Viuatilifu ni nini?
Viuatilifu ni wingi wa Kiuatilifu. Kiuatilifu ni sumu ambayo hutumika kuua, kuangamiza, kufukuza, au kuzuia visumbufu katika mimea. Visumbufu vya mimea vinaweza kuwa wadudu, kuvu (fangasi), magugu pamoja na baadhi ya wanyama na ndege.
Kiuatilifu kinaweza kunyunyizwa kwa kutumia bomba la kawaida (sprayer) au kutumia tanki maalumu lililoshikwizwa kwenye aidha trekta au aeroplane (ndege) au ndege nyuki (drone).
Ili kiuatilifu kiweze kufanya kazi kwa lengo lililokusudiwa, kuna mambo mengi ya msingi ya kuzingatia katika aidha maandalizi ya kunyunyiza au wakati wa kunyunyiza.
Unyunyiziaji wa viuatilifu ni kitendo cha kufikisha mchanganyiko wa kiuatilifu kwenye shabaha iliyokusudiwa kwa lengo la kudhibiti visumbufu.
Usiache kusoma makala hizi;
- Kilimo cha Pilipili Mwendokasi Tanzania: mbinu bora, faida kubwa
- Viuatilifu Hatarishi Vilivyopigwa Marufuku Tanzania 2026: Maamuzi ya TPHPA na Athari kwa Wakulima
- Jinsi ya kulima kabichi (cabbage) kwa mafanikio
- Kilimo cha vitunguu saumu Tanzania: Uzalishaji, Masoko na Faida
- Kilimo cha Viazi mviringo na Faida zake kwa Wakulima Tanzania
Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Wakati Wa Unyunyiziaji Viuatilifu
Ili kiuatilifu kiweze kufanya kazi kwa usahihi kuna mambo mhimu ya kuzingatia wakati wa maandalizi ya kunyuyiza au wakati wa kunyunyiza. Mambo hayo ni haya yafuatayo:-
1..Hatua ya ukuaji wa visumbufu
Ili kupata ufanisi bora shambulia visumbufu vikiwa katika hatua dhaifu ya maendeleo ya ukuaji wake kufuatana na makazi yake, tabia na mzunguko wa maisha yake.
Ukikosea unaweza kusababisha wadudu kuharibu mazao na pia wanaweza kuwa sugu juu ya kiuatilifu hicho. Pia kunyunyiza kiuagugu kipindi magugu yamekomaa hushindwa kuleta matokeo mazuri ya lengo.
2. Viwango vya sumu na ujazo kwa eneo (DOZI)
Unapotumia kiuatilifu hakikisha unasoma vizuri maelekezo ya matumizi ili uweze kutumia kipimo sahihi cha sumu katika ujazo sahihi wa maji.
Ukizidisha kipimo cha sumu husababisha athari kwa mmea, mazingira, kwa walaji na pia huongeza gharama kwani viuatilifu vingi vitahitajika kwa eneo dogo.
Aidha ukipunguza kiwango cha sumu husababisha kutotimia kwa lengo lililokusudiwa na hatimaye pia hufanya visumbufu kuwa sumu.
3. Maeneo ya shabaha lengwa
Tumia mbinu tofauti tofauti kunyunyiza kiuatilifu kulingana na maeneo ya shabaha lengwa.
Kwa mfano, kama unazuia wadudu ambao hukaa chini ya majani ya mmea hakikisha nozeli yako unaishusha chini na uigeuzie juu ili inyunyize vizuri chini ya jani.
4. Hali ya hewa
Upepo husababisha kupeperushwa kwa matone na kupelekwa yasikotakiwa. Hivyo unaponyunyiza hakikisha hali ya hewa ni tulivu isiyo na upepo mkali. Aidha kuna baadhi ya sumu hupungua nguvu zake baada ya zikinyeshewa mvua muda mfupi baada ya kunyunyizwa.
Nyunyiza kipindi ambacho hakuna dalili ya mvua kunyesha muda mfupi ujao. Pia kuna baadhi ya sumu hasa za magugu hazitakiwa kunyunyizwa wakati majani/magugu yana umande.
5. Aina ya bomba lifaalo
Uchaguzi wa bomba la kunyunyizia ni muhimu sana kwani kuna baadhi ya mimea hurefuka na kukufanya ushindwe kutumia bomba la mgongoni.
Kwa mfano; miembe, mikorosho, michungwa, miparachichi. Hivyo tumia bomba lifaalo kulingana na aina ya mazao.
6. Namna ya kutembea wakati wa kunyunyiza (kwa bomba la mgongoni)
Mnyunyizaji anatakiwa awe makini namna ya kutembea wakati ananyunyiza, asipokuwa makini kuna uwezekano wa kuruka baadhi ya sehemu.
Kutembea harakaharaka sana bila umakini husababisha dawa kutofikia kwa usahihi maeneo lengwa, aidha kutembea polepole sana hupelekea sumu nyingi kutumika katika eneo dogo, pia mnyunyizaji anatakiwa awe makini kukariri matone yanapoishia ili yaweze kukutana na matone mengine (overlap).
Soma hapa;
7. Kutumia viuatilifu sahihi na vilivyothibitishwa /sajiliwa na mamlaka husika
Unapotumia kiuatilifu hakikisha unatumia kiuatilifu kilichosajiliwa ili kuepuka kutumia vilivyo feki. Mamlaka inayohusika na usajili wa viuatifu hapa Tanzania ni Tropical pesticides research institute (TPRI), sasa ni Mamlaka ya Afya ya Mimea na Usimamizi wa Viuatilifu (TPHPA). TPHPA wamepiga marufuku mamia ya viuatilifu kuanzia Januari 2026, soma hapa kujua sababu na viuatilifu hatarishi vilivyopigwa marufuku.
Katika kifungashio cha kiuatililifu kagua alama zifuatazo kama zimewekwa kwa usahihi.
- Aina ya kiuatilifu
- Maelekezo ya matumizi ya kiuatilifu
- Maisha rufani (tarehe ya kutengenezwa/kuisha matumizi)
- Mtengenezaji
- Msambazaji
- Namba ya utambulisho
- Namba ya usajili na nembo ya TPRI
- Tahadhari
- Lugha – Kiswahili/kiingeleza
8. Aina ya kinyunyizo (nozeli) unayotumia
Vinyunyizo (nozzles) ni semu ya upande mmoja wa bomba iliyominywa ambapo kimiminika kinatoka kama mtrizi (a jet). Kwa lugha rahisi vinyunyizo hujulikana kama NOZELI ambayo ndipo mchanganyiko wa kiuatilifu hutokea na kufika katika mmea.
Ukubwa wa matone kutoka katika nozeli hutegemea aina ya kisumbufu lengwa kilicholengwa. Hivyo ili kumrahisishia mkulima kutambua ni matone ya aina gani yanatakiwa, ni vyema akafahamu rangi za nozeli na matumizi yake.
Nozeli zinatofautishwa kwa rangi tofauti kufuatana na ukubwa wa matone na kazi iliyokusudiwa. Rangi zinazotumika katika nozeli ni:- BLUU, NYEKUNDU, NJANO, KIJANI, NYEUPE NA MACHUNGWA
Jedwali lifuatalo linaonyesha mgawanyo wa nozeli kulingana na ukubwa wa matone na matumizi na rangi zake.
| Aina ya Matone | Rangi | Matumizi |
|---|---|---|
| Makubwa | Kijani | Kiuagugu kwa kunyunyiza katika udongo |
| Makubwa kiasi | Bluu | Kiua gugu na kabla ya magugu kuota |
| makubwa sana | Nyeupe | Kiuagugu kwa kunyunyiza katika udongo |
| Membamba | Mchungwa | Kuzuia wadudu na kuvu |
| Membamba sana | Nyekundu | Kuzuia wadudu na kuvu |
| Mnyunyizo wa kati | Njano | Kiuagugu na kabla ya magugu kuota |
Hitimisho
Viuatilifu ni sumu hivyo tahadhari inatakiwa wakati wa kutumia kwani husababisha madhara makubwa sana kwa mimea, binadamu na mazingira. Baadhi ya tahadhari muhimu kuchukua ni:-
- Vaa mavazi kinga unaponyunyiza kiuatilifu
- Usitumie kifungashio tupu cha kiuatilifu (empty container) kwa matumizi mengine
- Usitupe ovyo kifungashio tupu cha kiuatilifu (empty chemical containers)
- Usihifadhi kiuatilifu karibu na vyakula
- Usile wala kunywa chochote baada ya kutumia kiuatilifu bila kunawa na kuosha mikon vizuri

Asante kwa elimu nzuri lakini naomba unisaidie kutambua hizo aina mbalimbali za nozeli pamoja na matumizi yake kutokana na rangi zake
Nahitaji sana kujua mgawanyo halisi wa nozeli kutokana na matone yake
Ahsante kwa ushauri mzuri wa matumizi ya dawa naomba unisaidie list ya viwatilifu na matumizi yake
Rejea tovuti ya TPHPA, utapata orodha kamili
Naomba kufahamu mbinu zinazoweza kunisaidia au kunikinga wakati nachanganya viuatilifu
Muhimu zaidi ni kuvaa mavazi kinga kama vile boots, ovaroli, mask ya pua na mdomo, na miwani.
Asante nimeipenda sana
Naomba kujua ratiba sahihi ya kupulizia viwatilifu kwenye zao la kabichi.
Asante kwa Elimu nzuri ambayo kiukweli imenifaa maana nilikuwa sifahamu vitu vingi.Aidha nashukuru kwa maelezo mazuri ambayo ni muhimu sana, ningeomba pia kupata notes za viuatilifu na madaraja yake na jinsi ya kutumika