May 15, 2023

Kilimo cha Viazi mviringo na Faida zake kwa Wakulima Tanzania

Nchini Tanzania viazi mviringo (Solanum tuberosum) vina majina mengi, wengine huviita viazi ulaya wakimaanisha vinaasili ya Ulaya (English: Irish Potato) na wengine huviita viazi mbatata.

Kilimo cha viazi mviringo ni muhimu kwa usalama wa chakula, kuboresha lishe, ajira na kuongeza kipato nchini Tanzania.

Viazi mviringo ni miongoni mwa mazao makuu kumi ya chakula nchini Tanzania, na ni zao la tatu baada ya mahindi na mpunga kiuzalishaji. Kiasi kikubwa cha viazi mviringo kinazalishwa katika ukanda wa nyanda za juu kusini unaojumuisha mikoa ya; Njombe, Mbeya, Songwe na Iringa.

Jumla ya tani 337,803 za viazi mviringo zilizalishwa nchini mwaka 2018/19, kati ya hizo, tani 282,404 (83%) zilitoka Nyanda za Juu Kusini (Wizara ya Kilimo, 2019).

Mkoa wa Mbeya ndio unaoongoza kwa uzalishaji wa viazi mviringo nchini kwa 49.8%, ukifuatiwa na Njombe 19%, Iringa 10.8% na Songwe 3.9% katika msimu wa mazao wa mwaka 2018/19.

Kwa nyanda za juu kusini na kaskazini mwa Tanzania, mavuno ya viazi mviringo ni makubwa ukilinganisha na mazao mengine ya chakula kama mahindi.

Viazi mviringo vinaweza kulimwa mara 3 kwa mwaka kila baada ya miezi 3-4 ukilinganisha na zao la mahindi linalochukua miezi 10-12 kwa baadhi ya maeneo.

Viazi mviringo
Viazi mviringo

Mahitaji ya kiikolojia

Udongo

Kilimo cha viazi mviringo kinahitaji udongo mwepesi, wa-kichanga, au tifutifu na usiotuamisha maji. Udongo uwe na uwezo wa kupitisha hewa kwa urahisi na kufanya viazi kutanuka na kustawi vizuri. Lakini pia uwe na rutuba ya kutosha. Udongo mzito (wa mfinyanzi) sio mzuri kwa kuwa hauruhusu kukua kwa mizizi na kutanuka kwa viazi, na hivyo kupelekea viazi kuwa na maumbo mabaya (deformed shapes).

Uchachu wa udongo unatakiwa uwe kati ya pH 5 na 6.5 ili kurahisisha upatikanaji na matumizi ya viinilishe vya mmea. Udongo ulio na uchachu wa chini ya Ph 5 unatakiwa kurekebishwa kwa kuweka madini ya chokaa (Calcium Carbonate) kiasi cha Kg 400 kwa ekari moja.

Angalizo: Kila unapovuna mazao kuna kiasi cha viinilishe vinavyopotea (kutoka kwenye udongo) hivyo ni muhimu kupima na kujua afya ya udongo wa shamba lako. Matokeo ya tafiti ya udongo ndio mwongozo wa kiasi na aina ya mbolea inayotakiwa.

Hali ya hewa

 • Mwinuko na Joto

Viazi mviringo vinastawi vizuri sana kwenye maeneo yenye mwinuko wa kati ya mita 1700 na 3000 kutoka usawa wa bahari. Na hii ndio sababu maeneo yanayoongoza kwa uzalishaji wa viazi mviringo hapa Tanzania ni yale yaliyo katika miinuko.

Zao hili linahitaji hali ya hewa ya baridi na linaweza kuitwa zao la kipupwe. Joto linalofaa zaidi ni kuanzia nyuzi-joto 100C mpaka nyuzi-joto 260C.

Kwa mfano, maeneo ya Nyanda za Juu Kusini katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe na Rukwa. Na kwa upande wa kaskazini mikoa ya Manyara, Arusha, Tanga, Kilimanjaro na Mara. Na mko wa Morogoro baadhi ya maeneo.

Zao la viazi mviringo linahitaji mvua kiasi cha milimita 900 mpaka 1400 kwa kipindi cha miezi mitatu ili vistawi vizuri. Hata hivyo mvua ya wastani wa milimita 450 katika kipindi chote cha uzalishaji inaweza kustawisha viazi mviringo.

Uchaguzi wa shamba

Shamba la kupanda viazi mviringo linatakiwa lisiwe limepandwa viazi mviringo au mazao jamii ya viazi kwa kipindi cha msimu msimu mmoja (kwa viazi vya chakula) na angalau miaka mitatu iliyopita (kwa viazi vya mbegu).

Mazao jami ya viazi (Solanaceous crops) ni kama; nyanya, biringanya, pilipili hoho, mnavu, nyanya chungu, n.k. Mazao haya hushambuliwa na magonjwa na wadudu wale wale wanashambulia viazi mviringo. Hivyo kupanda viazi mviringo kwenye shamba lililovunwa mazao jamii ya viazi kutapelekea kuzaliana zaidi kwa vimelea vya magonjwa hayo.

Mfano; ugonjwa wa bakteria mnyauko (bacterial wilt) huathiri sana mazao jamii ya viazi kwa hivyo yanachangia magonjwa kwenye viazi mviringo vikipandwa kwa kurudia kwenye shamba moja au kwa misimu iliyofuatana na mazao jamii ya viazi.

Jinsi ya kuandaa shamba

Shamba kwa ajili ya kilimo cha viazi mviringo linatakiwa lisafishwe mapema, kabla ya mvua kunyesha na kulingana na ukanda na hali ya hewa ya eneo husika. Baada ya kusafisha shamba kinachofuata ni kukatua (ploughing) na kupiga halo (harrowing). Shamba likatuliwe kwa kina cha sentimeta 30 mpaka 45 sawa na futi moja mpaka moja na nusu (rula 1 – 1.5).

Lengo la kukatua ni kuchanganya udongo, kuchimbua magugu, kufanya udongo upitishe maji na hewa kirahisi na kuchanganya mabaki ya mazao ya msimu uliopita na udongo.

Lengo la kupiga halo (harrow) ni kuvunja-vunja mabonge ya udongo hivyo kufanya udongo kuwa laini na kukatakata magugu magugu yaliyolichimbuliwa shambani.

Upandaji wa viazi mviringo

Uchaguzi wa mbegu bora

Aina za Mbegu za Viazi Mviringo

Kuna aina nyingi za viazi mviringo nchini Tanzania. Baadhi ya mbegu za viazi mviringo zilizotolewa rasmi kulingana na utafiti na kuandikishwa kwa matumizi nchini Tanzania ni Sherekea, Asante, Meru, Tengeru, Sagitta, Rumba na Jelly.

Kilimo bora cha viazi mviringo kinaanza na matumizi ya mbegu bora. Tunashauri uchague aina ya mbegu inayotoa mavuno mengi na inayovumilia magonjwa, wadudu na ukame.

Aina tofauti za viazi mviringo zina matumizi tofauti kwenye masoko ya mijini na vijijini. Chagua mbegu kulingana na madhumuni ya mazao yatakayovunwa, kwa mfano kusindika, mbegu, chakula na kadhalika.

Sifa za Mbegu Bora za Viazi Mviringo

Mbegu bora za viazi mviringo zinatakiwa ziwe na sifa zifuatazo:

 • Aina inayotambulika na isiyochanganyika na aina nyingine
 • Isiyokuwa na michubuko, kidonda, magonjwa au wadudu wa aina yoyote
 • Iwe imepitia hatua zote za uzalishaji mbegu bora
 • Iwe na ukubwa wa wastani unaolingana na ukubwa wa yai la kuku (milimeta 35)
 • Zenye kutoa mavuno mengi zaidi kutoka kwenye shina moja
 • Zitoke katika aina ambayo haishambuliwi na magonjwa kama vile ukungu na mnyauko
 • Iwe imechipua vizuri na iwe na machipukizi zaidi ya manne yenye afya.

Uandaaji wa Mbegu Bora kwa ajili ya Kupanda

 • Chagua mbegu yenye ukubwa wa milimeta 35 hadi 45 (ukubwa wa yai). Hii itatoa viazi mviringo vyenye ukubwa wa uwiano mzuri; vikubwa, kati na vidogo wakati vikikomaa.
 • Mbegu ya viazi mviringo inatakiwa ichipushwe (pre-sprout) mapema ili iote mapema na kwa wakati mmoja kuepuka uwezekano wa kushambuliwa na magonjwa na wadudu.

Kiasi cha Mbegu kwa Ekari

Kwa mbegu ya ukubwa wa milimita 35-45, utahitaji kilo 800 hadi 1000 kwa ekari moja. Mkulima atatumia kilo 1200 kama mbegu zina ukubwa wa milimita 45 hadi 55. Endapo mkulima atatumia mbegu ya ukubwa wa chini ya milimita 35 atatumia kilo 400 hadi 600 au gunia 4 hadi 6 kwa ekari moja.

Msimu wa kupanda viazi mviringo

Msimu wa kupanda viazi mviringo unatofautiana kati ya sehemu na sehemu. Tunashauri uanze kupanda wakati kuna unyevu wa kutosha. Madhara ya kupanda wakati wa ukame ni: kupotea kwa virutubisho katika mbolea hususani naitrojeni, viazi kupoteza maji, kunyauka na kushindwa kuota, viazi kushambuliwa na magonjwa na wadudu waharibifu kabla ya kuota.

Hii husababisha uotaji mbaya na hatimaye uzalishaji mdogo. Viazi vinaweza kupandwa hata wakati kuna upungufu wa mvua kwenye mazingira ambayo mvua ni chache, lakini ni sharti mkulima afanye jitihada za kumwagilia.

Jinsi ya kupanda viazi mviringo

Kuna njia mbili kuu za kupanda viazi mviringo. Njia hizi ni kupanda kwa matuta na kupanda kwa sesa. Kwa uzalishaji mzuri wa viazi mviringo, tunashauri utumie njia ya matuta.

Mavuno mazuri ya viazi mviringo yanatokana na matumizi ya mbinu bora za kilimo kwa vile;

 • Kutumia mbegu bora na safi (zisizo na magonjwa), na zenye umri wa miezi 3 hadi 5.
 • Umakini wakati wa kupanda na kutumia nafasi zinazoshauriwa,
 • Kupalilia na uwekaji wa matuta wakati wa kupanda na kuinulia matuta baadaye wakati wa palizi.
 • Matumizi ya mbolea kulingana na vipimo vinavyooshauriwa kulingana na vipimo vya udongo wa eneo husika.

