Mkulima ni mfanyabiashara, na mfanyabiashara yeyote ni mtu anayelenga faida kubwa au hasara kidogo. Kwa hiyo ni muhimu kwa mkulima kujua thamani ya mazao yake ili…

Habari za kazi ndugu yangu na karibu tena katika muendelezo wa makala zetu za kilimo cha kisasa. Leo nimeona nikufahamishe namna sahihi unayotakiwa kuitumia kujua thamani ya mazao yako na hivyo uweze kupanga bei isiyo na hasara kwako. Mkulima ni mfanyabiashara, na mfanyabiashara yeyote ni mtu anayelenga faida kubwa au hasara kidogo. Kwa hiyo ni muhimu kwa mkulima kujua thamani ya mazao yake ili aweze kujua ni bei gani anayotakiwa kuuzia mazao yake lakini pia ajue bei ambayo akiuza kwayo atapata hasara.
Mkulima-ni-mfanyabiashara

Nimeamua kuleta somo hili kwa sababu wakulima wengi wanauza mazao yao sio kwa sababu wameiona faida ila tu kwa sababu ya msukumo wa soko/madalali na bei iliyopo wakati husika. Hivyo basi natarajia mpaka mwisho wa somo hili utakuwa umejifunza mambo unayotakiwa kufanya ili ujue thamani ya mazao yako na uweze kujipangia bei yako mwenyewe yenye kukuletea faida bila ya kushawishiwa na madalali.

Kabla hutujaendelea: hapa chini nimekuchagulia baadhi ya makala za kilimo bora ni nzuri sana, bofya ili uzisome:

Okay tuendelee, sasa basi unachotakiwa kufanya ni:
HATUA YA KWANZA
Mali bila daftari hupotea bila habari”. Waliona mbali sana waliosema maneno haya. Mkulima unatakiwa uwe na daftari la kutunzia kumbukumbu za shughuri zako zote za shamba. Tunza kumbukumbu za gharama zote ulizozitumia katika kilimo chako. Kama ulikodi shamba au ulinunua, ulilima kwa trekta, ukaajiri watu wa kupanda, ukanunua mbolea na madawa ya kuulia magugu na wadudu, kama uliajiri watu wa kupiga dawa shambani, mpaka kuvuna n.k gharama zote ulizotumia katika shughuri hizi zihifadhi kwani hii ndio dira yako. Hakikisha kuwa unatambua ukubwa/eneo la shamba ulilolima kama ni hekta moja au mbili ama ni ekari tatu au nne. Hapa utapata jumla ya gharama ulizotumia katika uzalishaji kwa eneo husika.
HATUA YA PILI
Pima jumla ya kiasi cha mavuno yako. Kiasi cha mavuno unaweza kukipima kwa idadi ya magunia au matunda, kwa uzito (Kg) au ujazo (lita au debe). Napendekeza upime kwa magunia, kilo au/na idadi ya matunda kwa sababu ndio vipimo tunavyotumia kuuza bidhaa zetu sokoni. Kama ni vitunguu utapima kwa kilo au magunia, yaani ujue umevuna magunia mangapi katika eneo ulilolima. Kama ni matikiti/matango basi utapima kwa idadi ya matunda, yaani jumla ya matunda uliyovuna. Kama ni mchele basi utaupima kwa kilo ili ufahamu umepata jumla ya kilogram ngapi. Pima mavuno yako kwa njia yoyote unayoitumia wewe ilimradi tu mwisho wa siku ujue umevuna kiasi gani. Hapa utapata jumla ya mavuno kwa eneo husika.

HATUA YA TATU
Katika hatua hii gawanya jumla ya gharama za uzalishaji kwa kiasi cha mavuno. Lengo letu hapa ni kujua umegharamia pesa kiasi gani kwa gunia moja au kilo moja au kwa tunda moja ulilovuna. Hii ndiyo thamani ya mazao yako. Ili tuelewane vizuri hapa tuchukulie kwa mfano gharama za uzalishaji ni TSh. Milion moja na nusu ulizotumia katika ekari moja:
 • Kama ulilima vitunguu na ukapata (kwa mfano) gunia 50: basi gharama ulizotumia kuzalisha gunia moja ni = 1,500,000/50 ambayo ni = TSh 30,000. Kwa hiyo ulitumia TSh 30,000 kuzalisha kila gunia moja la vitunguu (ikumbuke pointi hii) 
 • Kama ulilima matikiti na ukavuna matunda 4000: basi gharama ulizotumia kwa kila tikiti moja ni = 1,500,000/4000 = TSh. 375. Kwa hiyo thamani ya kila tikiti moja ulilozalisha ni Tsh 375 (Ikumbuke pointi hii) 
 • Na kama ulilima mpunga na ukataka kuuza mchele, tuseme umepata Kg 1000 za mchele: kwa hiyo gharama ulizotumia kuzalisha kila kilo moja ya mchele ni = 1,500,000/1000 = Tsh. 1500. Hivyo basi kila kilo moja ya mchele uliyozalisha imekugharimu Tsh. 1500 (ikumbuke pointi hii)

Sasa tupandishe kidogo gharama za uzalishaji, kutoka milioni moja na nusu mpaka milioni tatu kwa eneo lile lile la ekari moja:
 • Kwa vitunguu ambavyo umevuna gunia 50, basi gharama za kuzalisha kila gunia zitakuwa ni Tsh. 60,000 badala ya Tsh 30,000 (rejea mahesabu ya hapo juu) 
 • Kwa matikiti ambayo umevuna jumla ya matunda 4000 basi gharama za kila tikiti zitakuwa ni Tsh 750 badala ya Tsh 375 
 • Na kwa mpunga ambao umevuna Kg 1000 za mchele basi kila kilo moja itakuwa imekugharimu Tsh 3000 badala ya Tsh 1500
Unajua ni kwanini tumebadilisha gharama za uzalishaji? Lengo letu hapa ni kuonesha jinsi gani gharama za uzalishaji zinavyochangia katika thamani ya mazao yako na hivyo katika kufanya maamuzi ya bei yako ya faida. Ikiwa gharama za uzalishaji ni kubwa basi mazao yako yanathamani kubwa na hivyo basi ili upate faida ni lazima uuze kwa bei kubwa kuliko thamani yake kama tutakavyoona hapa chini.
HATUA YA NNE:
Sasa baada ya kujua thamani ya gunia moja au kilo moja au tunda moja, hatua nyingine ambayo ndio muhimu zaidi ni kupanga bei sahihi yenye faida utakayouzia mazao yako. Hapa tunahitaji kupanga bei ya mazao kwa kipimo husika yaani bei ya gunia moja au kilo moja au tunda moja. Bei yenye faida kwako ni ile itakayorudisha gharama zote ulizotumia katika uzalishaji wako. Sasa rejea hatua ya tatu hapo juu:
 • Kama jumla ya gharama za uzalishaji ni milioni moja na nusu: gunia moja la vitunguu lilikugharimu Tsh 30,000 hivyo basi bei nzuri kwako hapa ni kuanzia Tsh 35,000 kwani itarudisha gharama zako za uzalishaji (30,000) na kukupa faida ya Tsh 5000 kwa kila gunia moja. 
 • Na kama jumla ya gharama za uzalishaji ni milioni tatu: gunia moja la vitunguu lilikugharimu Tsh 60,000 hivyo basi ili upate faida ni lazima uuze vitunguu vyako kuanzia Tsh 65,000 hapo utakuwa umejilipa gharama zako na kubaki na faida ya Tsh 5000 kwa kila gunia. 
 • Hivyo hivyo utafanya kwa mchele, matikiti na mazao mengine yote uliyolima
Baada ya kujipangia bei yako sasa toka nje uangalie soko likoje, je bei uliyojipangia ni ndogo au kubwa kuliko iliyoko sokoni? Ikiwa bei uliyopanga kuuza mazao yako ni ndogo kuliko inayotembea sokoni kwa wakati huo (au bei ya sokoni ni nzuri zaidi kuliko uliyotegemea wewe) basi fanya hima uuze kwani utakuwa umevuka matarajio yako katika uzalishaji kitu ambacho kila mtu anakitamani.
Lakini ukiona bei ya sokoni ni mbaya yaani ni ndogo kuliko ile uliyotaka kuuzia mazao yako fanya moja kati ya yafuatayo:
 • Kwa mazao yanayohifadhika basi yahifadhi kwa muda ili kupisha hali mbaya ya soko. Hakikisha kuwa mazao yako yanahifadhika na una miundombinu ya kuhifadhia kwa angalau miezi mitatu hadi sita. Kumbuka kuwa unapoamua kuhifadhi unaongeza gharama za ulinzi na za kuhifadhi hivyo utakapotaka kuuza itabidi uzitilie maanani gharama hizi. Kwa maana nyingine ni kwamba unaongeza gharama za uzalishaji kwa hiyo utatakiwa kuongeza ile bei ya kuuzia (Fuata hatua nne tulizoelezea hapo juu). 
 • Na kwa mazao yasiyohifadhika kama mboga mboga na matunda (nyanya, matikiti) basi epuka hasara kubwa. Ninaposema epuka hasara kubwa namaanisha uza mapema kadri uwezavyo, kwani kuchelewesha kuna hasara tatu: (1) kuendelea kusubiri kunakuongezea wewe gharama za ulinzi na uhifadhi, (2) kusubiri kunaweza kusababisha kuoza kwa mazao yako kitu ambacho kitapunguza ubora na uwingi wa mazao na hatimaye kipato chenyewe na (3) Inawezekana wakati wewe unaendelea kusubiri bei ikazidi kushuka hivyo utajisababishia hasara kubwa zaidi. Kwa hiyo kwa mazao yasiyohifadhika uza mapema ili uepuke hasara kubwa zaidi.
Ushauri: katika kilimo chochote utakacho kifanya jitahidi sana kupunguza gharama za uzalishaji ili ujiongezee nafasi ya kupata faida kubwa zaidi. Punguza gharama zote zisizo za lazima, lakini usijisahau kiasi cha kuathiri ubora na wingi wa mavuno.

Kabla hatujamaliza kabisa nikukumbushe kuwa tumeshaandika baadhi ya makala za jinsi ya kufanya kilimo bora na chakisasa, zipo hapa chini (bofya kuzisoma):

Hivi ndivyo tunamaliza somo letu la leo, je umejifunza kitu chochote? Ulikuwa unafanyaje unapotaka kujua thamani ya mazao yako? Weka mawazo yako hapa chini kwenye comments. Tukutane tena Jumatatu ijayo katika makala nyingine tena…

Categories: Kilimo Biashara

Mtalula Mohamed

Mtaalamu wa kilimo, Blogger, na Mwandishi wa makala za Kilimo gazeti la Mwananchi. Unaweza kuwasiliana nami ukitaka kujua jinsi ya kufanya kilimo cha korosho, miwa na mazao mengine. Pia namna ya kutunza mazao yako; yaani kuhusu mbolea, madawa ya magugu, wadudu na magonjwa.

1 Comment

James Mndeme · July 10, 2017 at 20:28

Hii ni kweli kabisa tunakosea hapa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *