Utabiri wa Mvua za Vuli 2019
Dondoo muhimu za mvua za Vuli 2019
- Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli kipindi cha Oktoba – Disemba 2019, ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali kama vile kilimo na usalama wa chakula, mifugo na wanyamapori, n.k.
- Utabiri huu ni mahsusi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Nyanda za juu kaskazini mashariki, Pwani ya kaskazini, Ukanda wa Ziwa Viktoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma).
- Katika msimu wa mvua za vuli 2019, maeneo mengi ya nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na pwani ya kaskazini yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani. Aidha, mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Viktoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
Kanda ya Ziwa: Miko aya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga
Maeneo machache ya mkoa wa Kagera mvua za nje ya msimu zinaendelea toka mwezi Agosti na zinatarajiwa kusambaa katika maeneo mengine ya ziwa Viktoria hadi kufikia wiki ya pili ya mwezi Oktoba, Hivyo kuungana na msimu wa mvua za Vuli. Mvua hizo zinatarajiwa kuendelea kusambaa katika mikoa ya Mwanza, Geita, Mara, Simiyu na Shinyanga katika wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Oktoba.
Kiwango cha mvua kinachotarajiwa katika msimu huu ni mvua za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi ya ukanda huo. Msimu wa mvua za Vuli katika maeneo haya unatarajiwa kuisha kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Januari, 2020.
Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, pwani ya Visiwa vya Ungujana Pemba, pamoja na Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro
Mvua za vuli katika maeneo haya zinatarajiwa kuanza katika wiki ya pili ya mwezi Oktoba ingawa mtawanyiko wake unatarajiwa kuwa hafifu. Vipindi virefu vya ukavu na mvua chache pia vinatarajiwa katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani ya kaskazini.
Hata hivyo, mvua zinatarajiwa kunyesha katika kiwango cha wastani kuanzia wiki ya pili ya mwezi Novemba. Mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Disemba.
Usipitwe na makala hizi…
- Fahamu Kilimo Cha Matango (Cucumber)
- Jinsi ya Kuandaa na Kutunza Kitalu cha miche ya mbogamboga
- Jinsi ya kufanya Kilimo Bora cha Karoti
- Jinsi ya kufanya Kilimo cha Nanasi
- Jinsi ya kufanya Kilimo cha Vitunguu Maji kitaalam
Nyanda za juu kusini Mashariki: Mikoa ya Kilimoanjaro, Arusha na Manyara
Mvua za vuli katika maeneo ya Nyanda za juu Kaskazini Mashariki zinatarajiwa kuanza katika wiki ya nne ya mwezi Oktoba na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Mvua hizi zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Disemba 2019.
Athari za mvua za vuli na ushauri kwa kilimo na usalama wa chakula, mifugo na wanyamapori
Katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za vuli za wastani hadi chini ya wastani, upungufu wa unyevunyevu ardhini unatarajiwa kujitokeza. Upungufu wa malisho na maji kwa ajili ya mifugo pia unatarajiwa hivyo kusababisha uwezekano wa migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Wafugaji wanahamasishwa na kushauriwa kuvuna mifugo yao ikiwa bado katika hali nzuri. Wafugaji pia wanashauriwa kutunza mifugo yao kwa kuzingatia ushauri kutoka kwa maafisa ugani katika maeneo yao.
Sekta ya uvuvi, katika maeneo hayo, inaweza kuathiriwa kutokana na upungufu wa maji katika mabwawa ya samaki na hivyo wafugaji wanashauriwa kuimarisha miundombinu ya ufugaji wa samaki na kuzingatia matumizi sahihi ya maji.
Katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, shughuli za kawaida za kilimo zinatarajiwa. Aidha, malisho na maji ya kutosha kwa ajili ya mifugo na wanyamapori vinatarajiwa.
Imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania. Taarifa kamili hii hapa
Mwelekeo wa Mvua za Vuli Oktoba – Disemba 2018
Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2018, ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbali mbali wanaohitaji taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile Kilimo na Usalama wa Chakula, Mifugo na Wanyamapori, Maliasili na Utalii, Uchukuzi na Mawasiliano, Nishati na Maji, Mamlaka za Miji, Afya pamoja na Menejimenti za Maafa.
Mvua za vuli, zinazonyesha kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba, ni mahususi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Ukanda wa Ziwa Viktoria, nyanda za juu kaskazini mashariki, Ukanda wa Pwani ya kaskazini na wilaya ya Kibondo). Mvua za Vuli 2018 zinatarajiwa kuanza mapema katikati ya mwezi Septemba na mwanzoni mwa Oktoba, 2018 katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua.
Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo ya mkoa wa Kagera, Geita na wilaya ya Kibondo; mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na maeneo ya mashariki na kusini mwa Ziwa Viktoria. Mvua za juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya pwani ya kaskazini.
Disemba 2018
Kanda ya Ziwa Victoria: (Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga)
Mvua za vuli zinatarajiwa kuanza mapema, kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Septemba, 2018 katika maeneo ya mkoa wa Mara na kusambaa katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Geita na Kagera ifikapo wiki ya tatu ya mwezi Oktoba, 2018.
Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga na Simiyu. Mvua za wastani na vipindi vya mvua za chini ya wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Kagera, Geita na wilaya ya Kibondo.
Mvua za msimu wa Vuli zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Disemba, 2018 katika maeneo ya mikoa ya Mara na Simiyu, na kwa maeneo mengine ya ukanda wa Ziwa Viktoria mvua zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Januari, 2019.
Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Pwani, Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro):
Mvua zinatarajiwa kuanza mapema wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2018. Mvua za juu ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi. Vipindi vya ongezeko la mvua vinatarajiwa hususan katika ya miezi ya Oktoba na Novemba. Mvua za Vuli zinatarajiwa kuisha wiki ya tatu ya mwezi Disemba, 2018.
Nyanda za juu Kaskazini Mashariki: (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na
Manyara):
Mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya pili ya mwezi Oktoba, 2018 na
zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi. Mvua hizi zinatarajiwa kuisha wiki ya pili ya mwezi Disemba, 2018.
Athari na Ushauri: Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Wanyamapori.
Katika kipindi cha msimu wa mvua za vuli (Oktoba hadi Disemba) 2018 hali ya unyevunyevu wa udongo na upatikanaji wa chakula cha samaki vinatarajiwa kuimarika katika maeneo mengi ya ukanda wa nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na pwani ya kaskazini.
Hata hivyo, mazao yasiyohitaji maji mengi yanaweza kuathiriwa na hali ya unyevunyevu wa kupitiliza na maji kutuama. Magonjwa ya wanyama na upotevu wa samaki kutokana na uharibifu wa miundombinu ya kufugia samaki vinaweza kujitokeza kutokana na mvua za juu ya wastani zinazotarajiwa katika maeneo hayo.
Upungufu wa unyevunyevu unaweza kujitokeza katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani. Hivyo, wakulima katika maeneo hayo wanashauriwa kupanda mazao yanayotumia muda mfupi kukomaa na yanayostahimili ukame.
Malisho na upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo na wanyama pori vinatarajiwa kuwa vya kuridhisha katika maeneo mengi yanayotarajiwa kupata mvua za juu ya wastani na wastani. Hata hivyo upungufu wa maji kwa ajili ya mifugo na wanyamapori, ufugaji samaki, kupungua kwa samaki katika maji ya asili kutokana na kupungua kwa chakula cha samaki unaweza kujitokeza katika maeneo machache ya magharibi mwa Ziwa Viktoria.
Teknolojia ya uvunaji maji ya mvua iimarishwe ili kukidhi mahitaji ya maji katika kipindi cha ukavu. Pamoja na ushauri huu watumiaji wa taarifa za hali ya hewa wanashauriwa kupata ushauri zaidi kutoka kwa wataalam wa sekta husika ikiwemo maafisa ugani. Taarifa kamili inapatikana hapa
Imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.
Mwelekeo wa Mvua za Msimu Novemba 2018 – Aprili 2019
Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua (kanda ya magharibi, kati, nyanda za juu kusini magharibi, kusini mwa nchi, ukanda wa pwani ya kusini pamoja na maeneo yaliyoko kusini mwa mkoa wa Morogoro) katika kipindi cha miezi ya Novemba, 2018 hadi Aprili, 2019.
Mvua za Msimu ni mahususi katika maeneo ya magharibi mwa nchi, kanda ya kati, nyanda za juu kusini magharibi, kusini mwa nchi, ukanda wa pwani ya kusini pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro.
Maeneo haya yanapata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka, unaoanza mwezi Novemba hadi Aprili ya mwaka unaofuata.
Maelezo ya kina juu ya mwelekeo wa mvua hizo za msimu ni kama ifuatavyo…
Kanda ya Magharibi: (Mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa)
Katika kipindi cha NDJFMA 2018/19 mvua za juu ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika mkoa wa Tabora. Aidha, mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa.
Mvua hizi zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba, 2018 katika mikoa ya Kigoma na Katavi, baadae kutawanyika katika mikoa ya Rukwa na Tabora ifikapo wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Novemba, 2018 na zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2019.
Zingatio: NDJFMA = Novemba Desemba Januari Februari Machi Aprili
Kanda ya Kati: (Mikoa ya Singida na Dodoma)
Mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Novemba, 2018. Maeneo haya yanatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani hadi wastani katika kipindi cha NDJFMA 2018/19. Mvua zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Aprili, 2019.
Makala Muhimu:
- Kilimo cha Migomba (ndizi) Kisasa 2021
- Jinsi ya kufanya Kilimo cha Vitunguu Maji kitaalam
- Fahamu Kilimo Cha Matango (Cucumber)
- Jinsi ya kufanya Kilimo cha Nanasi
- Kilimo cha Matikiti Maji: Masoko na fursa za kibiashara
Nyanda za juu kusini magharibi na maeneo ya kusini mwa nchi (Mikoa ya Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Ruvuma pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro)
Mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Novemba, 2018 na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi kwa kipindi cha NDJFMA, 2018/19. Mvua zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2019 na wiki ya kwanza ya mwezi Mei, 2019.
Pwani ya kusini: (Mikoa ya Lindi na Mtwara)
Mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Novemba, 2018 na zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi katika kipindi cha miezi ya Novemba, 2018 hadi Januari, 2019.
Kipindi cha miezi ya Februari hadi Aprili, 2019 mvua zinatarajiwa kuwa za wastani katika maeneo mengi na zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2019 na wiki ya kwanza ya mwezi Mei, 2019.
Zingatio: Mwelekeo wa mvua uliotolewa hapa umezingatia zaidi kipindi cha msimu na hali ya mvua katika maeneo makubwa. Hivyo, viashiria vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mabadiliko ya muda mfupi katika maeneo madogo utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi.
Watumiaji wa taarifa za utabiri huu wanashauriwa pia kufuatilia tabiri za saa 24, siku 10 pamoja na za mwezi kama zinavyotolewa na Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania.
Makala Muhimu:
- Mbolea vunde [Mboji]: Jinsi ya kutengeneza, matumizi na faida zake
- Matumizi ya Mbolea ya Mboji na Faida Zake
- Jinsi Ya Kutengeneza Mbolea Ya Mboji Hatua Kwa Hatua
- Mahitaji ya Udongo na Mbolea katika kilimo cha Mahindi
Athari Na Ushauri kwa wadau wa Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Wanyamapori
Katika kipindi cha mvua za ‘Msimu’ (Novemba hadi Aprili) 2018/19 hali ya unyevunyevu wa udongo kwa ustawi wa mazao na upatikanaji wa chakula cha samaki vinatarajiwa kuimarika katika maeneo mengi.
Hata hivyo, mazao yasiyohitaji maji mengi, kama vile mahindi, maharage na mtama, yanaweza kuathiriwa na hali ya unyevunyevu wa kupitiliza na maji kutuama.
Aidha, magonjwa ya wanyama na uharibifu wa miundombinu ya kilimo na ile ya kufugia samaki vinaweza kujitokeza kutokana na mvua za juu ya wastani zinazotarajiwa katika maeneo hayo. Kwa upande mwingine, malisho na upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo na wanyama pori vinatarajiwa kuwa vya kuridhisha katika maeneo mengi.
Teknolojia ya uvunaji maji ya mvua iimarishwe ili kukidhi mahitaji ya maji katika kipindi cha baadae. Pamoja na ushauri huu watumiaji wa taarifa za hali ya hewa wanashauriwa kupata ushauri zaidi kutoka kwa wataalam wa sekta husika ikiwemo maafisa ugani.
Imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania. Bofya kupata taarifa kamili.
Mrejeo wa Mvua za Vuli 2018
Mvua za Vuli zinazoendelea katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka zilianza mwezi Septemba, hususani katika maeneo machache ya Ukanda wa Ziwa Victoria na yale ya pwani ya Kaskazini. Mtawanyiko wa mvua hizi bado ni hafifu katika maeneo mengi.
Kwa upande wa Nyanda za Juu Kaskazini-mashariki, mvua bado hazijaanza. Hali hii imetokana na joto la bahari kuendelea kuwa juu ya wastani katika pwani ya nchi ya Somalia na kupelekea unyevunyevu kuwa hafifu katika nchi yetu, hususani katika maeneo ya pwani ya Kaskazini na yale ya Nyanda za Juu Kaskazini-mashariki.
Mvua katika maeneo ya Ukanda wa Ziwa Victoria zinatarajiwa kuendelea vizuri katika kipindi kilichobakia cha msimu. Katika maeneo ya pwani ya Kaskazini, mtawanyiko wa mvua unatarajiwa kuanza kuimarika katika wiki ya nne ya mwezi Oktoba na kuendelea vizuri katika mwezi Novemba, 2018.
Kwa upande wa Nyanda za Juu Kaskazini-mashariki, mvua zinatarajiwa kuanza kuelekea mwishoni mwa mwezi Oktoba na kuimarika katika mwezi Novemba, 2018.
Hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa wa kuwa na mvua chache katika mwezi Disemba, 2018 katika maeneo mengi ya pwani ya Kaskazini na Nyanda za Juu Kaskazini-mashariki.
Hivyo wakulima wanaendelea kushauriwa kufuatilia utabiri wa siku kumi (10) na kupata ushauri kwa Maafisa Ugani.
Imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania. Bofya kupata taarifa kamili

Asante kwa utabiri
Shukran endelea kuwa nasi
Utabiri huu,ni mzuri sana kwani unatuwezesha kupanga mambo yetu vizuri.
Asanteni sana kwa utabiri.
Kila la heri kwenye msimu huu wa vuli ndugu Mahanda
Asante sana