Ni vizuri wakulima kushiriki majaribio shirikishi ili wajifunze namna ya kufanya shughuli za upandaji wa viazi.

Nafasi ya kupanda viazi mviringo

Nafasi ya kupanda inategemea aina ya mbegu, lengo la mavuno, hali ya udongo na zana zinazotumika kupandia. Nafasi ya kupanda viazi vya chakula ni SM 75 mapaka 80 kwa SM 30. Kina cha shimo ni SM 10 hadi 15. Nafasi ya kupanda viazi vya mbegu ni SM 60 mpaka 75 kwa SM 20 mpaka 25. Kina cha shimo ni SM 10 hadi 15.

Shamba la viazi mviringo
Shamba la viazi mviringo

Mbolea za kupandia viazi mviringo

Mbolea za kupandia viazi mviringo ni DAP, TSP na/au Minjingu phosphate. Kwa zao la viazi mviringo, tunashauri utumie Kg 100 (hadi 150) za DAP kwa ekari. Mbolea hii iwekwe kwa kiwango cha gramu 5 hadi 10 kwa kila shimo kisha ifukiwe na udongo kidogo ili kuepuka mbegu kugusana moja kwa moja na mbolea.

Hata hivyo unaweza kuchanganya mbolea ya kupandia na ya kukuzia halafu zote ukaziweka wakati wa kupanda. Lau utafanya hivyo, basi changanya Yara Mila Winner Kg 100 na Kg 50 za DAP kwa ekari. AU changanya Kg 100 za TSP (ama DAP) na Kg 100 za CAN kisha uziweke Pamoja.

Hii ni kwasababu tafiti hazioneshi utofauti kiuzalishaji ikiwa mbolea hizi zitawekwa katika nyakati tofauti au zote zitawekwa wakati wa kupanda.

Utunzaji Shamba la viazi mviringo

Udhibiti wa magugu

Palizi kwa Jembe la Mkono

Kwa kawaida magugu huondolewa kuzuia ushindani na zao kwenye maji, mwanga, rutuba na nafasi vinavyosababisha kupungua kwa mavuno.

Zao la viazi mviringo linatakiwa lipaliliwe kuanzia ya wiki 3 hadi 4 baada ya kupanda (au wiki 1 hadi 2 baada ya kuota) kutegemeana na hali ya hewa au magugu yanapojitokeza.

Jembe la mkono linafaa kwa palizi kwa vile linaweza kuondoa aina zote za magugu. Palizi hii inafaa ifanyike kabla ya viazi mviringo kuanza “kutaga”, kuepuka kukata viazi vidogo vinavyotanua.

Matuta yatengenezwe mara baada ya kupanda na wakati mkulima anafanya palizi ya kwanza aongeze udongo na kutengeneza matuta makubwa wiki ya 4-5 baada ya kuota.

Matuta ni muhimu kwa sababu zifuatazo:

 • Matuta huzuia viazi mviringo kupigwa na mwanga wa jua na kuwa na rangi ya kijani,
 • Matuta huzuia viazi kushambuliwa na nondo wa viazi na
 • Matuta husaidia kupunguza madoa ya kahawia yanayosababishwa na joto nyingi kwenye udongo.

Angalizo: Viazi mviringo vilivyopandwa kitaalamu vinafunika eneo lote na kuzuia uotaji wa magugu hasa wiki sita baada ya kupanda. Kama vimepandwa kwenye matuta suala muhimu ni kuondoa magugu na kusogeza udongo kwenye mashina.

Palizi kwa Kutumia Viuagugu

Kabla ya kupanda viazi: Viuagugu vinavyotumika kabla ya kupanda ni Paraquat na Glyphosate, mfano: Gramaxone, na Round up. Viuagugu hivi vipigwe wakati magugu yana ukijani na sio yakiwa makavu. Na lengo la kutumia viuagugu hivi ni kusafisha shamba kwa kuwa vinaua aina zote za magugu shambani hata kama kuna mazao (yote yatakufa).

Baada ya kupanda viazi:

Kabla viazi havijaota: unaweza kutumia viuagugu vya kuzuia magugu kuota kama vile: Pendimethalin na Acetoclor; AU viuagugu vya kuua aina zote za magugu (kama magugu yamewahi kuota) kama vile: glyphosate na paraquat.

Baada ya viazi kuota: unaweza kupiga viuagugu chaguzi ambavyo vitaua magugu pekee na kuacha viazi vikiwa salama. Navyo ni vile vinavyoua magugu aina ya nyasi (grass, poaceae family) mfano; Fusillade forte.

Angalizo: Mkulima atumie kanuni bora kama vile kusoma vifungashio jinsi ya kutumia viuatilifu hivi, kutumia vipimo vilivyo pendekezwa na kutumia zana za kujikinga wakati wakutumia viuatilifu hivi.

Mbolea za kukuzia viazi mviringo

Mbolea za viwandani

Mbolea za kukuzia viazi mviringo ni zile ambazo zinatoa virutubisho vinavyochochea kasi ya ukuaji wa viazi mviringo kufikia uzaaji nazo ni zile zenye kirutubisho cha naitrojeni (N). Miongoni mwa mbolea nyingi za kukuzia ni kama vile; Urea, Amidas, CAN, NPK, Yara Mila Winner, n.k.

Kwa ajili ya kukuza viazi mviringo tumia Kg 100 za NPK (17:17:17) (au Yara Mila Winner, au CAN) kwa ekari moja. Na mbolea hii iwekwe wiki nne baada ya viazi kuota.

Tunashauri mkulima atumie Muriate of Potash (MOP) kama udongo una kiwango kidogo cha kirutubisho aina ya Potasium. Mazao ya mizizi hutumia zaidi Potashium (K) kuliko Naitrojeni (N) na Fosforasi (P), kwa hiyo ni muhimu kutumia angalau kilo 20 za Potashium kwa ekari.

Haifai kutumia mbolea za nitrogen (yaani Urea, CAN, Amidas) zaidi ya kiwango kilichopendekezwa kwa sababu inasababisha majani ya viazi mviringo kuwa makubwa na viazi kuwa vidogo vidogo.

Angalizo: Hakikisha unatumia viwango sahihi vya mbolea. Na njia sahihi ya kujua upungufu wa virutubisho kwenye udongo ni kupima udongo wako. Pima udongo!

Shamba la viazi mviringo vilivyostawi vizuri
Shamba la viazi mviringo vilivyostawi vizuri

Mbolea za Asili

 1. Samadi: Mbolea hii inatokana na masalia ya Wanyama tunaowafuga majumba; kama vile ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku, nguruwe, farasi, n.k. Mabaki haya ni pamoja na kinyesi, mkojo, matandiko na mabaki ya malisho. Kwa maeneo ambayo samadi inapatikana matumizi ya tani 10 ya samadi iliyooza vizuri kwa ekari itasaidia uzaaji mzuri wa viazi mviringo na mazao mengine yatakayofuata kwenye kilimo mzunguko (crop rotation).

Mbolea za asili zina kiwango kidogo cha virutubisho ukilinganisha na zile za viwandani kwa hivyo unahitaji tani nyingi kwa ekari moja kufikia kiwango kinachohitajika.

 1. Mbolea ya mboji: Mboji inatengenezwa kwa kutumia mchanganyiko wa masalia ya mimea, matawi ya yaliyodondoka, magugu, majivu na takataka zingine za nyumbani. Ikiwezekana, ongeza samadi kwa kiasi kidogo wakati wa utengenezaji wa mboji. Ikiwa utahitaji kujifunza zaidi kuhusu mbolea ya mboji soma kwenye makala niliyo-link hapa.

Angalizo: Samadi na mboji bora ni ile iliyoozeshwa vizuri kwa kutunzwa na kuhifadhiwa kivulini. Usitumie plastiki ama vipande vya chuma kutengeneza mboji.

Wadudu wanaoshambulia Viazi mviringo

Nondo wa viazi mviringo

Nondo wa viazi mviringo wanashambulia viazi kuanzia vikiwa shambani na kwenye ghala. Wameenea zaidi kwenye maeneo yenye uvuguvugu, ukavu na yenye miinuko.

Funza wa nondo wa viazi mviringo wanatoboa kwenye ncha ya mmea mpaka kwenye shina, majani, vikonyo na viazi vyenyewe hasa wakati wa ukame.

Uharibifu mkubwa unaosababishwa na funza wa nondo ni vitobo au vishimo kwenye viazi vinavyosababisha mashambulizi ya magonjwa ya ukungu na bacteria na kupelekea viazi kuoza.

Kudhibiti na kutibu

Kutumia njia za asili

 • Kupanda kwa wakati; nondo huathiri zaidi viazi mviringo vilivyopandwa kipindi ambacho sio msimu wa kupanda. Panda viazi mviringo kwa msimu na kina kilichopendekezwa, cha zaidi ya sentimeta 3 kwani funza wa nondo hawawezi kuchimba kina kirefu.
 • Kutengeneza matuta kadri viazi mviringo vinavyokua na kufunika viazi mviringo na udongo. Matuta yanasaidia kuzuia nondo kutaga mayai kwenye viazi mviringo. Funza wanapoanguliwa huingia ndani ya viazi mviringo na kusababisha kuoza na pia wanakaa ndani ya viazi mviringo vilivyohifadhiwa ghalani.
 • Usafi wa shamba; teketeza viazi mviringo ambavyo havifai kwa matumizi, ondoa mimea mbadala na maotea ya viazi mviringo.
 • Kiuatilifu mbadala; matumizi ya mimea inayofukuza wadudu kwa mfano: Lantana Camara inasaidia hasa viazi mviringo vilivyohifadhiwa ghalani.
 • Kuondoa viazi mviringo haraka baada ya kuvuna. Viazi mviringo vilivyovunwa vinatakiwa viondolewe haraka kuepuka nondo kutaga mayai juu yake.

Matumizi ya viuadudu

Puliza viuadudu kwa mfano Karate 5EC, Karate 5CS, na Match 050EC. Nondo hutaga mayai wakati mmea ukiwa na maua, hivyo ni vema kupiga viuatilifu wakati huo.

Wadudu Mafuta [Vidukari: Aphids]

Mdudu mafuta ni mdudu mharibifu zaidi kati ya wadudu wanaoeneza magonjwa kwenye zao la viazi mviringo. Wadudu mafuta wenye mabawa wanaruka umbali mrefu kwa kusaidiwa na upepo. Wanashambulia majani, maua, mashina na machipukizi.

