Natarajia ujifunze mambo unayotakiwa kufanya ili ujue thamani ya mazao yako na uweze kupanga bei ya mazao yako mwenyewe yenye kukuletea faida bila ya kushawishiwa na madalali..

Habari za kazi ndugu yangu na karibu tena katika muendelezo wa makala zetu za kilimo cha kisasa. Naomba nianze kwa kukuuliza haya maswali: Umeshawahi kuuza zao ulilolima wewe mwenyewe? Niambie, ulitumia vigezo gani kupanga bei ya mazao uliyokuwa unauza? Tafadhali jibu maswali haya kwenye comments hapo chini.

Sasa basi kama nilivyoanza kwa maswali hapo juu, leo nimeona nikufahamishe namna sahihi unayotakiwa kuitumia kujua thamani ya mazao yako na hivyo uweze kupanga bei ya mazao isiyo na hasara kwako.

Mkulima ni mfanyabiashara, na mfanyabiashara yeyote ni mtu anayelenga faida kubwa sana au hasara kidogo sana. Kwa hiyo ni muhimu kwa mkulima kujua thamani ya mazao yake ili aweze kujua ni bei gani anayotakiwa kuuzia mazao yake lakini pia ajue bei ambayo akiuza kwayo itamletea hasara.


Jinsi-ya-Kupanga-bei-ya-mazao-yako

Nimeamua kuleta somo hili kwa sababu wakulima wengi wanauza mazao yao sio kwa sababu wameiona faida, ila tu kwa sababu wamevuna au msukumo wa soko/madalali na bei iliyopo wakati husika.

Hivyo basi natarajia mpaka mwisho wa somo hili utakuwa umejifunza mambo unayotakiwa kufanya ili ujue thamani ya mazao yako na uweze kupanga bei ya mazao yako mwenyewe yenye kukuletea faida bila ya kushawishiwa na madalali.

Kabla hutujaendelea: hapa chini nimekuchagulia baadhi ya makala za kilimo bora, nimeona zisikupite:


Ok tuendelee, sasa basi unachotakiwa kufanya ni:

HATUA YA KWANZA:  Tunza kumbukumbu

Mali bila daftari hupotea bila habari”. Waliona mbali sana waliosema maneno haya. Mkulima unatakiwa uwe na daftari la kutunzia kumbukumbu za shughuri zako zote za shamba. Tunza kumbukumbu za gharama zote ulizozitumia katika kilimo chako.

Kama ulikodi shamba au ulinunua, ulilima kwa trekta, ukaajiri watu wa kupanda, ukanunua mbolea na madawa ya kuulia magugu na wadudu, kama uliajiri watu wa kupiga dawa shambani, mpaka kuvuna n.k gharama zote ulizotumia katika shughuri hizi zihifadhi kwani hii ndio dira yako.

Hakikisha kuwa unatambua ukubwa/eneo la shamba ulilolima kama ni hekta moja au mbili ama ni ekari tatu au nne. Hapa utapata jumla ya gharama ulizotumia katika uzalishaji kwa eneo husika.


HATUA YA PILI: Pima jumla ya kiasi cha mavuno yako

Kiasi cha mavuno unaweza kukipima kwa idadi ya magunia au matunda, kwa uzito (Kg) au ujazo (lita au debe). Napendekeza upime kwa magunia, au kilo au/na idadi ya matunda kwa sababu ndio vipimo tunavyotumia kuuza bidhaa zetu sokoni. Kama ni vitunguu utapima kwa kilo au magunia, yaani ujue umevuna magunia mangapi katika eneo ulilolima.

Kama ni matikiti/matango basi utapima kwa idadi ya matunda, yaani jumla ya matunda uliyovuna au jumla ya kilo. Kama ni mchele basi utaupima kwa kilo ili ufahamu umepata jumla ya kilogram ngapi. Pima mavuno yako kwa njia yoyote unayoitumia wewe ilimradi tu mwisho wa siku ujue umevuna kiasi gani. Hapa utapata jumla ya mavuno kwa eneo husika.


HATUA YA TATU: Tambua Thamani ya mazao yako

Katika hatua hii gawanya jumla ya gharama za uzalishaji kwa kiasi cha mavuno. Lengo letu hapa ni kujua umegharamia pesa kiasi gani kwa gunia moja au kilo moja au kwa tunda moja ulilovuna. Hii ndiyo thamani ya mazao yako.

Ili tuelewane vizuri hapa tuchukulie kwa mfano gharama za uzalishaji ni TSh. Milion moja na nusu (1,500,000) ulizotumia katika ekari moja:

 • Kama ulilima vitunguu na ukapata (kwa mfano) gunia 50 za kilo 100 kila moja: basi gharama ulizotumia kuzalisha gunia moja ni = 1,500,000/50 ambayo ni = TSh 30,000. Kwa hiyo ulitumia TSh 30,000 kuzalisha kila gunia moja la vitunguu (ikumbuke pointi hii) 
 • Kama ulilima matikiti na ukavuna matunda 4000: basi gharama ulizotumia kwa kila tikiti moja ni = 1,500,000/4000 = TSh. 375. Kwa hiyo thamani ya kila tikiti moja ulilozalisha ni Tsh 375 (Ikumbuke pointi hii) 
 • Na kama ulilima mpunga na ukataka kuuza mchele, tuseme umepata Kg 1000 za mchele: kwa hiyo gharama ulizotumia kuzalisha kila kilo moja ya mchele ni = 1,500,000/1000 = Tsh. 1500. Hivyo basi kila kilo moja ya mchele uliyozalisha imekugharimu Tsh. 1500 (ikumbuke pointi hii)

Sasa tupandishe kidogo gharama za uzalishaji, kutoka milioni moja na nusu mpaka milioni tatu kwa eneo lile lile la ekari moja:

 • Kwa vitunguu ambavyo umevuna gunia 50, basi gharama za kuzalisha kila gunia zitakuwa ni Tsh. 60,000 badala ya Tsh 30,000 ya kwenye mfano wa kwanza (rejea mahesabu ya hapo juu).
 • Kwa matikiti ambayo umevuna jumla ya matunda 4000 basi gharama za kila tikiti zitakuwa ni Tsh 750 badala ya Tsh 375 ya kwenye mfano wa kwanza.
 • Na kwa mpunga ambao umevuna Kg 1000 za mchele basi kila kilo moja itakuwa imekugharimu Tsh 3000 badala ya Tsh 1500 ya kwenye mfano wa kwanza hapo juu.

Kwanini tumebadilisha gharama za uzalishaji? Lengo letu hapa ni kuonesha jinsi gani gharama za uzalishaji zinavyochangia katika thamani ya mazao yako na hivyo katika kufanya maamuzi ya bei yako ya faida.

Ikiwa gharama za uzalishaji ni kubwa basi mazao yako yanathamani kubwa na hivyo basi ili upate faida ni lazima uuze kwa bei kubwa kuliko thamani yake kama tutakavyoona hapa chini.


HATUA YA NNE: Kupanga bei ya mazao yenye faida

Sasa baada ya kujua thamani ya gunia moja au kilo moja au tunda moja, hatua nyingine ambayo ndio muhimu zaidi ni kupanga bei sahihi yenye faida utakayouzia mazao yako. Hapa tunahitaji kupanga bei ya mazao kwa kipimo husika yaani bei ya gunia moja au kilo moja au tunda moja. Bei yenye faida kwako ni ile itakayorudisha gharama zote ulizotumia katika uzalishaji wako. Sasa rejea hatua ya tatu hapo juu:

 • Kama jumla ya gharama za uzalishaji ni milioni moja na nusu: gunia moja la vitunguu lilikugharimu Tsh 30,000 hivyo basi bei nzuri kwako hapa ni kuanzia Tsh 35,000 kwani itarudisha gharama zako za uzalishaji (30,000) na kukupa faida ya Tsh 5000 kwa kila gunia moja. 
 • Na kama jumla ya gharama za uzalishaji ni milioni tatu: gunia moja la vitunguu lilikugharimu Tsh 60,000 hivyo basi ili upate faida ni lazima uuze vitunguu vyako kuanzia Tsh 65,000 hapo utakuwa umejilipa gharama zako na kubaki na faida ya Tsh 5000 kwa kila gunia. 
 • Hivyo hivyo utafanya kwa mchele, matikiti na mazao mengine yote uliyolima

Baada ya kujipangia bei yako sasa toka nje uangalie soko likoje, je bei uliyojipangia ni ndogo au kubwa kuliko iliyoko sokoni?

Ikiwa bei uliyopanga kuuza mazao yako ni ndogo kuliko inayotembea sokoni kwa wakati huo unaweza kuuza au kuangalia namna nyingine ya kuongeza faida zaidi. Lakini ukiona bei ya sokoni ni ndogo kuliko ile uliyopanga kuuzia mazao yako, fanya moja kati ya yafuatayo:

 • Kwa mazao yanayohifadhika basi yahifadhi kwa muda ili kupisha hali mbaya ya soko. Hakikisha kuwa mazao yako yanahifadhika na una miundombinu ya kuhifadhia kwa angalau miezi mitatu hadi sita. Kumbuka kuwa unapoamua kuhifadhi unaongeza gharama za ulinzi na za kuhifadhi hivyo utakapotaka kuuza itabidi uzitilie maanani gharama hizi. Kwa maana nyingine ni kwamba unaongeza gharama za uzalishaji kwa hiyo utatakiwa kuongeza ile bei ya kuuzia (Fuata hatua nne tulizoelezea hapo juu). 
 • Na kwa mazao yasiyohifadhika kama mboga mboga na matunda (nyanya, matikiti) basi epuka hasara kubwa. Ninaposema epuka hasara kubwa namaanisha uza mapema kadri uwezavyo, kwani kuchelewesha kuna hasara tatu:
  1. Kuendelea kusubiri kunakuongezea wewe gharama za ulinzi na uhifadhi,
  2. Kusubiri kunaweza kusababisha kuoza kwa mazao yako kitu ambacho kitapunguza ubora na uwingi wa mazao na hatimaye kipato chenyewe na
  3. Inawezekana wakati wewe unaendelea kusubiri bei ikazidi kushuka hivyo utajisababishia hasara kubwa zaidi. Kwa hiyo kwa mazao yasiyohifadhika uza mapema ili uepuke hasara kubwa zaidi.

Ushauri: katika mradi wowote wa kilimo biashara utakao ufanya jitahidi sana kupunguza gharama za uzalishaji ili ujiongezee nafasi ya kupata faida kubwa zaidi. Punguza gharama zote zisizo za lazima, lakini usijisahau kiasi cha kuathiri ubora na wingi wa mavuno.

Kabla hatujamaliza kabisa nikukumbushe kuwa tumeshaandika baadhi ya makala za jinsi ya kufanya kilimo bora na chakisasa, zipo hapa chini (bofya kuzisoma):

Naomba nimalize kwa kukuuliza tena haya maswali: Umeshawahi kuuza zao ulilolima wewe mwenyewe? Kama ndio, hebu tuambie, ulitumia vigezo gani kupanga bei ya mazao uliyokuwa unauza? Tafadhali jibu maswali haya kwenye comments hapo chini.

0 0 vote
Article Rating

Mtalula Mohamed

I like blogging. In order utilize my profession I chose to share, to blog, a few tips and tricks about farming and agriculture to anyone interested.

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
James Mndeme
James Mndeme
2 years ago

Hii ni kweli kabisa tunakosea hapa

Brian
Brian
9 months ago

Nauliza gunia la kilo 100 la marage Lina Sado ngapi au debe ngapi nahitaji kujua

error: Content is protected !!
2
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x

Join Our Farming Community