Mnamo tarehe 07 Januari 2026, Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), chini ya Wizara ya Kilimo, ilitoa taarifa rasmi ya kuondoa sokoni idadi kubwa ya viuatilifu hatarishi vilivyokuwa vinatumika nchini.
Uamuzi huu umetokana na tathmini ya kisayansi na kisheria iliyobaini kuwa baadhi ya bidhaa hizo ni hatari kwa afya ya binadamu, wanyama, na mazingira, au zimekuwepo sokoni kwa muda mrefu bila kufanyiwa mapitio ya usalama yanayotakiwa kisheria.
Kwa wakulima, hili si tangazo la kawaida. Ni mabadiliko ya msingi kwenye uendeshaji wa kila siku wa shughuli za kilimo. Hatua hii ni ishara ya wazi kuwa Tanzania inahamia kwenye kilimo kinachozingatia afya, mazingira na soko la dunia.
Kwenye makala hii tutajadili kwa kina maamuzi yaliyofanywa na TPHPA na athari zake kwa wakulima, wauzaji wa pembejeo na jamii ya kimataifa.
Viuatilifu vilivyopigwa marufuku na kuondolewa sokoni ni vipi?
Uamuzi wa TPHPA umejikita kwenye makundi makuu matatu ya bidhaa/viuatilifu:
1. Viuatilifu 130 Hatarishi zaidi (Highly Hazardous Pesticides)
Hivi ni viuatilifu ambavyo, kwa mujibu wa vigezo nane (8) vya FAO/WHO, vina madhara makubwa sana kwa binadamu, wanyama na mazingira kama ifuatavyo;
- Kusababisha saratani kwa binadamu
- Kuharibu mfumo wa uzazi kwa binadamu
- Kusababisha mabadiliko ya vinasaba (genetic mutation)
- Kudumu kwenye udongo na maji kwa muda mrefu
Baadhi ya viambata hivi vilikuwa vinatumika kwenye mazao ya chakula cha kila siku, jambo linaloongeza hatari kwa mlaji wa mwisho bila hata yeye kujua.
Baadhi ya viuatilifu vilivyoondolewa vinaangukia kwenye WHO Class 1B, kundi la dawa zinazotambuliwa kimataifa kuwa ni hatarishi sana (Highly hazardous pesticides – HHPs) zinazoweza kusababisha sumu kali au kifo hata kwa kiwango kidogo cha matumizi.
Hapa ndipo viuatilifu vyote vyenye viambata vya Dichlorvos vinapoangukia. Mifano mizuri ni Roach 500EC na Bachlorvos 500EC. Dawa hizi zimekuwa chanzo cha ajali nyingi za sumu mashambani, hasa kwa wakulima wadogo wasiokuwa na vifaa kamili vya kujikinga. Rejea jedwali namba 1 kwa mifano zaidi, lipo mwishoni.
2. Kupigwa marufuku kwa Paraquat, Paraquat Dichloride, Acephate na Dimethoate
Hapa ndipo kwenye kelele nyingi, hasa kwa Paraquat. Ni nani asiyeijua ‘’choma’’ au ‘’babua’’? Karibu kila mkulima anaijua paraquat kwa majina hayo kutokana na uwezo wake wa kubabua, kuchoma na kuua kabisa magugu ya aina zote kwa haraka sana.
Ukweli mchungu ni kuwa ‘’Paraquat ilikuwa ni rasihi kuitumia; inafanya kazi kwa haraka na kwa uhakika’’, lakini pia:
- Inasababisha vifo vya haraka ikimezwa hata kwa kiasi kidogo
- Ina historia ndefu ya ajali za sumu mashambani
- Inahusishwa na madhara ya kudumu ya mfumo wa fahamu
Hebu niambie, ni nani angependa kuendelea kutumia viuatilifu hatarishi kama hivi vinavyosababisha madhara ya kudumu au hata vifo kwa binadamu? Nieleze kwenye comment.
Kwa upande mwingine, viuatilifu vyote vyenye viambata vya Acephate na Dimethoate navyo vimeondolewa na kupigwa marufuku kutokana na ushahidi wa kisayansi unaoviunganisha na saratani, uharibifu wa ini, figo na mfumo wa homoni. Rejea jedwali namba 2 lililopo mwishoni kwa mifano halisi ya viuatilifu. Kama ulikuwa hujui, sasa hakuna kisingizio tena.
3. Viuatilifu 675 ambavyo usajili wake haukuhuishwa kwa zaidi ya Miaka 10
Viuatilifu hivi havikuondolewa kwa sababu vyote ni sumu kali, bali kwa sababu usalama wake haukuthibitishwa upya kwa viwango vya sasa. Lakini pia kutohuishwa kwa usajili kwa kipindi chote hicho kunadhihirisha mmiliki kutokuwa na uhitaji wa Kiuatilifu husika. Rejea jedwali namba 3 (lipo mwishoni) kuona orodha ya viuatilifu hivi.
Nanukuu…
Mamlaka inapenda kuutaarifu Umma kuwa kuanzia tarehe ya taarifa hii;
Taarifa rasmi ya TPHPA
1) Hakutakuwa na ruhusa ya kuingiza nchini bidhaa za Viuatilifu vyenye viambata tendaji vilivyotajwa.
2) Usajili wa Viuatilifu vyenye viambata amilifu vilivyotajwa katika vipengele vya 1 na 2 hapo juu hautakubaliwa.
Wafanyabiashara wote walio na akiba ya bidhaa hizo nchini wanaarifiwa kumaliza akiba hiyo ndani ya kipindi kisichozidi miaka miwili.
Kupigwa marufuku kwa viuatilifu hivi kuna athari gani kwa mkulima?
Hili ni eneo ambalo lazima lisemwe wazi, bila kupaka rangi. Kuondolewa na kupigwa marufuku viuatilifu hivi kutaathiri moja kwa moja kilimo chetu wakulima. Sasa, hizi hapa ni athari kwa wakulima za kuondolewa kwa viuatilifu hivi sokoni;
Athari za muda mfupi
- Hakutakuwa tena na zile dawa ulizozizoea kama Paraquat, Mission, Bayleton 25 WP, Innovex 360SC, Rustall 375 EC, Linkonil 500SC, Falconil Super 72% SC na Banko Plus.
- Kutakuwa na dawa mbadala ambazo zinaweza kuwa ghari, zisipatikane kwa urahisi mwanzoni, au kuhitaji maarifa zaidi kuzitumia.
- Utalazimika kujifunza upya mbinu za udhibiti wa wadudu na magonjwa bila kutegemea viuatilifu pekee.
Athari (faida) za muda mrefu ambazo ni kubwa zaidi
- Kulinda afya ya mkulima na wafanyakazi shambani kunakoendana na kupungua kwa magonjwa yasiyoeleweka yanayotokana na kemikali.
- Uhakika wa mazao kuwa salama kwa walaji wa mwisho
- Kufunguka kwa masoko ya kimataifa yanayozingatia afya za walaji na usalama wa chakula.
Kwa ujumla huu ni msukumo wa lazima kwa wakulima kuelekea matumizi ya mbinu shirikishi za kudhibiti visumbufu (Integrated Pest Management – IPM) na matumizi ya dawa kama suluhisho la mwisho, na sio la kwanza kama ilivyo kwa wengi. Ili viuatilifu viweze kutumika kwa tija bila kuleta madhara yoyote kwa wakulima, mazingira na walaji, fuata mbinu za matumizi sahihi na salama za viuatilifu.
Marufuku kwa viuatilifu hatarishi ina maana gani kwa wauza pembejeo?
Kwa wauza pembejeo, huu ni wakati wa kujitathmini. Licha ya TPHPA kutoa muda wa mpito usiozidi miaka miwili kwa wauzaji kumaliza bidhaa walizonazo, waagizaji, wasambazaji na wauzaji wa pembejeo za kilimo wanapaswa kutambua kuwa;
- Biashara ya pembejeo si biashara ya kuuza sumu tu, muuzaji wa pembejeo anatakiwa awe mshauri wa kilimo pia.
- Uuzaji wa viuatilifu vilivyopigwa marufuku ni kosa la jinai.
- Uelewa wa mikataba ya kimataifa pamoja na usalama na sheria za viuatilifu si hiari tena.
Je, kuondolewa kwa viuatilifu hatarishi kunapeleka ujumbe gani kwa jamii ya kimataifa?
Hatua hii pia ina ujumbe mzito nje ya mipaka ya Tanzania. Nchi yetu ni mwanachama wa mikataba mikuu ya kimataifa inayodhibiti matumizi ya kemikali hatarishi, ikiwemo:
- Stockholm Convention – kudhibiti kemikali zinazodumu muda mrefu kwenye mazingira
- Rotterdam Convention – kuhakikisha kemikali hatarishi haziingii sokoni bila taarifa na ridhaa
- Montreal Protocol – kuimarisha tahadhari dhidi ya kemikali zenye madhara ya muda mrefu
- International Plant Protection Convention (IPPC) – kulinda afya ya mimea bila kuhatarisha biashara ya kimataifa
Uamuzi huu wa Serikali ya Tanzania kupitia TPHPA ni utekelezaji wa moja kwa moja wa wajibu wa Tanzania katika mikataba hii. Kwa lugha rahisi: Tanzania inasema wazi kuwa haiwezi kuwa dampo la kemikali ambazo dunia imezikataa.
Kwa soko la dunia, huu ni ujumbe wa kujiamini unaomaanisha ‘’mazao ya Tanzania yanazalishwa chini ya mifumo inayoheshimu afya na mazingira.’’ Hii itaongeza imani ya wanunuzi wa kimataifa kwenye mazao ya Tanzania.
Maswali yanayoulizwa mara nyingi kuhusu kupigwa marufuku kwa viuatilifu hatarishi Tanzania
Kwa nini TPHPA imeamua kupiga marufuku viuatilifu hatarishi Tanzania?
TPHPA imeamua kupiga marufuku viuatilifu hivi ili kulinda afya ya binadamu, wanyama na mazingira. Tathmini imebaini kuwa baadhi ya viuatilifu vilivyokuwa sokoni vina madhara makubwa kiafya, vikiwemo kusababisha saratani, kuharibu mfumo wa uzazi na kusababisha mabadiliko ya vinasaba. Aidha, bidhaa 675 zimeondolewa kwa sababu usajili wake haukuhuishwa kwa zaidi ya miaka kumi, hali inayokiuka matakwa ya kisheria na usalama wa kisayansi.
Ni viuatilifu gani vilivyopigwa marufuku kabisa Tanzania kuanzia 2026?
Kuanzia Januari 2026, viuatilifu vyote vyenye viambata vya Paraquat, Paraquat dichloride, Acephate na Dimethoate vimepigwa marufuku kabisa Tanzania. Mbali na hivyo, bidhaa 130 zenye viambata vilivyoainishwa kama Highly Hazardous Pesticides (HHPs) kwa mujibu wa vigezo vya FAO/WHO pia zimeondolewa sokoni.
Je, nifanye nini ikiwa bado nina akiba ya viuatilifu vilivyopigwa marufuku shambani au dukani?
TPHPA imetoa kipindi cha mpito cha hadi miaka miwili kwa wafanyabiashara na wakulima waliokuwa tayari na akiba ya bidhaa hizo, ili kuzimaliza kwa kufuata masharti yaliyowekwa. Hata hivyo, kuanzia tarehe 07 Januari 2026, ni marufuku kabisa kuingiza nchini, kusajili au kusambaza bidhaa mpya zenye viambata vilivyopigwa marufuku.
Ni madhara gani ya kiafya yanayohusishwa na viuatilifu hivi hatarishi?
Viuatilifu vilivyopigwa marufuku vimehusishwa na madhara makubwa ya kiafya kama vile saratani, uharibifu wa mfumo wa uzazi, kuathiri homoni, na mabadiliko ya vinasaba. Kwa mfano, Paraquat imehusishwa na visa vingi vya vifo vya sumu, huku Dimethoate ikitajwa kusababisha uharibifu wa ini, figo, mfumo wa tezi na mfumo wa neva.
Ninaweza kupata wapi orodha kamili ya viuatilifu vilivyopigwa marufuku Tanzania?
Orodha kamili ya viuatilifu vilivyopigwa marufuku, ikijumuisha bidhaa 130 za HHPs, Paraquat na bidhaa zake, pamoja na bidhaa 675 ambazo usajili wake haujahuishwa kwa zaidi ya miaka 10 sasa, inapatikana kwenye tovuti ya Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA). Kwa urahisi, tumekuwekea link zake zote mwishoni mwa makala hii.
Hitimisho
Kwa kumalizia; Kuondolewa kwa viuatilifu hatarishi si ajali ya kisera. Ni matokeo ya kisayansi, kuheshimu mikataba ya kimataifa na kuthamini afya ya mkulima kama mimi na wewe. Na huu si mwisho wa kilimo, bali ni mwanzo wa kilimo kinacholinda afya ya mkulima na wafanyakazi shambani, mazingira, walaji wa mwisho na kilimo kinachokubalika kitaifa na kimataifa.
Usalama wa shamba lako na afya yako huanza na wewe. Je, dawa unazotumia bado zinaruhusiwa? Hakiki orodha rasmi ya TPHPA kabla ya msimu ujao wa kilimo. Tumekuwekea hapa orodha kamili ya viuatilifu vilivyopigwa marufuku;

How can I join in MogriCulture