Kuna aina nyingi sana za wadudu wanaoathiri mpunga katika hatua mbalimbali za ukuaji wa mpunga. Wanapokithiri na wasipodhibitiwa hupunguza kiasi cha mavuno shambani.

i) White flies (Funza weupe)

Dawa/Kudhibiti: Nyunyiza dawa ya Thiodan, Endosulfan (Thionex), Fipronil (k.m. Regent 3G), Fenthion (k.m. Lebaycid)

ii) Rice stalk borer waharibifu

Kudhibiti: Nyunyiza dawa ya Thiodan, Endosulfan (Thionex), Fipronil (k.m. Re­gent 3G), Fenthion (k.m. Lebaycid) Ili mkulima aweze kupata mazao mengi na bora inashauriwa kutumia dawa za kuzuia magonjwa na wadudu wanaoshambulia mimea na njia zinginezo.


Kuvuna, Kukausha, Kusafisha na Kuhifadhi Mpunga

Kuvuna: Mpunga uko tayari kuvuna wakati asilimia themanini (80%) ya rangi ya mpunga kwenye masuke imebadilika na kuwa dhahabu. Mpunga unavunwa kwa kukata bua pamoja na suke lake.

Kuvuna-mpunga-kwa-siko

Uvunaji wa mpunga

Kukausha: Rundika pahali pakavu k.m. kwenye tuta la jaruba halafu pigapiga (thresh) ili kutenganisha masuke na mpunga. Kama mpunga hayajakauka vizuri hukaushwa zaidi juani kwa siku 3-4 ili kupunguza unyevunyevu kufikia kiwango kinachofaa kwa kuhifadhi (14%). Ni muhimu mpunga ukauke vizuri ili usioze ukiwekwa ghalani.

Kusafisha: Mpunga uliyokauka vizuri hupepetwa na vilevile mapepe huondolewa. 

Kuhifadhi: Mpunga safi huwekwa kwenye gunia na magunia kupangwa vizuri ghalani juu ya mbao yasiguse sakafu.

Je ungependa kupata Muongozo wa kilimo cha mpunga utakao kufahamisha gharama za uzalishaji na hatua zote za utunzaji wa mpunga? Wasiliana nasi ujipatie copy yako

Click to Tweet

Usipitwe na…

Acha comment yako hapa chini ili ku-share mawazo na wakulima wenzetu.

Categories: Mazao ya nafaka

Mtalula Mohamed

I like blogging. In order utilize my profession I chose to share, to blog, a few tips and tricks about farming and agriculture to anyone interested.

25 Comments

baraka john · September 4, 2017 at 4:28 pm

Maelezo mazuri sana

Johnson Said Mussa · March 19, 2018 at 12:24 pm

Nimefurahi kwa maelezo mazuri ya namna ya kulima mpunga. Nipo na andaa shamba, maelezo yamenipa mwongozo mzuri

  Mtalula Mohamed · March 19, 2018 at 8:45 pm

  Karibu sana, sio vibaya ukiwa unatupa mrejesho kadri unavyoendelea na mradi wako

   Saimon · January 10, 2019 at 1:22 pm

   Uko vizuri mtaalam Mungu akubariki

yusuph George · September 23, 2018 at 9:50 am

Naitaj kufaham Ni mbolea gan inashauliwa kutumika ili kurutubisha shamba kabla ya kupanda mmea wa mpunga..?

Elisha Jackson · November 1, 2018 at 10:59 pm

Toka mwaka jana nilianza kujihusisha na kilimo cha mpunga na sikupata mazao kutokana na kutokujua ratiba na muda gani wa kupanda na aina gani ya mbegu inatakiwa kupandwa na kwa muda gani. na mwezi huu wa kumi na moja 2018 nitaenda tena morogoro kufatilia mashamba naomba kuelekezwa je ni muda sahihi huu wa kuanza kulima maana safari hii nataka kulima kitalamu yaani mpunga wa kupandikiza,naomba msaada jamani.

  Mtalula Mohamed · November 4, 2018 at 9:18 am

  Mr Elisha huu ni muda sahihi Kwa Mpunga. Unachotakiwa ni kuanza shughuri za kuandaa kitalu na shamba. Unaweza pia kujipatia muongozo wetu wa kilimo cha Mpunga ili ujue hatua site za utunzaji wa Mpunga na gharama zake.

Mtalula Mohamed · November 4, 2018 at 9:19 am

Mr Elisha huu ni muda sahihi Kwa Mpunga. Unachotakiwa ni kuanza shughuri za kuandaa kitalu na shamba. Unaweza pia kujipatia muongozo wetu wa kilimo cha Mpunga ili ujue hatua site za utunzaji wa Mpunga na gharama zake.

  Moro Sauti · November 6, 2018 at 5:46 am

  Nakupongeza sana Class mate wangu Mtalula kwa elimu unayoitoa
  Keep it up.

   Mtalula Mohamed · November 9, 2018 at 10:20 am

   Shukrani sana kaka Moro Sauti. Naomba unisambazie ujumbe huko uliko

    augustino mshoro · January 20, 2019 at 6:23 pm

    nisaidie no yako tafadhar

     Mtalula Mohamed · January 29, 2019 at 2:21 pm

     Karibu sana Mr Augustino, 0655570084

Isaack Mbalale · November 15, 2018 at 10:33 am

Shukran Ndugu Kwa Elimu Unayoitoa.

frank ngowi · December 17, 2018 at 5:55 pm

nahitaji mbegu ya kisasa inayozaa sana ntaipataje no ni 0763777779

  Mtalula Mohamed · December 18, 2018 at 2:42 pm

  Unaweza kuitafuta Saro 5, ni mbegu inayosifiwa sana na wakulima kwa kuzaa sana. Nenda ASA (Agricultural Seed Agency) Morogoro, wanayo hii mbegu

   Aminaeli kajewa · December 19, 2018 at 12:00 pm

   Hekta moja yaweza to a gunia ngapi!?
   Na je naweza tumia kiasi gani cha mbegu ya saro 5 kwa hekta!?

    Mtalula Mohamed · January 12, 2019 at 11:33 am

    Mavuno ya gunia 25 mpaka 40 yameripotiwa na wakulima mbalimbali. Unaweza kutumia kg30 mpaka 40 kwa hekta moja

Celestine · January 9, 2019 at 3:46 pm

Congratulation men, it is a nice guide

Rehema obathus · January 24, 2019 at 9:44 pm

Mr mtalula ni wakati gani napaswa kutumia dawa ya kuua magugu kwenye mpunga?

  Mtalula Mohamed · January 29, 2019 at 7:54 am

  Unapoona magugu yanakua kwa kasi kuliko unavyoweza kudhibiti. Mwezi mmoja baada ya kupandikiza mpunga, unaweza kupiga dawa ingawa unatakiwa uzingatie pia kasi ya ukuaji wa magugu kwenye shamba lako

Noel Albano · January 26, 2019 at 9:33 am

Nahitaji kulima mpunga lkn pia nimepata maelezo yenye ufumbuz ktk nililo kuwa nataka kulifanya lkn ,naomba msaada nimbegu ipi ambayo no nzur kwa kipato nahata kibiashara:?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *