Utangulizi muhimu
Nyanya ni zao la mboga linalolimwa sehemu nyingi duniani kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na pia kama zao la biashara. Nyanya ni aina ya mboga inayo zalishwa kwa wingi sana duniani. Kwa Tanzania, nyanya ni zao la kwanza katika mazao ya mboga linalolimwa na kuliwa kwa wingi ukilinganisha na mboga zingine. Nyanya hutumika karibu katika kila mlo.
Kulingana na umuhimu wa zao la nyanya kama chakula na pia kama zao linalomwingizia mkulima kipato, kuna haja ya kutoa mafunzo kuhusu mbinu bora za uzalishaji wa nyanya.
Maeneo yanayolima nyanya
Inadhaniwa kuwa asili ya nyanya ni nchi ya Peru au Equador huko Amerika ya Kusini. Mmea huu ulianza kuzalishwa kama zao katika nchi ya Mexico na baadaye kusambaa katika nchi nyingine za ulimwengu.
Nchi zinazolima nyanya kwa wingi duniani ni pamoja na USA, Italia na Mexico. Kwa upande wa Africa ni; Malawi, Zambia na Botswana. Zao hili hulimwa pia katika nchi za Africa Mashariki, ikiwemo Kenya, uganda na Tanzania.
Kwa upande wa Tanzania mikoa inayolima nyanya kwa wingi hasa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na biashara ni pamoja na Mkoa wa Kilimanjaro (Hai, Moshi na Rombo), Arusha (Arumeru), Morogoro (Mgeta), Iringa (Ilula), Tanga (Lushoto), Mbeya (Mbeya vijijini) na Singida.

Mazingira yanayofaa kwa kilimo cha nyanya
Hali ya Hewa:
Nyanya hustawi vizuri zaidi kwenye mazingira ya joto la wastani kuanzia nyuzi joto 18-27 sentigreti. Mvua nyingi husababisha mlipuko wa magonjwa ya ukungu kama vile Baka jani chelewa).
Udongo:
Nyanya hustawi kwenye aina zote za udongo kuanzia udongo wa kichanga, mweupe wa tifutifu hadi udongo wa mfinyanzi, ili mradi uwe na mboji ya kutosha na usiosimamisha/tuamisha maji. Pia uwe na uchachu wa wastani yaani pH 6.0 – 7.0.
Mwinuko:
Nyanya hustawi vizuri kutoka sehemu za mwambao hadi kwenye mwinuko wa mita 400-1500 kutoka usawa wa bahari; yaani nyanda za chini, kati hadi za juu kutoka usawa wa bahari. Nyanya zinazopandwa nyanda za juu sana hukumbwa na mvua za mara kwa mara ambazo huambatana na magonjwa ya jamii ya ukungu; kama Bakajani chelewa (Late Blight).
Mbegu bora za nyanya
Kutokana na tabia ya ukuaji, mbegu za nyanya zinagawanyika katika makundi mawili:
- Nyanya ndefu (indeterminate) kwa mfano ANNA F1, Tengeru 97, Marglobe (M2009). Aina hizi za nyanya hufanya vizuri zaidi zinapopandwa ndani ya greenhouse. Uvunaji wake ni wa muda mrefu; zipo ambazo zinavunwa hata zaidi ya miezi 6, yaani hiyo miezi 6 ni ya uvunaji.
- Nyanya fupi (determinate) kwa mfano Tanya, Cal J, Mwanga, Onyx, Roma VF (nyanya mshumaa)
Kulingana na uchavushaji, nyanya zinagawanyika katika makundi mawili:
- Nyanya za OPV (Open Pollinated Variety) – Hizi ni aina za kawaida
- Nyanya Chotara – hybrid: Hizi ni nyanya zilizoboreshwa, aina hii zina mavuno mengi, kati ya hizo zipo aina fupi na ndefu.
Hata hivyo katika karne hii ya 21, nyanya zinazopendelewa kulimwa zaidi na wakulima, ni zile zinazoweza kuvumilia magonjwa, zinazo zaa sana, na zenye ganda gumu ili kufanikisha usafirishaji, na kuhifadhika kwa siku nyingi bila kuharibika mapema. Nyanya zinazoonyesha kuwa na sifa ya kuhifadhika bila kuharibika mapema ni kama:
a) Tengeru’97 ambayo ina sifa vifuatazo:
- Huzaa sana kutokana na wingi wa matunda na muda mrefu wa kuvuna, ambao hufikia michumo mikubwa kati ya 6-7 kuanzia kuvuna hadi mwisho wa mavuno.
- Aina hii ina sifa ya kuwa na ganda gumu, hivyo haziharibiki haraka wakati wa kusafirisha au kuhifadhi (wastani wa siku 20)
- Zina sifa ya kuvumilia baadhi ya magonjwa kama vile ugonjwa wa kunyauka.
- Tengeru’97 hustahimili mashambulizi ya minyoo fundo (Root knot nematodes)
b) Tanya
- Sifa kubwa ya Tanya ni kwamba nayo huzaa sana
- Huwa
na ganda/ngozi ngumu ambayo inazuia kuoza au kuharibika kwa urahisi
wakati wa kusafirisha au wakati wa kuhifadhi kwa muda mrefu. - Tanya nayo ina ladha nzuri inayopendelewa na walaji wengi
Zingatia: Tatizo la Tanya na T97 ni kwamba si kubwa sana kama marglobe 2009. Lakini ukubwa ni karibu unge karibiana, haujapishana sana. Kwa ujumla, ukubwa na wingi wa mazao hutegemea sana matunzo, udongo, hali ya hewa na mazingira kwa ujumla.
Maandalizi ya shamba la nyanya
Shamba la nyanya liandaliwe mwezi mmoja au miwili kabla ya kupanda miche. Mara baada ya kulima choma nyasi juu ya udongo au ondoa magugu yote yanayoweza kuhifadhi wadudu na magonjwa ya nyanya.
Siku moja au mbili kabla ya kuhamishia miche ya nyanya shambani, mwagilia sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya kuhamishia miche ya nyanya. Andaa mashimo ya nyanya kutegemeana na idadi ya miche uliyonayo, nafasi na aina ya nyanya. Nafasi ya kupandia nyanya ni wastani wa sentimita 50 – 60 kwa 50 – 75 kutegemeana na aina au zao litakalo changanywa na nyanya.
Sasa unaweza kujipatia Kitabu (PDF) cha Mwongozo wa kilimo cha Nyanya sasa hivi kwa bei nafuu sana. Kitabu hiki kimeboreshwa zaidi kwa ushauri wa kitaalam, mapendekezo ya kiasi, na aina za mbegu bora, mbolea na viuatilifu vya kutumia pamoja na mchanganuo wa bajeti ya kilimo na faida. Bofya hapa kukipata ndani ya Whatsapp au bofya hapa kukipata kwa email.
Jinsi ya kupanda nyanya
- Weka samadi viganja viwili au gram 5 za mbolea ya kupandia kwenye shimo kabla ya kupanda mche.
- Hamisha miche toka kitaluni pamoja na udongo wake
- Sambaza mizizi vizuri kwenye shimo bila kukunja.
- Fukia miche kina kile kile ambacho shina lilikuwa limefukiwa kitaluni.
- Mwagilia
maji ya kutosha kulingana na unyevunyevu uliopo kwenye udongo kisha
weka matandazo na kivuli ili kupunguza uharibifu unaosababishwa na
mionzi ya jua.
Jinsi ya kutunza nyanya shambani
Umwagiliaji wa nyanya
Nyanya, kama ilivyo kwa mazao mengine, zinahitaji maji mengi ili kuzaa matunda yenye afya. Kutegemeana na aina ya udongo, unaweza kumwagilia nyanya mara mbili kwa wiki.
Hakikisha unapanga ratiba maalum ya kumwagilia na unaifuata ili kuepuka kumwagilia kiholela holela kwani umwagiliaji usio na mpangilio huathiri afya ya matunda ya nyanya na kupelekea nyanya kuoza kitako (tomato blossom end rot).
Unapotumia vifaa kama water can au mpira jitahidi sana usimwagilie kwenye majani ya mmea au matunda kwa sababu kulowesha mmea kunavutia wadudu na magonjwa ya ukungu unaoharibu nyanya.
Zingatia: usituamishe maji kwenye bustani au shamba la nyanya.
Palizi: Kudhibiti magugu
Hakikisha shamba ni safi wakati wote, palilia shamba na hakikisha magugu yote hasa yale ya jamii ya nyanya yamelimiwa chini. Palilia shamba lako wiki ya pili au ya tatu baada ya kupandikiza miche, lakini unaweza kupalilia kila unapoona magugu kwani shamba linatakiwa kuwa safi muda wote. Unaweza kuondoa magugu kwa kutumia dawa za kuua magugu au jembe la mkono.
Magugu ni hatari kwa sababu tatu:
Kwanza: magugu yanashindana na mimea katika kuchukua nafasi na hivyo mimea kushindwa kujitanua.
Pili: magugu huzuia mimea ya nyanya kupata mwanga wa jua wakutosha hivyo kuifanya mimea kushindwa kujitengenezea chakula cha kutosha.
Na tatu: magugu hushindana na mimea ya nyanya kufyonza virutubisho/chakula ardhini kitu ambacho kinapelekea mimea kuwa dhaifu. Pia magugu yanahifadhi wadudu na magonjwa na hivyo kuhatarisha zaidi usalama wa nyanya.
Mahitaji ya mbolea kwenye nyanya
Mbolea za kupandia nyanya
Tumia mbolea ya DAP au Minjingu wakati wa kupandikiza miche shambani. Kiasi cha gram 5 ambayo ni sawa sawa na kifuniko kimoja cha soda inatosha kwa kila shimo lenye mche mmoja. Tanguliza mbolea kwanza kwenye shimo kisha funika na udongo kiasi ili mbolea isigusane moja kwa moja na mizizi ya nyanya.
Mbolea za kukuzia nyanya
Tumia mbolea kama vile CAN, NPK, au SA kukuzia mimea ya nyanya. Mbolea ya kukuzia iwekwe kipindi cha wiki mbili au tatu baada ya kupandikiza nyanya shambani. Tumia kifuniko kimoja cha soda kwa shina. Mbolea hii iwekwe kuzunguka shina la nyanya kwa umbali wa sentimeta 5 kutoka kwenye shina. Mbolea hii inaweza kuwekwa mara mbili kabla ya mvuno wa kwanza.
Ili kurefusha kupindi cha uzaaji wa zao la nyanya (na hata mazao mengine yatoayo matunda kama vile nyanya chungu, biringanya, na pilipili hoho) inapaswa kuongezea mbolea katika kipindi cha uvunaji mfano baada ya kuvuna mara mbili unashauriwa kuongeza mbolea ya samadi na mbolea kama vile NPK.
Hii inasaidia mmea kuendelea kutoa maua bila kuchoka. Kwa kawaida nyanya fupi jamii ya “Roma” huweza kuzaa na kuvunwa kwa kipindi cha wiki 6 hadi 8 tu. Lakini kama utakuwa unaongezea mbolea na kukazania matunzo ya shambani (hasa usafi wa shamba na kumwagilia maji ya kutosha), nyanya zinaweza kuendelea kuzaa kwa muda mrefu zaidi.
Hii ni tofauti na mazoea ya wakulima wengi kuwa mara nyanya zianzapo kuzaa huduma za palizi na usafi wa shamba huachwa na kutilia maanani kazi ya kuvuna pekee. Hii inajitokeza zaidi kwenye aina ya nyanya fupi.
Kuweka matandazo
Matandazo ni nini? Matandazo ni nylon, majani au takataka za mimea zinazowekwa shambani au bustanini kwa lengo la kutunza unyevu na kuzuia au kupunguza kasi ya uotaji wa magugu, pia yakioza huongeza rutuba kwenye udongo.
Mfano wa matandazo yanayoweza kutumika katika shamba la nyanya ni: nylon/turubai (plastic mulch), majani makavu, majani ya migomba, pumba za mazao, takataka za mbao.
Plastic mulch inawekwa kabla ya kupandikiza miche shambani lakini matandazo mengine yawekwe baada ya kupandikiza miche. Na inafaa yawekwe kuzunguka eneo la shimo la mmea au katika shamba zima. Hivyo ni vizuri matandazo ya aina hii yawekwe mara tu baada ya kupandikiza (kama shamba halina magugu) au baada ya palizi ya kwanza.
Kupogolea matawi
Punguza matawi na vikonyo ili kuongeza mwanga wa kutosha kwenye nyanya pamoja na kuruhusu mzunguko wa kutosha wa upepo na kusababisha mazingira magumu ya wadudu maadui kwenye nyanya, hasa wale wanaopenda kiza na magonjwa yanayopendelea unyevunyevu.
Kwa nyanya fupi ni vizuri kuhakikisha kuna matawi mengi iwezekanavyo ili kuweza kupata matunda mengi zaidi. Hivyo usipunguze matawi katika aina hii ya nyanya. Kwa nyanya ndefu zenye kuhitaji uegemezi, unashauriwa kukuza nyanya kwa tawi moja lisilo na vichipukizi pembeni au matawi mawili na kuacha mnyanya urefuke.
Kupogolea majani
Kupunguza majani ni muhimu pia katika kupunguza maambukizo ya ukungu katika shina na pia kutoa nafasi ili mwanga kupenya na kuruhusu mzunguko wa hewa. Kwa nyanya ndefu, majani ya chini ya matunda huondolewa kadiri unavyo endelea kuvuna.
Majani yapunguzwe kipindi cha asubuhi kwa kutumia mkono na siyo kisu kwani kinaweza kueneza magonjwa kutoka mche hadi mche. Ondoa majani yote ambayo yana dalili za magonjwa, yaliyozeeka, yaliyobadilika rangi na kuwa njano au kuanza kukauka. Wakati wa utoaji majani kuwa makini kutojeruhi shina kwani maambukizi yanaweza kuanzia hapo.
Kumbuka: Matawi na majani ya chini ya mmea wowote huwa hayana msaada sana katika uzaaji wa matunda na zaidi ni kwamba kwa kiasi kikubwa yamepoteza uwezo wake wa kutengeneza chakula. Hivyo kuendelea kubaki kwake kutapunguza chakula ambacho kingeenda kuongeza wingi na ukubwa wa matunda.
Kusimikia miti (staking)
Nyanya ziwekewe miti/mambo ili kuzuia zisianguke au kutambaa kwenye udongo, jambo ambalo linaweza kusababisha madhara mengi kwa nyanya. Nyanya zinazotambaa zinahitaji kusaidiwa kuonyeshwa njia ili zisiguse chini.
Nyanya zinapotambaa ardhini au kugusa chini zinaweza kuambukizwa wadudu na magonjwa ya ardhini kwa urahisi sana na pia wakati wa jua kali nyanya huchomwa na joto kali la ardhini.
Hivyo basi shindilia mti mmoja (pigilia chini mambo) kando ya kila mmea wa nyanya na tumia kamba kufunga shina la mmea kwenye mti huo. Simika miti wiki mbili baada ya kupandikiza miche. Miti iwe imara na isiyooza haraka. Iwe na urefu wa mita moja hadi mbili na unene usiopungua sm 2.
Changamoto za kilimo cha nyanya
Kilimo cha nyanya, kama ilivyo kwa mazao mengine ya bustani, kinakabiliwa na changamoto mbalimbali kulingana na uwezo wa mbegu kustahimili wadudu, magonjwa na hali za hewa. Kwa ujumla nyanya zinakumbwa na changamoto za wadudu na magonjwa na kutokana na ukubwa wa matatizo haya, nimekuandalia makala zifuatazo ili usisome kwa upana wake.
- Magonjwa ya nyanya na jinsi ya kuyatibu
- Wadudu waharibifu wa zao la nyanya na namna za kuwadhibiti
- Ugonjwa wa nyanya kuoza kitako
Mavuno ya nyanya kwa ekari
Mavuno ya nyanya yanatofautiona kulingana na aina ya mbegu iliyotumika, na matunzo ya yake. Lakini kwa ujumla mbegu chotara (hybrid) zinatoa mavuno makubwa zaidi ukilinganisha na mbegu za kawaida (OPV).
Nyanya aina ya Assila F1 inatoa mpaka tani 25 kwa ekari, Eden F1 inatoa mpaka tani 45 kwa ekari na Anna F1 inatoa mavuno yanayofikia tani 74 (greenhouse) kwa ekari moja. (Ref)
Uvunaji wa nyanya
Nyanya zinachukua siku 70 mpaka 90 kuwa tayari kuvuna tangu kupandikizwa. Nyanya zinatakiwa kuvunwa zinapokuwa zimekomaa lakini bado zikiwa na rangi ya kijani. Wakati wa kuvuna nyanya, tenganisha tunda na kikonyo chake na sio kikonyo na shina ili kuepuka kuujeruhi mmea kitu ambacho kinaweza hurahisisha maambikizi ya magonjwa kwa mimea.
Wakati mzuri wa kuvuna ni asubuhi na jioni. Inatakiwa nyanya ziwekwe kwenye vyombo vinavyopitisha hewa, na vyombo maarufu ni matenga. Matenga ya nyanya yanaweza kuwa yametengenezwa kwa mbao au mianzi. Mara tu baada ya kuvuna/kuchuma nyanya inashauriwa zikusanywe chini ya kivuli kwa muda ili ziweze kutoa joto la shambani kabla ya kuzifungasha kwenye matenga.
Sasa unaweza kujipatia Kitabu (PDF) cha Mwongozo wa kilimo cha Nyanya sasa hivi kwa bei nafuu sana. Kitabu hiki kimeboreshwa zaidi kwa ushauri wa kitaalam, mapendekezo ya kiasi, na aina za mbegu bora, mbolea na viuatilifu vya kutumia pamoja na mchanganuo wa bajeti ya kilimo na faida. Bofya hapa kukipata ndani ya Whatsapp au bofya hapa kukipata kwa email.

Nyanya zangu zina kauka shina lote wakati tayar zmekomaa je nifanyaje
Jaman naomba msaada nyanya zangu matunda hayawi makubwa nitumie bolea gani?
Tumia mbolea aina ya CAN ,itakusaidia kunenepesha matunda,na vilevile kutengeneza ngozi ngumu ya tunda.Vilevile madini ya calcium yatasaidia kuondoa athari ya kuungua kitako
Elimu nzuriii Sanaa, ila mngetupatia na elimu ya kustawisha Nyanya kipindi Cha masika
Ipo vizur hii somo
Kaka nyanya zangu napatia wap soko nimeivisha tiali
Habari Nina nyanya zangu lakini zimeshambuliwa sana na myauko mpakaa navurugwa
Nina nyanya zangu lakini zimeanza kutoa matunda na nyingi Zina Naya Ila Sasa nimepata changamoto ya mnyauko kiukweli unanitesa sana naomba nsaada plz
Ninapenda kilimo cha nyanya. Ila tatzo sina ujuzi
Jifunze nasi kwa makala zetu na uliza endapo hutaelewa. Karibu sana
Nikilima nyanya kwenye udongo wa kichanga na tifitifu wapi ntapata mavuno zaidi?
Kote ikiwa utahudumia kulingana na mahitaji ya kila aina ya udongo.
Napenda kilimo Cha nyanya ila sijajua mtaj wake
Kaka Miche Mia mbili hamsini ntavuna tenga ngapi kaka
Napenda kilimo Cha nyanya ila sijajua mtaj wake
Ahsante sana kwa kutupa elimu wadau wa kilimo
Swali langu:
Nifanye nini kabla sijasia mbegu kwenye kitalu?
Andaa kitalu na uweke mbolea na uichanganye vizuri na udongo.
Samahani je nyanya zaweza ku stawi vizuri Dar es salaam
Nyanya zinahitaji hali ya hewa ya ubaridi, hata hivyo zinaweza kustawi katika mazingira mbalimbali ya joto, hata Dar es salaam!
Aina ya sawa zinazo takiwa kwenye nyanya
So nice document
Thank you
Nataka kulima nyanya je in mbegu IPO bora kwa sasa maana kuna aina nyingi sana kwa sasa
ni aina gani ya nyanya inafaa kwa wakati wa mvua???
Nimesoma kote lakini sikuona namna ya kuaandaa kitalu na sijui kinatakiwa kipandikizwe baada ya muda gani….??
Kilimo cha nyanya
Nyanya zangu zimeanza kuiva ila zimekutana na unyaufu na zinaniathiri kwa kasi sana naomba ushauri wenu
naitwa ANDREW KICHERE BENZO kutoka musoma
Changamoto kubwa tulionayo huku kwetu ni soko yani mkulima unatumia gharama kubwa mpaka kuivisha mzigo unakubari ila ukifika sokoni unatamani ata kulia
Huku kwetu tunavunia kwenye matenga yanayochukua PC 12 za plastic Lita 20 bei ya kawaida ni 45000 unajikuta unavuka shamba la ekari 2 unatoa Tenga 15 ila kwa hivyo vimbao nilivyoviona apo juuu ni vizuri zaidi wateja wanaovitumia tutembereeni ña sisi huku mtusaidie jamani.
Ahsante kwa elimu nzuri
Naomba kujua kama mna makurdi ya WhatsApp mniunge 0753111558
Nashukuru kujiunga na kikundii hiki. Nia yangu na tamanio langu Ni kujifunza zaidi juu ya uzalishajii wa nyanya pamoja na marketing zake.
Naomba kupewa elimu juu ya upandaji wa nyanya
Naitaji nilime nyanya nimesoma vizur nimeelewa kanuni
Lima tuu ni zao zuri na faida nzur
Nashukuru kwa kujiunga katika kikundi hiki naitaji kujifunza zaidi juu ya uzalishaji wa nyanya
Watu tunaolima nyanya Kwa sisi tunaoanza tungekuwa
Na group la what’s up lingesaidia sana. Mimi ndo nimeanza kulima nyanya mwaka huu ndo zinaanza kutoa maua na matunda nahitaj dawa ya kuchangamsha maua
Nimejifunza kitu
Endelea kuwa nasi ujifunze mengi zaidi
Namna ya upandaji wa nyanya mstari kea mstari ni sm ngapi
Nafasi ya kupandia nyanya ni wastani wa sentimita 50 – 60 kwa 50 – 100
Mdagan nilafiki Kwa kilimo chanya kati ya kifuku na masika na kwenye kuotesha nyanya kwenye kitalu ili kuzipanda na ni nyanya ipi yenyekuvumilia kwenye magonjwa
NATAKA KUJIFUNZA KILIMO BORA CHA NYANYA
Hongera kwa elimu bora
Hongereni sana,elimu ni nzuri,,,,
Natamani kujifunza kilimo bora na chenye faida
Nimepata elimu, nashauri muendelee kutupa elimu iliyo madhubuti kama hii
Nyanya zangu zina wik mbili toka niweke kwenye kitalu je nifanye nini ili niweze kuja kupata mavuno mazuli