March 18, 2023

Kilimo cha Bamia: Muongozo wa mafanikio

0  comments

Bamia ni zao la mbogamboga linalotambulika kitaalamu kama Abelmoschus esculentus lenye asili ya Ethiopia na Afrika ya magharibi. Lakini kwa sasa kilimo cha bamia kimeeenea katika nchi nyingi za ukanda wa kitropiki.

Kilimo cha bamia nchini Tanzania kimekuwa ni nyenzo muhimu kwa wakulima kujipatia kipato, lakini mafanikio hayapatikani bila ujuzi na mipango sahihi. Likiwa kama zao lenye lishe nzuri na matumizi mengi, bamia ina uwezo wa kuleta manufaa makubwa kwa wakulima na walaji.

Bamia ni zao lenye mchango mkubwa katika afya ya mwanadamu na ni chanzo muhimu cha vitamini na madini ya potasiam na chokaa ambayo ni muhimu kwa afya ya mifupa, meno na husaidia ufanyaji kazi mzuri wa misuli. Wakulima walio wengi hususan wakulima wadogo, hutegemea zao hili kama chanzo cha kipato kutokana na kutumiwa na watanzania walio wengi.

Hata hivyo, ni muhimu kujua hatua zote zinazohitajika kufanya kilimo cha bamia ili kiwe na mafanikio. Kwenye mwongozo huu, tutadurusu vipengele muhimu vya kilimo cha bamia nchini Tanzania, ikijumuisha: maandalizi ya shamba, jinsi ya kupanda, mahitaji ya udongo, mahitaji ya mbolea, udhibiti wa wadudu na magonjwa, na mbinu za kuvuna.

Kupitia somo hili, natumai utajifunza maarifa mahsusi yatakayokuwezesha kufikia mavuno ya bamia yenye mafanikio na kuongeza kipato chako. Endelea …

Bamia aina ya Emerald
Bamia aina ya Emerald green

Eneo linalofaa kwa kilimo cha bamia

Bamia ni zao linalolimwa katika maeneo mengi nchini. Baadhi ya maeneo yanayolima zao la bamia kwa Tanzania ni pamoja na mikoa ya Morogoro, Dodoma, Tabora, Pwani na Mbeya.

Ni muhimu kuchagua eneo linalofaa kwa kilimo cha bamia kabla ya kuanza uzalishaji. Ni vyema eneo litakalotumika katika kilimo cha bamia liwe na urahisi wa upatikanaji maji kurahisisha umwagiliaji.

Vilevile shamba liwe lenye kufikika kwa urahisi ili kufanya wepesi katika kuhudumia shamba na usafirishaji wa mazao kwenda sokoni au kufikiwa kwa urahisi na wanunuzi wanaofuata mazao shambani.

Zao la bamia hushambuliwa sana na minyoo fundo (nematodes). Hivyo usichague eneo ambalo limetoka kutumika katika kilimo cha mazao yanayoweza kushambuliwa na minyoo fundo kama vile viazi vitamu, nyanya, bilinganya na pilipili hoho.

Kwa tahadhari unaweza kulima zao hili katika eneo ambalo limetoka kutumika kwa kilimo cha mazao ya nafaka kama vile mahindi na mtama kwa kuwa mazao haya hayashambuliwi na minyoo fundo.

Mazingira yanayostawisha bamia vizuri

Hali ya Hewa na Mwinuko

Bamia ni zao linalopendelea hali ya joto hivyo hustawi katika maeneo yenye hali joto kuanzia nyuzi joto za sentigredi 21 hadi 35. Ustawi mzuri zaidi huonekana katika maeneo yenye joto la nyuzi za sentigredi 21 mpaka 30. Hali joto zaidi ya nyuzi za sentigredi 42 huweza kusababisha kudondoka kwa maua. Bamia hustawi vizuri katika maeneo ya mwinuko tofauti hadi mita 1000 kutoka usawa wa bahari yenye mvua za wastani.

Udongo

Zao la bamia hustawi katika udongo wa aina nyingi wenye rutuba, kina, uwezo wa kuifadhi maji vizuri na usiotuamisha maji. Hata hivyo zao hili hufanya vizuri zaidi linapolimwa katika udongo wa tifutifu yenye kichanga wenye rutuba ya kutosha na tindikali kuanzia Ph 5.8 hadi 6.5. Mbegu za bamia hushindwa kuota kabisa pale joto la udongo linapokuwa chini ya nyuzi za sentigredi 16.

Maandalizi ya shamba la Bamia

Muda wa Kuandaa

Shamba la bamia liandaliwe mapema mwezi mmoja kabla ya kupanda ili kuruhusu magugu na mabaki ya mazao kuoza vizuri. Kwa kilimo cha kutegemea mvua ni vyema maandalizi yaanze mapema kabla ya kuanza kwa mvua za masika. Inashauriwa kuanza maandalizi mapema mwezi Januari. Kwa kilimo cha umwagiliaji unaweza kuanza maandalizi muda wowote kulingana na mahitaji na soko unalolilenga.

Namna ya Kuandaa shamba

Shamba huandaliwa kwa kufyeka nyasi, kung’oa visiki na kulima kabla ya kupima na kuweka matuta.

 (i) Kulima

Shamba hulimwa kwa kutumia jembe la mkono, jembe la kukokotwa na wanyama, power tillers au matrekta. Matumizi ya jembe la kukokotwa na wanyama, power tillers na matrekta hurahisisha shughuli ya kulima na kuifanya iwe na ufanisi kwani hukatua udongo vizuri na kuufanya uwe tifutifu.

Unapotumia jembe la mkono katika kulima hakikisha unakatua udongo katika kina cha kutosha sm 20 mpaka sm 30 na kulainisha mabonge. Udongo uliokatuliwa vizuri hupitisha hewa inayohitajika na mmea, hurahisisha ukuaji wa mizizi na kuifadhi maji vizuri.

(ii) Kupima shamba (field layout)

Ni muhimu kuanza kupima shamba kabla ya kuanza kuandaa matuta ili kupata matuta yaliyo katika mpangilio mzuri na mistari ya mimea shambani iliyonyooka vizuri. Kabla ya kupima matuta ni muhimu pia kujua nafasi ya kupandia utakayo tumia ili kupata ukubwa sahihi wa kila tuta.

Kwa mfano kwa nafasi ya kupandia ya sm 60 × sm 40 kwa matuta makubwa unaweza kutengeneza kila tuta katika upana wa sm 1.2 na urefu wowote.  Acha nafasi ya m 1 kuzunguka shamba na njia kila baada ya tuta upana wa sm 50. Tumia Tape measure au kamba yenye vipimo kupima shamba huku ukiweka alama za matuta na njia kwa kuchomeka mambo (pegs) katika kila kona ya tuta na kuzungushia kamba.

(iii) Kuweka matuta

Inashauliwa kupanda bamia katika matuta ili kusaidia mizizi kukua vizuri na udongo kuhifadhi maji. Wakati wa kiangazi, tengeneza matuta yaliyodidimia kidogo ili kufanya maji yaweze kukaa kwenye udongo na wakati wa masika matuta yainuliwe kidogo toka kwenye usawa wa ardhi ili kuzuia maji yasituame.

Matuta yanaweza kuwa makubwa au madogo kulingana na matakwa ya mkulima. Matuta makubwa hupandwa mistari miwili na matuta madogo hupandwa mstari mmoja. Tengeneza matuta kwa kufuata alama zilizowekwa wakati wa kupima shamba.

Jinsi ya Kupanda Bamia

Zao la bamia huweza kupandwa moja kwa moja shambani au kwa kuanzia kitaluni. Hata hivyo kama mbegu zako zinauwezo mzuri wa kuota, ni bora ukapanda mbegu moja kwa moja ili kupunguza gharama zisizo na msingi. Na ikiwa utaamua au kulazimika kuanzia kitaluni hakikisha unafuata taratibu zote za uandaaji na utunzaji wa kitalu. Na Upandikize miche pindi inapokua na majani halisi matatu hadi manne.

Maandalizi ya Mbegu za bamia

Unahitaji mbegu za bamia kiasi cha kilo moja (kg 1) mpaka moja na nusu (kg 1.5) kupanda eneo la ekari moja. Hata hivyo kiasi hiki kinaweza kuathiriwa na nafasi ya kupandia na uotaji wa mbegu.

Mbegu za bamia ni ngumu kidogo katika kuota hivyo ni vyema ziandaliwe ili kurahisisha uotaji wake. Mbegu za bamia huandaliwa kwa kuziloweka katika maji ya vuguvugu kwa muda wa masaa ishirini na nne ili kuchochea uotaji. Mbegu za bamia huchukua muda wa siku 5 hadi 10 kuota.

Aina ya mbegu za bamia

Kuna aina tofauti za mbegu za bamia zinazopatikana Tanzania kama vile Clemson Spineless, Emerald Green, White Velvet, Perkins Mammoth na Dwarf Prolific. Mbegu ambazo hutumika na wengi ni

 • Clemson spineless: mbegu hii inatabia ya kukua urefu wa mita 1 hadi 1.5 na kuzaa bamia za kijani zenye urefu karibu sm 15. Huchukua siku 55 hadi 58 kuanza kuvuna.
 • Emerald green: mbegu hii ina tabia ya kukua hadi urefu wa m 1.5 na kuzaa bamia za kijani zenye urefu wa sm 18 hadi 20. Huchukua siku 58 hadi 60 kuanza kuvuna.
 • White velvet: mbegu hii inatabia ya kukua urefu wa m 1.5 hadi 1.8 na kuzaa bamia ndefu, nyembamba, zilizochongoka na zenye urefu wa sm 15 hadi 18.
Bamia aina ya Clemson spineless
Bamia aina ya Clemson spineless

Nafasi ya Kupandia bamia

Bamia huweza kupandwa katika nafasi tofauti kuanzia sm 60 hadi 80 kati ya mstari na mstari na sm 30 hadi 50 kutoka shimo hadi shimo. Hakikisha unafuata maelekezo ya mbegu husika juu ya nafasi pendekezwa.

Hatua za Upandaji wa bamia

Unaweza kufuata hatua zifuatazo katika upanzi wa mbegu za bamia shambani:

 1. Mwagia maji mengi shambani masaa kumi na mbili kabla ya kupanda mbegu ili kulainisha udongo na kurahisisha upanzi.
 2. Chimba mashimo ya kupandia yenye kina cha sm 2 hadi 3 katika nafasi iliyopendekezwa kwa mbegu itakayotumika mistari miwili miwili kila tuta kwa kutumia kamba iliyowekwa vipimo.
 3. Weka viganja viwili vya mkono vya samadi iliyoiva katika shimo la kupandia kisha changanya na udongo kupata mchanganyiko mzuri. Kwa mbolea ya kupandia kama DAP weka kizibo kimoja cha soda katika kila shimo la kupandia kisha fukia mbolea kwa tabaka dogo la udongo kabla ya kupanda mbegu. Kiasi cha kilo hamsini za mbolea ya DAP kinatosha kutumika katika eneo la ekari moja.
 4. Panda mbegu mbili katika kila shimo, fukia kwa udongo mwepesi, shindilia na kisha mwagia maji.

Utunzaji wa bamia baada ya kupanda

Matunzo ya shamba ni muhimu sana kwa sababu huamua kiasi cha mavuno unayoweza kupata kutoka shambani. Shamba ambalo halipati matunzo mazuri hata kama mbegu bora inayozaa sana itatumika mavuno bado yatakuwa hafifu.

Matunzo ya shamba hujumuisha mambo yafuatayo …

Umwagiliaji

Kuna njia tofauti za umwagiliaji ambazo zinaweza kutumika katika umwagiliaji wa bustani ya bamia kama vile umwagiliaji wa njia ya matone (drip irrigation), wa njia ya mifereji na umwagiliaji wa kutumia can.

Maamuzi ya njia ya kumwagilia utakayoichagua nashauri yazingatie tija ya mradi husika. Usipoteze pesa uliyowekeza kwenye shamba lako kwa kulimwagilia kwa njia duni; badala yake weka miundombinu mizuri itakayokuletea tija katika uzalishaji wako.

Ratiba ya umwagiliaji izingatie mambo yafuatayo: aina ya udongo, hatua ya ukuaji wa mimea yako na msimu wa uzalishaji.

Udongo wa kichanga unapoteza maji kwa haraka sana; bamia zinahitaji maji mengi zikiwa katika hatua ya kutoa maua na matunda; na wakati wa kiangazi upotevu wa maji ardhini ni mkubwa sana. Hivyo basi ni muhimu sana kuhakikisha shamba lako linapata maji kwa wakati stahiki kwa kuzingatia sababu kama hizi.

Kupandikiza na Kupunguzia miche

Kagua uotaji wa mbegu siku 10 hadi 14 tangu kupanda. Pandikiza mashimo yote ambayo hayakuota, mapema kadri utakavyoweza.

Unaweza kung’oa miche iliyozidi kwenye shimo moja na kupandikiza kwenye mashimo ambayo hayakuota. Hatahivyo hili lifanyike anagalau wiki tatu tangu kupanda wakati mimea imefikia urefu wa sm 10 mpaka 15.

Mahitaji ya mbolea za kupandia na kukuzia

Kwa mbolea ya kupandia kama DAP: Kiasi cha kilo 50 za mbolea ya DAP kinatosha kutumika katika eneo la ekari moja. Weka kizibo kimoja cha soda katika kila shimo la kupandia kisha fukia mbolea kwa tabaka dogo la udongo kabla ya kupanda mbegu.

Kwa mbolea ya kukuzia tunayoshauri utumie NPK kiasi cha kilo 50 kwa ekari. Mbolea ya NPK hutoa virutubisho vitatu muhimu vya Naitrojeni, Fosfeti na Potash. Mbolea hii iwe na uwiano wa 1:1:2 kwani zao hili huhitaji uwiano mzuri wa potasiam na virutubisho vingine ili kupata matunda. Endapo naitrojeni itazidi, mmea utazalisha majani mengi pasipo matunda na kusababisha mavuno hafifu.

Weka mbolea ya kukuzia wiki sita tangu kupanda kwa kiwango cha kifuniko kimoja cha soda kuzunguka shina sm 5 kutoka shina lilipo na kurudia kuweka tena kila baada ya wiki mbili hadi mwisho wa kuvuna.

maua ya bamia
Maua ya bamia

Kupiga Dawa za wadudu na magonjwa

i. Dawa za ukungu

Uchaguzi wa dawa za ukungu hufuatana na magonjwa yanayoshambulia zao husika hivyo ni vema kujua magonjwa yanayoshambulia zao la bamia kabla ya kuchagua dawa za kutumia kama kinga au tiba pale magonjwa yanapojitokeza.  Unaweza kuanza kupiga dawa ya ukungu wiki moja hadi mbili tangu miche kuota na kurudia kila baada ya wiki moja hadi mbili kutegemeana na maelekezo ya dawa husika.

ii. Dawa za kuua wadudu

Nyunyizia dawa ya kuua wadudu baada ya kuona wadudu waharibifu katika shamba lako ili kuweza kuchagua dawa sahihi ya kudhibiti aina ya wadudu waliovamia bustani yako.

Kudhibiti Magugu

Palizi ifanyike kuanzia wiki ya nne tangu kupanda na kurudia kila baada wiki mbii hadi tatu. Hakikisha hakuna magugu bustanini katika kipindi cha kutoka maua na kutengenezwa kwa matunda ili kuepusha ushindani wa mazao na magugu katika kupata maji, rutuba, hewa na mwanga. Magugu pia hutoa fursa kwa vimelea vya magonjwa na wadudu kujificha na kufanya mashambulizi kwa mazao.

Unaweza kudhibiti magugu kwa kutumia matandazo (mulch), au kwa kupalilia kutumia jembe la mkono au dawa za viuagugu. Ni muhimu kuondoa magugu na kuweka shamba katika hali ya usafi kila wakati.

Kuweka Matandazo

Matandazo husaidia kudhibiti magugu, kuifadhi unyevu na kuongeza rutuba katika udongo. Kwa matokeo mazuri katika udhibiti wa magugu inashauriwa kuweka matandazo kwa kuyatandaza katika udongo katika kina cha sm 10 mpaka 15 maeneo yote ya tuta kuzunguka mashimo ya miche.

Matandazo ya asili kama mabua ya nafaka, pumba za mpunga, maganda ya karanga na maranda ya mbao yanaweza kuwekwa kabla ya kupandikiza baada ya kuchimba mashimo ya kupandia au baada ya kupandikiza. Matandazo ya plastiki huwekwa mapema kabla ya kupandikiza baada ya kuandaa matuta.

Uvunaji wa Bamia

Kiwango cha mavuno

Ekari moja ya bamia hutoa mavuno ya wastani wa tani tano mpaka nane.

Hata hivyo kiwango cha mavuno ya bamia kwa ekari moja hutegemeana na matunzo ya shamba, uwezo wa kuzaa wa mbegu iliyotumika na idadi ya mimea katika shamba. Mbegu za aina tofauti zina uwezo tofauti wa kuzaa na hivyo mavuno huwa tofauti. Vilevile mashamba tofauti yaliyopandwa mbegu ya aina moja na kupata matunzo ya viwango tofauti huwa na kiwango tofauti cha mavuno.

Muda wa Kuvuna

Bamia huchukua siku 50 hadi 60 kuanza kuvuna. Huwa tayari kuvunwa siku tano tangu kutoka kwa maua zikiwa bado changa na zenye urefu wa sm 5 hadi 10 kutegemeana na aina ya mbegu. Hivyo basi inashauriwa kuvuna bamia kila baada ya siku tatu tangu mvuno wa kwanza wakati wa asubuhi. Uvunaji wa bamia unaweza kuendelea kwa muda wa siku 30 hadi 40 tangu mvuno wa kwanza.

bamia tayari kuvunwa
Bamia tayari kwa kuvuna

Jinsi ya kuvuna bamia

 1. Andaa vifaa na vyombo vya kuvunia kama vile kisu, mkasi na ndoo au chombo chochote cha plastiki kwa kuvisafisha kwa maji safi na sabuni.
 2. Andaa sehemu utakayokuwa unaweka bamia wakati wa kuvuna iliyo kivulini karibu na shamba na utandike turubai.
 3. Wakati wa kuvuna kata kikonyo cha bamia karibu na tawi linaloshikilia tunda kisha weka tunda kwenye ndoo. Hakikisha unavuna bamia na kikonyo chake ili zisiharibike kwa urahisi.
 4. Ndoo inapojaa bamia beba ukazitandaze katika turubai lililo tandikwa karibu na bustani ili zipate hewa na zipoe kutoka katika joto la shamba (field heat) kabla ya kuzipakia.
 5. Safisha vizuri vyombo vya kuvunia kwa maji safi na sabuni kila baada ya kumaliza siku ya kuvuna ili kuzuia vimelea vya magonjwa.

Mambo ya kuzingatia wakati wa uvunaji

Usiache bamia zikomae kabla ya kuvuna kwa sababu bamia zilizokomaa huwa ngumu na zenye nyuzi nyuzi na hivyo hazina soko kwa matumizi ya nyumbani. Vilevile kuacha bamia zikomae katika mmea husababisha mmea kuacha kuzaa mapema na hivyo mavuno huwa madogo.

Tumia kisu au mkasi wakati wa kuvuna ili kuepuka kuathiri shina na kusumbua mizizi ya mmea. Vilevile usivune bamia zinazoonyesha dalili ya kuoza au kuathiriwa na wadudu. Kwa baadhi ya watu bamia huweza kusababisha muwasho wa ngozi hivyo hakikisha unavaa suruali ndefu na shati la mikono mirefu wakati wa kuvuna.

bamia zilizochumwa
Bamia zilizochumwa

Soko la Bamia na Bei zake

Bamia ni moja ya mazao ya mboga yanayozalishwa na kuliwa kwa wingi nchini Tanzania. Zao hili linapatikana katika maeneo mengi ya nchi na linauzwa katika masoko mengi yaliyopo kote nchini. Soko la bamia Tanzania linategemea mahitaji ya ndani na nje ya nchi.

Katika soko la ndani, bamia huliwa na watu wengi kutokana na ladha yake nzuri na kustawi kwa zao hilo katika maeneo mengi ya Tanzania. Wachuuzi wa mboga na matunda huuza bamia kwenye masoko ya miji mikubwa, maduka ya mboga na matunda, na kwenye vituo vya mabasi. Bei ya bamia inategemea na msimu, ugumu wa upatikanaji wake, na eneo la soko.

Mfano kwa mwezi Oktoba 2023, kiroba cha kilo 50 cha bamia kilikuwa kinauzwa kati ya TZS 10,000 na TZS 25,000 katika maeneo mbali mbali ya mkoa wa Morogoro.

Katika soko la nje, Tanzania ina fursa ya kuuza bamia nchi za nje kutokana na ubora wake na mahitaji ya kimataifa. Bamia huuza hasa katika nchi jirani kama vile Kenya, Uganda, Rwanda, na Burundi. Pia, Tanzania ina fursa ya kuuza bamia nchi za Ulaya, Asia na Mashariki ya Kati.

Hata hivyo, changamoto za soko la bamia Tanzania ni pamoja na ukosefu wa teknolojia bora ya kuhifadhi na usafirishaji wa zao hilo, uzalishaji mdogo na usimamizi duni wa ubora wa zao. Serikali inajitahidi kusaidia wakulima wa bamia kupitia sera zinazolenga kuinua uzalishaji na ubora wa zao hilo, kuboresha mifumo ya masoko, na kutoa mafunzo kwa wakulima juu ya mbinu bora za uzalishaji na usimamizi wa ubora.

Faida za bamia mwilini

Bamia ina faida nyingi kwa afya ya binadamu kutokana na virutubisho na madini ambayo inayo. Baadhi ya faida za bamia kwa mwili ni pamoja na:

 1. Kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo: Bamia ina kiwango kikubwa cha nyuzinyuzi na madini ya potassium ambayo husaidia kudhibiti shinikizo la damu na kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo.
 2. Kuimarisha mfumo wa kinga: Bamia ina kiwango kikubwa cha vitamini C na antioxidants ambazo husaidia kuimarisha mfumo wa kinga wa mwili na kupambana na magonjwa mbalimbali.
 3. Kuimarisha afya ya ngozi: Bamia ina vitamini C, A na antioxidants ambavyo husaidia kudumisha afya ya ngozi na kuzuia uharibifu unaosababishwa na mionzi ya jua na uchafu.
 4. Kupunguza hatari ya kisukari: Bamia ina nyuzinyuzi nyingi na sukari ya kawaida, ambayo inasaidia kudhibiti viwango vya sukari kwenye damu na kupunguza hatari ya kisukari.
 5. Kusaidiakupunguza uzito: Bamia ina karoli kidogo sana.
 6. Kusaidia katika umeng’enyaji wa chakula: Kwa kuwa bamia ina nyuzinyuzi nyingi.
 7. Kusaidia kuzuia upofu wa usiku: Bamia ina kiwango kikubwa cha vitamini A ambayo ni muhimu kwa afya ya macho na inaweza kusaidia kuzuia upofu wa usiku.
 8. Kupunguza hatari ya ugonjwa wa figo: Bamia ina potassium ambayo husaidia kudhibiti kiwango cha sodium kwenye damu na kupunguza hatari ya ugonjwa wa figo.
 9. Kusaidia katika afya ya ubongo: Bamia ina virutubisho vinavyosaidia afya ya ubongo kama vile folate, vitamini B6 na B12, ambavyo husaidia katika kuboresha kumbukumbu na kazi za utambuzi.

Hitimisho

Kwa kumalizia, kilimo cha bamia nchini Tanzania kina uwezekano wa kuwa mradi wenye faida kubwa, lakini kinahitaji mipango makini, maandalizi na utekelezaji.

Ukifuata mbinu zilizoainishwa kwenye mwongozo huu utajiongezea nafasi ya kufaulu na kuzalisha mazao yenye ubora wa hali ya juu yanayokidhi matakwa ya walaji.

Kumbuka kuandaa shamba lako vizuri, kuchagua wakati sahihi wa kupanda, kutumia mbolea za kupandia na kukuzia, kudhibiti wadudu na magonjwa, na kutumia mbinu sahihi za uvunaji.

Kwa kujitolea na kufanya kazi kwa bidii, unaweza kuanzisha biashara ya kilimo cha bamia na kuleta matokea chanya kwenye afya na uchumi wa jamii yako.

Hivyo basi, kunja mikono ya shati lako, vaa buti zako za shamba, uanze safari ya mafanikio ya kilimo cha bamia!

Jipatie kitabu cha makala hii


Tags

Bamia, Bustani


You may also like

{"email":"Email address invalid","url":"Website address invalid","required":"Required field missing"}
>