Kwa kawaida husababisha majeraha kwenye mmea hasa wale wanaoeneza ugonjwa wa virusi. Wanafyonza utomvu wa mmea, wanaudhoofisha na kuambukiza magonjwa ya virusi. Makundi (colonies) yao yanaweza kutambuliwa kwa urahisi kwenye ncha ya mimea na chini ya majani.

Njia za kudhibiti

 • Panda mbegu safi.
 • Hifadhi wadudu rafiki ni muhimu katika kudhibiti udaka/wadudu mafuta.
 • Kagua shamba mara kwa mara.
 • Chagua maeneo ya uzalishaji yenye joto la chini, mvua ya kutosha na upepo mkali. Maeneo haya huwa na wadudu mafuta/udaka wachache.
 • Ndani ya eneo la uzalishaji viazi elekeza shamba unapotokea upepo kuanzia mashamba ya biashara na yenye mazao mengine jamii ya viazi ili kupunguza kuenea kwa virusi kupitia wadudu mafuta ambao hubeba virusi.
 • Zuia mimea michanga isishambuliwe na udaka. Virusi vinavyotokeza mwanzoni mwa msimu kwa mimea michanga huwa chanzo cha maambukizi kwa mimea mingine kwenye msimu.
 • Vuna mbegu za viazi siku 8 hadi 10 baada ya kushambuliwa na wadudu mafuta au maambukizi ya virusi yakionekana, kuepuka maambukizi kwa kuwa virusi vinahitaji muda kushambulia viazi.
 • Ondoa magugu yote yenye maua ya njano ambayo huvutia udaka na mimea mingine inayobeba wadudu ndani ya shamba na kuzunguka shamba.
 • Kinga viazi mviringo wakati wa kuhifadhi kwa kuzuia kupata udaka.
 • Teketeza mimea iliyoathirika na magonjwa.
 • Bidhaa za muarobaini ni muhimu katika kupunguza uwingi wa udaka kwenye viazi mviringo.
 • Bidhaa za magugu ya Artemisia vulgaris zimeonekana kuwa na sumu ya kuua udaka (Metspalu and Hiiesar, 1994).
 • Tumia dawa kama Actara 25WG, Match 050EC, Dyanamec 018EC na Karate 5SC mara uwaonapo wadudu.

Nzi weupe

Hawa ni wadudu ambao kwa kawaida wanaonekana chini ya majani ya mmea wakifyonza utomvu. Wanaeneza magonjwa ya virusi kama virusi vya viazi mviringo X (PVX), virusi vya kusokota majani ya viazi viringo (PLRV), virusi vya viazi mviringo Y (PVY), virusi vya viazi mviringo A (PVA) na virusi vya viazi mviringo S (PVS). Angamiza wadudu hawa kwa kutumia viuadudu mfano Actara 25WG, Karate 5EC.

Sota [Viwavi: Cutworms]

Wadudu hawa wanakaa chini ya udongo karibu na mimea ambapo wanatembea na kukata mashina kwenye usawa wa udongo mara tu yanapochomoza hasa wakati wa kiangazi.

Sota/viwavi wanakula majani ya viazi mviringo na kusababisha majeraha ambayo yanaruhusu vimelea vya magonjwa kama bakteria yanayosababisha magonjwa ya kuoza. Mashina ya viazi mviringo yanajeruhiwa chini au juu ya usawa wa udongo.

Funza wa sota/kiwavi wanakula majani ya mimea na kuingia ardhini na baadaye kuwa vipepeo. Wanadhibitiwa kwa kupulizia viuatilifu vya mguso na vinavyopenya mfano Karate 5EC na Match 050EC mara tu dalili za uharibifu zinapoonekana.

Mafeng’enesi [White grubs – Phyllophaga spp]

Mafeng’enesi ni funza wa mdudu aitwae Beetle (June beetle, May beetle, na Japanese beetle). Wadudu hawa hushambulia miche na kukata, pia hushambulia sana kiazi chenyewe, huvikata na kutafuna hivyo kuharibu ubora na kupunguza mavuno. Funza hawa hujitokeza kwenye mashamba yenye mabaki ya mazao yaliyokauka na kubaki muda mrefu shambani.

Njia za kuthibiti mafeng’enesi

Njia za asili

 • Kuvuna mapema kuepuka uharibifu katika viazi mviringo.
 • Kuzuia na kuondoa magugu ili kupunguza utagaji wa mayai.Kulima mapema kwa kina kirefu na kupindua udongo ili kuwaleta wadudu juu, maana jua, ndege na wadudu wengine huwashambulia na kuwala.
 • Tumia wadudu rafiki kama nyigu (parasitic wasps) and pyrgotic flies.
 • Epuka kupanda viazi mviringo katika shamba lililoshambuliwa na mafeng`enesi msimu uliopita.

Kutumia viuadudu

Ni vigumu sana kuangamiza wadudu hawa maana huenda chini ya udongo mita moja. Tumia Karate 5EC na Karate 5CS ili kuwazuia, piga kuzunguka shina chini ya udongo, kuua lava na kuangamiza vikobe (beetles) watagao mayai. Muunganiko wa njia hizi zote huleta matokeo mazuri zaidi.

Kanitangaze [Nondo wa nyanya: Tuta absoluta]

Kantangaze ni mdudu mharibifu anayeshambulia viazi mviringo na mazao mengine kama nyanya, pilipili hoho, bilinganya n.k. Kanitangaze anaweza kuenea kwa kutumia mbegu iliyoathirika, kutoka mmea hadi mmea, mabaki yaliyopo shambani pia yanaweza kuathiri mazao mapya yatakapopandwa.

Njia za kudhibiti

 • Tumia mbegu ambayo haijaathirika.
 • Tumia kilimo mzunguko na mazao ambayo siyo ya jamii ya viazi mviringo.
 • Zingatia usafi wa shamba kwa kuteketeza mabaki yote ya mazao na magugu ambayo yanaweza kuhifadhi huyu mdudu.
 • Tumia kemikali kama Match 050EC, Dynamec 018EC, Belt plus Imidac, Abamectin na muarobaini, (Azadracta indica) mara baada ya kuona dalili za uvamizi wa mdudu huyu kwa kuona michirizi ya ukwanguaji wa majani.

Magonjwa hatari ya Viazi mviringo

Bakajani Chelewa [Late blight: Phytophthora infestans]

Bakajani Chelewa ya viazi mviringo, inayosababishwa na kiumbe kama kuvu, ni tishio la mara kwa mara popote ambapo viazi mviringo hukuzwa. Shamba nzima (100%) inaweza kusafishwa kwa muda mfupi usipodhibiti. Uchaguzi wa mbegu safi, yenye afya na ilivyothibitishwa ni muhimu. Pia kuondoa mabaki ya mizizi kutoka mazao ya msimu uliopita.

Dalili za Ugonjwa

Ugonjwa huu unaonekana zaidi kwenye majani, shina pamoja na viazi vyenyewe. Kwenye shina mashambulizi yanaonekana zaidi kama viazi mviringo vimepandwa miezi yenye unyevu na mvua nyingi. Joto la nyuzi kati ya 100C na 250C na mvua nyingi au umande huufanya ugonjwa huu kutokea kwa urahisi.

Ugonjwa husambaa kwa kasi na kuua idadi kubwa ya majani wakati wa mawingu, baridi na unyevu. Ukungu mweupe huonekana chini ya majani yaliyoshambuliwa. Michirizi yenye kahawia iliyokolea au zambarau huonekana kwenye kingo, vikonyo au ncha ya majani ya chini. Mmea mzima unaweza ukafa katika siku chache.

Njia za kudhibiti Bakajani Chelewa (Late blight)

 1. Ondoa maotea yote ya mimea na uyafukie au kuchoma.
 2. Panda mbegu yenye ukinzani na Bakajani Chelewa.
 3. Epuka kupanda maeneo yenye matatizo ya ugonjwa yanayokuwa na unyevu muda mrefu au ambayo ni vigumu kupuliza dawa.
 4. Epuka kumwagilia maji mengi nyakati za jioni.
 5. Ondoa masalia ya viazi mviringo. Inaweza ikawa chanzo cha ugonjwa msimu unaofuata.
 6. Kagua shamba mara kwa mara; hasa maeneo ya chini yenye unyevu, pembeni ya miti, katikati ya shamba na maeneo mengine.
 7. Endelea kupuliza dawa za ukungu kwenye majani kwa kuzingatia ratiba.
 8. Pindi Bakajani Chelewa inapoonekana ni dawa za ukungu/fangasi tu ndiyo zinaweza kudhibiti ugonjwa

Kudhibiti kwa njia ya viuakuvu na njia za asili

Kudhibiti kwa njia za viuatilifu

Matumizi ya viua kuvu (dawa za ukungu) vyenye kutibu ukungu ni ya lazima mara mmea uotapo. Zinazopendekezwa ni Ridomil, Dithane 45, Bravo, Funguran, Milraz. Tambua kuwa mara uonapo dalili za ugonjwa kwa macho ni kipindi ambacho ugonjwa umeshashambulia sana zao lako kwa ndani hivyo umeshachelewa kuudhibiti.

Ni muhimu kuwa na mpangilio sahihi wa unyunyizaji wa sumu za kuzuia na kutibu magonjwa ya ukungu kila wiki lakini (kwa) kutegemeana na hali ya hewa ili kulinda na kuendeleza afya na uhai wa zao lako.

Mfano: Ili kuzuia ugonjwa wa ukungu tumia Ridomil. Changanya gram 100 za kiuatilifu hiki na lita 20 za maji na unyunyuzie baada ya kila wiki mbili au tatu kutegemeana na hali ya hewa.

Kama ni Karate; nyunyizia kiasi cha mililita 20 hadi 40 za kiuadudu katika lita 20 za maji ili kuzuia wadudu kama nzi weupe na wengine.

Tumia vifaa vya kujikinga wakati wote unapotumia sumu za kudhibiti magonjwa na wadudu. Tahadhali za matumizi ya viuatilifu nimeziandika kwa kina kwenye makala hii.

Namna ya kudhibiti kwa njia za asili

 • Tumia mbinu bora za kilimo kama usafi wa shamba na kilimo mzunguko. Usipande viazi mviringo sehemu moja kila msimu au palipolimwa mazao jamii ya viazi kama nyanya, biringanya na aina zote za pilipili na nyanya chungu.
 • Zingatia ratiba ya umwagiliaji (epuka kumwagia jioni sana). Tumia nafasi sahihi ya upandaji hupunguza nafasi ya mimea kuwa na unyevu muda mwingi na kugusana na udongo hivyo kupunguza kuenea kwa magonjwa.
 • Epuka kufanya kazi shambani mimea ikiwa na unyevu.

Angalizo: Ni vema kupiga dawa za ukungu kabla ya kuona dalili za ugonjwa. Ni vigumu kuepuka matumizi ya viuakuvu kwa kuwa kuna hatari ya kupoteza mazao yote. Sumu nyingi za kuvu hutumiwa kama kinga. Baadhi hufanya kazi kwa kuingia ndani ya mmea, ilhali nyingine huwa juu juu kwenye majani, kwa lengo la kuuzuia kustawi kwa ugonjwa huo.

Bakajani Wahi (Early Blight)

Bakajani wahi hushambulia majani na mashina ya viazi mviringo na kuzifanya sehemu zilizoshambuliwa kuwa kavu na zenye rangi ya udongo mfano wa duara.

Njia za kudhibiti Bakajani Wahi

Njia hizi ni sawa na zile za kudhibiti Bakajani Chelewa.

Angalizo: Viuakuvu vyenye kiambata amilifu mfano Metalaxyl, Mandopro-mid Difenaconazole vina uwezo wa kutibu tatizo. Mfano Ridomil Gold 68 WG MZ, Revus Top 250 CS na Score 250 EC.

Viuakuvu vya kuzuia ugonjwa huu ni vyenye kiambata amilifu kama Chlorothalonil, Mancozeb, Azoxystrobin, Mandipro-pamid Difenaconazole.

Mfano: Ortiva 250 CS, Daconil 720 CS, Score 250 EC, Revus Top 250 SC na Ridomil Gold 68 WG MZ. Puliza dawa za ukungu/fangasi mara kwa mara.

Matumizi ya mbinu shirikishi (IPM)

Hii inahusisha mjumuiko wa mbinu tofauti kama vile:

 • Matumizi ya mbegu zenye ukinzani wa magonjwa.
 • Matumizi kidogo ya viuatilifu.
 • Usafi wa shamba; uondoaji wa mabaki shambani baada ya kuvuna pamoja na kung’oa maotea yanayojitokeza shambani kati ya msimu na msimu.
 • Kuondoa viazi vyenye ugonjwa wakati wa kuvuna na katika ghala.
 • Kuzuia mashambulizi ya viazi mviringo vikiwa shambani kwa kutengeneza matuta.
 • Kukata majani wiki mbili au tatu kabla ya kuvuna.

Bakteria Mnyauko / Kinyausi

Ugonjwa huu unasababishwa na vimelea vinavyoitwa Ralstonia solanacearum. Vimelea vinaishi kwenye mbegu na udongo ulioathirika. Mnyauko huenea kupitia viazi mviringo vilivyoathirika, vimelea vya ugonjwa vilivyobaki kwenye udongo, mafuriko au maji ya kumwagilia, zana za kilimo (jembe au kasha la kuhifadhia viazi mviringo).

Dalili za Ugonjwa

Kwenye hatua za mwanzo ugonjwa unapoanza majani na mashina hunyauka mchana hata kama kuna unyevu wa kutosha kwenye udongo. Jinsi ugonjwa unavyoendelea, na mnyauko unaendelea. Katika hatua ya juu ya ugonjwa, vimelea vya bakteria vinatoka kupitia kwenye macho ya kiazi na kuingia kwenye udongo.

Njia za kudhibiti Bacteria Mnyauko

Mbinu shirikishi (IPM)

Mbinu shirikishi zilizokuwa zikitumika ni pamoja na:

 • Kilimo mzunguko kwa kupanda mazao ambayo siyo jamii ya viazi mviringo
 • Kufanya palizi kwa wakati
 • Kung’oa maotea ya viazi mviringo kabla ya kupanda
 • Kulima kwa kina kilichopendekezwa ili kuharibu vimelea vya bakteria
 • Kutumia mbegu ambayo haina magonjwa, kuzingatia usafi na kukinga ghala na vyombo vya kutunzia mbegu kwa kuteketeza masalia ya mazao baada ya kuvuna.

Quarantine

Epuka kusafirisha viazi mviringo kutoka eneo lenye maambukizi ya Bakteria Mnyauko kwenda kwenye eneo ambalo halina maambukizi. Pia kudhibiti minyoo fundo ya aina ya (Melodogyne incognita) na mwingiliano wao na vimelea vya bacteria mnyauko (R. solanacearum).

Minyoo fundo wanasababisha majeraha kwenye mizizi ya viazi mviringo na kurahisisha kuingia kwa bacteria. Minyoo fundo idhibitiwe kwa kupiga viuatilifu kama Actara 25WG kwenye udongo wenye unyevu kuzunguka shina la viazi mviringo.

Magonjwa ya virusi

Dalili za magonjwa ya virusi zinaonekana kwenye aina zote za viazi mviringo. Magonjwa ya virusi yanasambazwa kupitia wadudu kama wadudu mafuta, thrips, chiriku na nzi weupe pia na mbegu iliyoathirika.

Mimea iliyoathirika na magonjwa ya virusi inatoa viazi mviringo vidogo-vidogo na visivyofaa kutumika kama mbegu. Zuia na kuua wadudu waenezeo virusi uwaonapo shambani kwako kwa kutumia viuadudu kama Actara 25WG, Karate 5EC, Karate 5CS, Dynamec 018EC na Match 050EC.

Njia za kudhibiti virusi

 • Matumizi ya mbegu zenye ukinzani
 • Mbegu zisizo na magonjwa
 • Kung’oa na kuteketeza mimea iliyoathirika
 • Matumizi ya viuatilifu kudhibiti wadudu wanaoeneza magonjwa ya virusi

Uvunaji wa viazi mviringo

Muda wa kuvuna

Aina nyingi za viazi mviringo zinazolimwa Tanzania zinakomaa kati ya siku 90 na 120 baada ya kupanda. Hivyo unatakiwa kukagua shamba kabla ya kuvuna ili kuhakikisha kama viazi vimekomaa.

Dalili za viazi mviringo kukomaa:

 1. Majani yanabadilika kutoka rangi ya njano na kuanza kukauka au kufa kabisa.
 2. Na kama ukichimbua basi ngozi ya kiazi huwa ni ngumu na haiwezi kuondolewa kirahisi inaposuguliwa kwa vidole
 3. Na ni rahisi kutenganisha viazi na mizizi. Ukiona hivi, basi viazi vimekomaa na vinaweza kuvunwa na kutumika.
Uvunaji wa viazi mviringo
Uvunaji wa viazi mviringo

Kiasi cha mavuno

Mavuno ya viazi mviringo kwa ekari ni kati ya tani 8 hadi 10 kwenye shamba lililotunzwa kwa kufuata taratibu tulizoeleza au kanuni zingine za kilimo bora zinazolazimiana na mazingira yako.

Hata hivyo kiasi cha mavuno kitatofautiana kulingana na aina ya mbegu utakayoitumia.

Jinsi ya kuvuna Viazi Mviringo

Maandalizi ya Kuvuna

Unapokaribia wakati wa kuvuna, fanya yafuatayo:

 • Sitisha kumwagilia kama mwezi mmoja kabla ya muda ya muda wa kuvuna.
 • Kata mashina yote ya viazi shambani sentimeta 10 kutoka usawa wa ardhi. Au pulizia sumu ya kuua magugu ili kuua mashina ya viazi mviringo. Fanya hivi wiki 2 hadi 3 kabla ya tarehe ya kuvuna.
 • Lengo la kufanya hivi ni kuzuia maambukizi ya magonjwa ya virusi na fangasi. Na kuruhusu ngozi ya viazi ikomae vizuri.
 • Andaa utaratibu na vifaa vya uvunaji. Hii ni pamoja na vibarua, majembe, mifuko/viroba na kamba za kushonea.
 • Andaa usafiri na/au mteja kama utauzia shambani.

Namna ya Kuvuna viazi mviringo

Vuna viazi mviringo kwenye shamba kavu, lisilo na ubichi.

Viazi mringo vinavunwa kwa kuchimbua “mizizi” kwenye matuta vilimopandwa. Ikiwa shamba lina ubichi, baada ya kuvuna viazi viachwe shambani kwa angalau siku moja vikauke kabla ya kuviweka kwenye viroba au mifuko kwa ajili ya kusafirisha au kuvihifadhi.

Umakini unahitajika sana wakati wa kuchimbua ili kuhakikisha “mizizi”, ambayo ndiyo viazi vyako, haiharibiwi (haichubuliwa wala kukatwa) kwa namna yoyote ile ili kulinda ubora wake.

Viazi mviringo vilivyoharibiwa (yaani vyenye vidonda) vinaoza kirahisi sana hivyo kufanya visihifadhike kwa matumizi ya siku za usoni. Lakini pia viazi vilivyochubuka au vyenye vidonda havina soko, na hivyo kubakia kama hasara kwako mkulima.

Viazi vinavyotegemewa kuhifadhiwa kwa muda mrefu; vianikwe kivulini au mahali penye ubaridi (jotoridi la nyuzi 70C hadi 150C) na pasipo na unyevu kwa muda wa wiki mbili.

Hii itasaidia viazi mviringo “kupona” kutokana na mikwaruzo au majeraha madogo madogo yaliyopatikana wakati wa kuvuna na kusafirisha. “Kupona” huku kutasaidia kuongeza uwezo wa viazi kuhifadhika kwa muda mrefu. Viazi vilivyopona vinaweza kuhifadhiwa kwa mpaka miezi miwili.

Usithubutu kuviosha viazi kwa maji mpaka pale utakapo hitaji kuvitumia kwa chakula. Kuosha viazi mviringo kunapunguza uwezo wake wa kuhifadhika.

Jipatie kitabu cha makala hii


Tags

viazi mviringo


You may also like

Kilimo Bora Cha Karanga

Kilimo Bora Cha Karanga
 • hlw, mm n mwanafunzi wa chuo kikuhulia cha tanzania
  naitaji kufaham aina ipi ya kiazi inawza ikastahili hali ya chumvi chumvi kweny ardhi, na ipi haiwezi kabisa

 • {"email":"Email address invalid","url":"Website address invalid","required":"Required field missing"}
  >